Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki ( EACOP ) umeanzisha mpango wa kuwasaidia waguswa wa mradi huo wanaoishi pembezoni mwa miji, maarufu kama watu wa asili katika sekta ya kilimo na ufugaji kwa kuwapatia pembejeo za kilimo na mbegu bora za mifugo ili kuwaendeleza kiuchumia.
Utaratibu huu ni mbali na ule wa fidia za pesa, nyumba pamoja na vyakula (food basket) walivyokuwa wanapewa kwa muda wa mwaka mmoja kupitia mpango wa kuwasaidia kurejesha makazi yao (Livelihood Restoration) baada ya maeneo yao kupitiwa na mradi huu.
Akiongea wakati wa kikao cha robo ya nne kati ya EACOP na watu hao kutoka jamii za Masai, Wa-akie, Wa-Bargaig pamoja na Wataturu, Fatuma Mssumi, Kiongozi wa Kitengo cha Mahusiano wa EACOP kwa upande wa Tanzania amesema kuwa wagoswa ambao ardhi zao zimechukuliwa na mradi ndio wanaofaidika na utaratibu huu.
Lakini elimu itakayotolewa kuhusu kilimo na ufugaji pia itawanufaisha majirani wanaopakana nao hata kama sio waguswa wa mradi huu katika kusaidia jamii zao.
“Tumekuwa tukiwasapoti watu wa asili katika maeneo tofauti tofauti ili kuboresha maisha yao kwa sababu EACOP inafuata taratibu za kimataifa na kuheshimu haki za binadamu,”
“Baada ya waguswa kulipwa fidia mbalimbali zikiwemo fidia za nyumba bora za makazi, sasa tunaboresha maisha yao kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali kupitia kilimo na ufugaji kupitia maofisa ugani,” amesema Bi Mssumi.
Amesema kwa upande wa mifugo, wale wanaofuga watapewa mbegu nzuri za kisasa zinazohimili magonjwa na wale wanaojihusisha na kilimo pia watapewa mbegu bora ili kupata mazao bora.
“Tutawapatia wataalamu wa kilimo (maofisa ugani) ambapo waguswa wataonyesha ardhi wanazotaka kulimiwa na wataalamu pamoja na mambo mengine, watapima afya ya udongo, kuwapa elimu ya kutayarisha mashamba na kuwashauri aina gani nzuri ya mazao kwa ajili ya kilimo , kikiwemo kilimo mseto yanayoendana na maeneo yao,” amesema Bi. Msummi.
Amesema pia elimu ya ujasiriamali kwa waguswa hao tayari imeanza kutolewa kwa waguswa wa mkoa wa Kagera na utaratibu huu utafuata katika mikoa mingine ambapo mradi huu umepita.
Mmoja wa waguswa wa mpango huu, Yona Shing’adeda Gidabukushida , Kiongozi wa Mila wa Watatoga kutoka Hanang, mkoa wa Manyara amesema tayari kuna baadhi ya waguswa wameanza kufaidika na mpango huu katika maeneo yao.
Amesema wapo waliosaidiwa kwa upande wa kilimo na kupata mavuno mengi kwa ushauri wa wataalamu.
Anasema pia walifanya zoezi la kupandikiza mbegu bora za mifugo kwa kutumia madume ya ng’ombe, lakini zoezi hili halikuwa na mafanikio makubwa na badala yake wameomba kutumia mbegu zinazowekwa katika chupa.
Akitoa elimu kwa jamii za waguswa wakati wa mkutano huo, Shukuru Tuke Lemoringata, ambaye ni Afisa Mifgo na Katibu wa viongozi wa kimila wa Kimasai katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara amewataka waguswa hao ambao wengi wao ni wa jamii za kifugaji kuzingatia ufugaji bora wa kisasa, badala ya kuwa na mifugo mingi bila tija.
Pia amewataka kuzingatia taratibu za chanjo za mifugo yao, ili kuepukana na magonjwa mbalimbali inayoathiri mifugo yao.
Pia Bw. Lemoringata ameushukuru mradi wa EACOP kwa kuendelea kuwasapoti waguswa wa mradi huo na kuwasaidia katika maeneo mbalimbali ya kijamii.
Lakini pia ameusifu mradi huo kwa kuendelea kuwashirikisha watu hao wa jamii za pembezoni katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo kupitia mikutano inayofanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu, ili kuwapa taarifa za maendeleo ya mradi na kujadiliana nao kwa pamoja juu ya fursa au changamoto yoyote inayoweza kujitokeza katika maeneo yao wakati mradi huu unaendelea kutekelezwa.
Pamoja na mambo mengine, jamii hiyo ya watu wa pembezoni waliusifu mradi huo kwa kuendelea kuheshimu mila, desturi na tamaduni zao wakati mradi huu ukitekelezwa.
Kwa mujibu wa Dkt. Elifuraha Laltaika ambaye ni Mshauri wa mradi wa EACOP kwa watu waguswa wanaoishi pembezoni mwa mji, mradi huu umekuwa ukikutana na jamii hizo mara moja kila baada ya miezi mitatu kujadili maendeleo ya mradi na kuangalia maeneo ambayo wanaweza kushirikiana.
Mradi wa EACOP ambao unapita katika mikoa nane hapa nchini, una urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi rasi ya Chongoleani mkoani Tanga.
Wanahisa ni TotalEnergies yenye asilimia 62, wakati Mashirika ya Maendeleo ya mafuta (TPDC- Tanzania na (UPDC kwa upande wa Uganda ) yana miliki asilimia 15 kila moja na shirika la mafuta la China (CNOOC) linamiliki asilimia nane tu katika mradi huu.