Weledi wa Sayansi ya Siasa wanaitambulisha siasa kuwa ni mfumo wa maridhiano unaohusisha kikundi cha watu walioafikiana kuwa na uamuzi wa pamoja (politics involves the making of a common decision for a group of people).
 Kadhalika, uamuzi wa aina hiyo unahusisha wanachama wote wa kikundi hicho bila kubaguana. Na kwamba ili kikundi cha siasa kiweze kujitosheleza kiuamuzi, ni lazima kitayarishe miongozo kinachowaongoza wanachama katika kufikia uamuzi ulioafikiwa kwa pamoja. Miongozo hiyo ni kama vile katiba, kanuni, sheria na taratibu.


Kwa tafsiri ya hapo juu, tunapata picha kwamba kikundi cha watu waliokubaliana kuanzisha chama cha siasa (a political party), kamwe haruhusiwi mtu kuongea mambo yanayohusu kikundi kama mtu binafsi bali kuzungumzia kikundi kwa niaba ya wanachama wengine.
Hivyo, masuala yanayoashiria mambo ya kibinafsi hayana nafasi katika chama chochote kinachofuata misingi na maadili ya siasa. Mojawapo ya maadili yanayohusu siasa ni kama vile kutokuwa mnafiki, mchochezi, mwongo, mbinafsi n.k.


Kawaida, malengo ya vyama vyote vya siasa hayatofautiani. Lengo kubwa ya chama cha siasa ni kushiriki kwenye chaguzi, kushinda Serikali za Mitaa na Serikali Kuu, kushika dola na kuunda Serikali. Hakuna chama cha siasa ambacho kina malengo tofauti na hayo niliyoyaainisha hapo juu. Vinginevyo kiwe ni chama cha msimu au chama pandikizi.


Mara nyingi vyama vya aina hii ndivyo vinavyogeuzwa kuwa vikundi vya kigaidi. Kazi kubwa ya vyama vya aina hiki ni kuhakikisha Serikali haitawaliki. Viko tayari kuiangusha Serikali lakini vyenyewe visiunde Serikali mpya.
Nimelazimika kuanza na dibaji ya mada hii kwa kuangalia nafasi za vyama vya siasa na malengo yake ili kuipa nguvu hoja ninayotazamia kuizungumzia katika makala hii.


Nijuavyo, kwa muhtasari vyama vyote kutoka kambi za upinzani duniani hasimu wao mkuu ni chama tawala. Kadhalika (chama tawala nacho kikishindwa kwenye uchaguzi, nacho kinachukua nafasi ya kuwa chama cha upinzani. Hivyo, hasimu wake mkuu anakuwa chama kipya kilichoshinda.
Inapotokea vyama vya upinzani vikaanza kuwa mahasimu vyenyewe kwa vyenyewe, basi hapo itakuwa imeingizwa chuki binafsi. Na kwamba kitendo hicho kinatafsiriwa kama viongozi wa vyama hivyo kutokomaa kisiasa.


Ni hivi karibuni, wadau wengi walishindwa kuamini masikio na macho yao pale waliposhuhudia mafahali wawili wanaotoka kambi moja ya upinzani, wakitunishiana msuli mithili ya mahasimu wanaotoka pande mbili tofauti.
Mchezo huo wa kutia aibu, ulianzia pale Naibu Katibu Mkuu (Bara) Chadema, John Mnyika, alipoanza kumshambulia Zito Kabwe, kiongozi mkuu (ACT-Wazalendo) kwenye hotuba aliyotoa katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.


Mnyika alinukuliwa akirusha mawe kwenye kambi ya Zitto akiwakataza wananchi kutohudhuria mkutano wa Zitto, ambaye naye alikuwa mbioni kuhutubia kwenye viwanja hivyo siku iliyofuata. Mnyika alidai kuwa Zitto ni msaliti wa wapinzani. Alikwenda mbali zaidi na kusema Chadema hawako tayari ACT-Wazalendo kujiunga na Ukawa.
Aidha, alisema Chadema haiwezi kuikaribisha ACT-Wazalendo kwa sababu ya kukosa imani yao akifikia hatua ya kuwaita wasaliti. Hapa ndipo ninapofikia kuchanganyikiwa, najihoji; Chadema kabla hawajaanzisha chama hicho walikuwa ni wanachama wa chama gani cha siasa!
Na kwamba inakuaje wamwite Zitto msaliti na kufika hatua ya kutoiamini ACT-Wazalendo wakati na wao pia walitoka kwenye chama kingine cha CCM? Nani kati yao — Zitto (ACT-Wazalendo) na Mnyika (Chadema) — ni msaliti aliyekubuhu!
Hata hivyo, katika majibu ya maelezo hayo ya Mnyika, Zitto anasema; “Mwanzo walipotufukuza walitwambia tukatafute vyama vingine, hilo likafanyika, tulipopata vyama vya kufanyia siasa, wakasema vipo kwa ajili ya kugawa upinzani.


