Na Daniel Limbe,JamhuriMedia, Biharamulo
Katika kukabiliana na adha kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera,serikali imetenga zaidi ya bilioni 77 kwaajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa usambazaji maji kutoka ziwa Viktoria.
Mradi huo unatazamiwa kuwanufaisha watu takribani watu zaidi ya 27,432 ambao wanaishi maeneo ya mji wa Biharamulo na vijiji jirani hatua itakayosaidia kuondokana na kero ya kugombea maji na wengine kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Biharamulo mjini(Buwsa) Mhandisi Siraji Basiga, ameiambia Jamhuri Digital kuwa mradi huo utatekelezwa hivi karibuni na kwamba maji hayo yatatoka eneo la wilaya ya Chato mkoani Geita, baada ya taratibu za kiutendaji kukamilika na kwamba hatua hiyo itakuwa ndiyo mwarobaini wa uhaba wa maji kwa wananchi hao.
Takribani kata tano zikiwemo zilizo nje ya Mamlaka ya mji wa Biharamulo ambako bomba kubwa za maji zitapita nazo zitanufaika na mradi huo ikiwemo ajira za muda mfupi kwa jamii.
“Katika kukabiliana na kumaliza changamoto ya maji kwenye mji wa Biharamulo na majirani zake,mradi mkubwa wa maji usanifu wake umefanyika chini ya Mhandisi mshauri “Don Consultant” kupitia Wizara ya maji ambapo tayari upembuzi na usanifu wa mradi huo umekamilika” amesema Basiga.
Aidha katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, amesema Mamlaka hiyo inaendelea kuwaelimisha wananchi kuacha kulima kwenye vyanzo vya asili vya maji ndani ya mita 60 kama sheria inavyoelekeza.
Mbali na hilo Mamlaka imewataka wananchi kuwa sehemu ya ulinzi wa miundombinu ya maji ili iweze kudumu na kuwanufaisha wananchi wengi kwa muda mrefu zaidi badala ya wao kugeuka wahujumu kwa kuipora na kusababisha adha hiyo kuendelea.
Baadhi ya wananchi mjini Biharamulo wemesema,mpango huo utasaidia kukuza vipato vyao kutokana na sasa kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kuzalisha mali.
Aidha wameitaka serikali kupanua mtandao wa upatikaji wa maji hadi vijijini kwa madai kuwa bado yapo maeneo ambapo wananchi wanatumia maji ya kwenye madimbwi kwa kushirikiana na wanyama hali inayosababisha kutumia fedha nyingi kujitibia magonjwa yatokanayo na maji machafu.
Hata hivyo,Diwani wa Kata ya Biharamulo mjini,David Mwenenkundwa,amesema hali ya upatikanaji wa maji kwenye kata yake angalau inaridhisha ukilinganisha na hali ilivyokuwa awali ambapo maji yalikuwa yakipatikana mara mbili tu wiki.
“Kwa kweli hali ya sasa siyo mbaya sana angalau wananchi wanapata maji kiasi frani ukilinganisha na miaka ya nyuma,nawapongeza sana Mamlaka ya maji mjini Biharamulo na ninawaomba waongeze juhudi ili kuondoa kabisa adha iliyopo” amesema Mwenenkundwa.
Kwa upande wake,msimamizi msaidizi wa mradi wa maji Biharamulo mjini,Edmund Balongo,amesema kiasi kinachopaswa kwa sasa ili kukidhi haja ya maji mjini hapo ni wastani wa mita za ujazo 1,920 kwa siku tofauti na kinachozalishwa cha mita za ujazo 1440 tu.
Aidha Mamlaka hiyo imekuwa ikitegemea kuvuna maji kupitia vyanzo vyake vikuu sita ikiwemo kile cha Kuziba,Runyinya,Kagango,Nyakahura ambapo kuna Bwawa na visima,Bisibo ambapo kuna kisima, na Nyarukongogo.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu,ameipongeza serikali kwa hatua hiyo na kwamba itakuwa mkombozi kwa wananchi wake, kutokana na awali kuwepo kwa baadhi ya malalamiko ya uhaba wa maji ambayo yamekuwa yakipatikana kwa takribani saa 12 pekee.