Soko la muziki wa Tanzania linakua siku hadi siku. Dalili za kukua kwa muziki zinadhihirishwa na ongezeko la wasanii wanaoibuka mara kwa mara. Hali hii imewafanya wasanii wakongwe na waliopata kuwika katika muziki kwa kiasi kikubwa, kufikiria kujipanga upya ili kuendana na soko la kisasa.
Msanii maarufu wa muziki nchini, Lucas Mkenda ‘Mr. Nice’, amesema kuwa kwa sasa yuko mbioni kuhakikisha kwamba anatoka upya ili aendelee kukamata soko la muziki ndani na nje ya nchi kama ilivyokuwa awali.
Akizungumza na JAMHURI Dar es Salaam hivi karibuni, Mr Nice amesema kuwa muziki wa sasa unahitaji ushindani wa hali ya juu, hali ambayo amesema kuwa imemsababisha yeye kutulia na kufikiria kujipanga upya akiwa na lengo la kukamata soko la kisasa.
“Muziki wa sasa hivi unahitaji umakini zaidi kutokana na ushindani uliopo, kwa hiyo kukaa kwangu kimya si kwamba nimeacha kufanya muziki bali najipanga ili kuendana na wakati uliopo, kila siku mambo yanabadilika, muziki wa sasa huwezi kuulinganisha na ule wa miaka kumi iliyopita,” amesema.
Amesema kwamba kwa sasa anachofanya ni kutunga nyimbo zenye hadhi na zinazozingatia utamaduni na maadili ya Kitanzania. “Ninachoamini sasa hivi ni kwamba kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa baadhi ya wasanii, hii inakwenda kinyume na mila na desturi zetu kama Watanzania,” alisema Mr Nice.
Mr Nice anaamini kuwa muziki wake kwa sasa unakubalika kutokana na jinsi wapenzi wa muziki wake walivyozipokea nyimbo zake mpya, alizotoa hivi karibuni na kufanikiwa kufanya maonesho kadhaa hapa nchini.
“Kwa wale wanaofuatilia muziki wangu watakubaliana na mimi kuwa nyimbo zangu kama Bwana Shamba, Tabia Gani na ule wa Akina Mama ambao umetoka hivi karibuni jinsi zilivyokubalika, hii inanipa moyo kwamba bado nakubalika katika fani na kuna uwezekano mkubwa kuendelea kulikamata soko kutokana na ubunifu wangu,” amesema.
Dalili za msanii huyo kurejea kwa kishindo zilianza kuonekana tangu mwaka jana, alipoanza kufanya maonesho mbalimbali katika mikoa kadhaa hapa nchini. Maonesho yake yalipokewa kwa kishindo na washabiki wa muziki.
Mr Nice anasema kuwa kitendo hicho kilimtia moyo kuona kuwa mbali ya kuimba nyimbo zake mpya, lakini bado kuna baadhi ya mashabiki wake ambao walionekana kupenda hata nyimbo zake za zamani kama vile Fagilia, Kuku Kapanda Baiskeli na nyinginezo.
Kuhusu ujio wa vijana wengi katika fani, Mr Nice amesema kuwa hakumtishii amani na kwamba kila mwanamuziki ana nyota yake kutokana na muziki anaoufanya.
“Mimi nina wapenzi wangu wanaopenda ladha ya muziki wangu, kwa hiyo hata akiibuka mwanamuziki mwingine atakuwa na wapenzi wake kutokana na ladha ya muziki wake, huu ni ushindani tu, lakini mwisho wa siku ubora utaendelea kuwa palepale,” amesema