“Tukasema tupo tayari kuunganisha nguvu ya pamoja kwa ajili ya kuiondoa CCM, wenzetu pia hili hawalitaki. Sasa ni wajibu wenu (wananchi) kutambua watu gani hawataki kuiondoa CCM.
“Wananchi watambue tuna nia ya dhati lakini wenzetu wanaweka ugomvi binafsi mbele ya maslahi ya Taifa. Sisi ACT-Wazalendo bado tupo tayari kushirikiana kwa mujibu wa msingi,” alimalizia Zitto.


Awali, katika dibaji ya mada hii nilikumbushia maana ya ‘siasa’, pia nilikumbushia maana ya chama hasimu na kwamba inapotokea vyama vya upinzani vikaanza kuwa mahasimu vyenyewe kwa vyenyewe, basi hiyo inaitwa chuki binafsi.
Aidha, nilisema siasa ni mfumo wa maridhiano yanayohusisha kikundi cha watu waliokubaliana kuwa na uamuzi wa pamoja. Swali la kujiuliza, kwa kuwa viongozi wa Ukawa walikubaliana kwa pamoja kuunda nguvu kwa makusudi mazima ya kuiong’oa CCM madarakani, kulikoni Chadema wajichukulie madaraka ya kuikatalia ACT-Wazalendo kujiunga nao?


Madaraka hayo ya kuikatalia ACT-Wazalendo isiungane na Ukawa wameyapata wapi? Je, ni lini vyama vingine viliridhia kukasimu madaraka hayo kwa Chadema? Nani alimpa Mnyika madaraka ya kuzungumzia mambo yanayohusu vyama vinavyounda Ukawa katika suala nyeti kama hilo?
Kama nilivyotangulia kusema, ili kikundi cha siasa kiweze kujitosheleza kiuamuzi, lazima kitayarishe miongozo kama vile katiba, kanuni, sheria alimradi kuwazuia viongozi wa aina yake Mnyika wanaoropoka hovyo.


Ni aibu kwa vyama vya upinzani kuanza kushambuliana vyenyewe kwa vyenyewe ilhali vikiwa na lengo moja ya kukiong’oa madarakani chama tawala.
Wadau wengi wameishutumu Chadema wakihoji uhalali wao wa kujifanya kama wao ndiyo “Alfa na Omega”, kwamba kinachotakiwa kiamuliwe kutoka kambi ya upinzani basi ni lazima wao ndiyo wa kukibariki. Huo ni udikteta na ubinafsi uliokithiri.


Zitto alishajiuzulu na kuhamia chama kingine. Kwanini Chadema waendelee kumfuatilia huko? Wameshindwa kutafuna mfupa wa CCM sasa wanaelekeza nguvu zao kutaka kutafuna mfupa mdogo wa ACT-Wazalendo. Chadema wasiote ndoto za Ali Nacha ya kuiondoa CCM madarakani wakiwa na mawazo finyu kama za Mnyika.
Mnyika anapojinasibu kwa kumwita Zitto msaliti wakati yeye (Zitto) alishakihama chama hicho, anakusudia kuleta picha gani katika kambi ya upinzani? Kweli wahenga walinena ‘nyani haoni kundule’. Kama ni usaliti, basi viongozi wote kutoka kambi ya upinzani ni wasaliti.
Viongozi wote wa Chadema walizaliwa kutoka tumbo la CCM. Watwambie ni lini walirudisha kadi za CCM hadharani. Huo usaliti wanauona wa Zitto wenyewe hawajioni?


Chadema wasitarajie kupata mteremko wa kuiong’oa CCM madarakani kwa staili hii ya kumsakama Zitto. Wakitaka kushiriki wakubali yaishe, kama ni usaliti basi kambi nzima ya upinzani ni wasaliti.
Huko nyuma, Chadema waliiita CUF CCM-B, mashoga. Kama hiyo haitoshi, waliwaita NCCR-Mageuzi pandikizi la CCM na (Mbatia) Mbunge wa Viti Maalum.


Leo wanasema Zitto Kabwe ni msaliti na hawana imani na ACT-Wazalendo, je, wao Chadema walitoka kwenye tumbo lipi? Tumbo la malaika au tumbo la CCM? Mwasisi wa Chadema, Mzee Edwin Mtei alikuwa nani ndani ya CCM?
Chadema wakitaka kushika dola sharti wakubali yaishe. Wamwache Zitto afanye siasa zake. Wote wametoka kwenye tumbo moja; uzao mmoja wa CCM.

Simu: 0713-399004 / 0767 399004
Email: [email protected]