Na Mwandishi wetu, JajhuriMedia, Simiyu

Waziri wa Kilimo Husein Bashe (mb) amewasili katika Jimbo la Kisesa na kukutana ana kwa ana na mbunge wa Jimbo hilo Luhaga Mpina.

Waziri Bashe amemshauri Mpina kuacha kufanya siasa katika zao la pamba kwani Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, inahitaji kuona fedha zinazotengwa zinanufaisha wakulima.

Waziri Bashe amewaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwa Serikali inarejesha kitalu cha mbegu kuwapatia ruzuku ya dawa za wadudu katika zao la mahindi na pembejeo na mbegu katika zao la pamba.

Naye Mkuu wa Mkoa Simiyu Kennan Kihongosi amemuhakikishia Waziri Bashe kuwa yeye ndiye mwenye dhamana na mkoa huo ametumwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuleta maendeleo hivyo hatovumilia kuona baadhi ya watu wanatumia siasa ili kukwamisha juhudi za maendeleo mkoani humo.

Hata hivyo Mpina amesema yuko tayari kuweka tofauti zake na Waziri Bashe pembeni na kuungana katika masuala ya maendeleo na shughuli za Serikali.

Waziri Bashe ametua jimboni humo katika mkutano na wananchi wa jimbo hilo wakati wa kufunga mashindano ya michezo mbalimbali ya Mwandoya.

Ametumia fursa hiyo kukutana na mbunge Mpina ambapo amemshauri kuacha siasa katika zao la pamba kwa maslahi ya wananchi.

“Rais Samia amefanya kazi kubwa katika kilimo hapa na mimi nataka nisisitize tuweke mambo mengine pembeni aache siasa na sitaki siasa katika zao la pamba, nafahamu zipo changamoto lakini tulipotoka sio tulipo sitakubali mtu arudishe nyuma jitihada hizi kwani wanaoteseka ni wananchi ,”amesema.

Aidha amekabidhi trekta 40 kwa jimbo hilo na kuwataka maafisa kilimo na ugani kuacha kukaa mjini na kuishi vijijini ili waweze kuwasaidia wakulima utaalamu na kufikia malengo ya Serikali ya kilimo chenye tija.

Amewashukuru wazee wa kimila kwa kumsimika kuwa mtemi wa jimbo hilo.

“Nami leo nimesimikwa kuwa mtemi wa Kisesa hivyo Mpina akinitambia pale bungeni kwa kuingia na fimbo ya uchifu nami nitaingia na yangu,”amesema.

Naye Mkuu wa mkoa huo Kennan Kihongosi amemuhakikishia Waziri Bashe kuwa yeye ndio mwenye dhamana na mkoa huo, hivyo hawezi kuvumilia watu wanaotafuta umaarufu katika siasa na kuingiza masuala ya maendeleo.

“Nimetumwa kazi na Rais Dk. Samia, Simiyu ni ya kwanza ama ya pili katika kuzalisha pamba hivyo kwa wananchi ni zao la kiuchumi sitaki wanasiasa watumie zao hilo kutafuta umaarufu shida zinazosemwa katika zao hilo si za kweli wananchi wa Kisesa msikubali kutumika,”amesema

Naye Mbunge Mpina ametumia fursa hiyo kumkaribisha Bashe Kisesa na kueleza kuwa wanazo tofauti zao hali iliyowafikisha hadi mahakamani lakini yupo tayari kushirikiana naye katika masuala ya utendaji wa serikali.