Ibwera ni kata iliyoko katika Tarafa ya Katerero, Wilaya ya Bukoba Vijijini. Sehemu hiyo si kame sana ukilinganisha na sehemu nyingine zenye ukame hapa nchini. Ina mito ya kutosha na imezungukwa na maziwa mengi madogomadogo ambayo yanaipa sifa ya kutoonekana yenye ukame.

Kata hiyo imezungukwa na mto mmoja mkubwa wenye sifa ya kimataifa, mto ambao unatengeneza Bonde la Mto Ngono. Hilo ni bonde kubwa ambalo hata mtu akiwa nchini Rwanda au Burundi likitajwa mara moja anakwambia liliko.

Kwa upande mwingine, kata hiyo imepakana na Ziwa Ikimba, ambalo ni la tatu kwa ukubwa katika Mkoa wa Kagera, mkoa ambao umejaliwa kuwa na hifadhi kubwa ya maji yanayoongozwa na Ziwa Victoria ambalo wakazi wa maeneo ya Bukoba huliita Ziwa Rweru.

Lakini kutokana sehemu kubwa ya Kata ya Ibwera kutokuwa karibu na mito kwa kila kijiji, wakazi wa maeneo hayo wamezoea kuyafuata maji ya matumizi ya nyumbani kwa mwendo mrefu kila siku, kitu ambacho kimetokea kuwa adha katika maeneo yao.

Kutokana na sababu hiyo ulifanyika mpango wa kuwaletea maji karibu na maeneo yao wakazi wa Ibwera, kusudi badala ya kuyafuata maji katika umbali wa kilometa nne kwa kila mwananchi, kwenda na kurudi au hata zaidi, wananchi wanaweza kuyapata maji katika umbali usiofikia nusu kilometa.

Tangu wazo hilo la mradi wa maji limeanza kushughulikiwa ndani ya Kata ya Ibwera ni zaidi ya miaka mitatu, lakini umeenda kwa mwendo wa kusuasua, mpaka alipokuja mkuu wa Wilaya ya Bukoba kuuzindua mwishoni mwa mwaka jana, hakuridhika nao na kuacha maelekezo kuwa uwe umekamilika kufikia Januari 4, mwaka huu.

Tarehe hiyo ilipofika mkuu wa Wilaya ya Bukoba akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Juma Aweso, ndipo wakafika na kuuzindua rasmi mradi huo.

Lakini jambo la kushangaza ambalo wananchi wanalitilia shaka ni kwamba maji yalionekana tu siku ya uzinduzi, ambapo Naibu Waziri Aweso alishuhudia mwenyewe maji yakichotwa kutoka kwenye bomba, huku naibu waziri huyo akimtwisha maji mama mmoja siku ya uzinduzi kama ishara ya kukomesha tatizo la kufuata maji umbali mrefu.

Lakini baada ya siku hiyo hakuna maji yanayoonekana sehemu nyingine katika maeneo yote ya kitongoji cha Ibwera yalikofungwa mabomba ya kuchotea maji.

Swali linaloulizwa na wakazi wa Ibwera ni je, mradi mzima wa maji ulitegemewa kuonyesha maji siku ya uzinduzi tu mbele ya naibu waziri? Maana baada ya Aweso kuondoka tatizo la maji limerudi palepale kama lilivyokuwa kabla ya uzinduzi wa mradi.

Kitu alichokishuhudia mwandishi wa makala hii ni chanzo cha maji hayo katika sehemu inayoitwa Mujumo, ambako alipelekwa na Diwani wa Kata hiyo ya Ibwera, Ahmed Kiobya,  kwenda kujionea mwenyewe hali halisi.

Eneo hilo linaonekana lilivyo safi sana kulinganisha na maeneo mengine mengi ambayo mwandishi huyu ameyatembelea kikiwemo chanzo cha maji yaingiayo jijini Dar es Salaam, Ruvu Juu.

Ila wananchi wa Ibwera wanasema wao wanachokijali si uzuri wa chanzo cha maji tu, isipokuwa ni maji yenyewe yatiririke kwenye mabomba yaliyowekwa katika maeneo yao.

Wananchi wa Ibwera wamebaki kuyaangalia tu mabomba yasiyotoa maji huku wao wakihangaika kutafuta maji ya kutumia wakati wakikipongeza chanzo cha maji yao, Mujumo, na kukiona kama kitu cha baraka kwao.

Ni kweli kwamba maeneo yao yamewekwa mabomba ambayo kila mahali pa kukingia maji pamezungushiwa seng’enge na kutiwa kufuri ili kuzuia watu wasiokuwa na ustaarabu wasiweze kuyamwaga maji. Ila kuna sehemu nyingine wanakodai kuwa tangu mradi huo uzinduliwe bado hawajayaona maji yakitoka katika mabomba yao.

Kwa maelezo yaliyopo ni kwamba mradi huo umegharimu zaidi ya Sh milioni 500. Wakati fedha hizo zikionekana kuwa nyingi na zilikusudiwa kumaliza tatizo la maji katika Kata ya Ibwera, bado maji yameendelea kuwa ndoto isiyojulikana kukamilika kwake.