Lengo la kufikia uchumi wa kujitegemea imekuwa ni dhamira ya Tanzania kwa muda mrefu. Hatua mbalimbali za kimaendeleo zimekuwa zikichukuliwa ili kufikia azma hiyo.
Ili kufikia azma hiyo, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imebainisha malengo matatu ambayo ni kuwaletea wananchi maisha bora na mazuri; kudumisha uongozi bora na utawala wa sheria; na kujenga uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani.
Ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Serikali imeandaa mpango elekezi wa miaka 15 ambao umegawanywa katika mipango mitatu ya miaka mitano mitano. Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2011/12-2015/16 unafikia ukomo Juni 2016 na kutoa nafasi ya kuanza kwa awamu ya pili.
Mpango wa kwanza wa maendeleo umefanikiwa katika nyanja mbalimbali ikiwamo nishati, miundombinu, huduma za jamii, kilimo, maendeleo ya rasilimali watu pamoja na uendelezaji wa huduma za utalii, biashara na fedha.
Mpango wa pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano unatarajiwa kuanza 2016/17 hadi 2020/21. Mpango huo umejikita zaidi katika maendeleo ya uchumi wa viwanda na rasilimali watu.
Uchumi wa viwanda ilikuwa ahadi mojawapo ya Rais wa Awamu ya Tano, Mhe. Dkt. John Magufuli, aliyeahidi kufufua uchumi wa viwanda na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Ahadi hiyo imeonekana katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano uliowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao vya Bunge la Bajeti Aprili, 2016.
Dkt. Mpango anasema kiasi cha Sh trilioni 107 kinahitajika ama kitatumika kugharamia mpango na miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka 5 ijayo, sawa na wastani wa Sh trilioni 21.4 kila mwaka.
Anabainisha kuwa Serikali itachangia Sh trilioni 59, sawa na wastani wa trilioni 11.8 kila mwaka ili kufanikisha hilo. Sekta binafsi inatarajiwa kushiriki kikamilifu ili kufikia azma hiyo.
Dkt. Mpango anabainisha kuwa mpango huo umejikita zaidi katika mambo manne yaliyolenga katika kujenga uchumi wa viwanda, ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.
Mosi, mpango huo umelenga kukuza uchumi na kujenga msingi wa uchumi wa viwanda. Mpango huu utaleta mapinduzi ya kilimo ambayo yatachochea maendeleo ya watu na viwanda.
Hii ni fursa kwa wananchi na wawekezaji binafsi kuchangamkia sekta ya kilimo, ambayo pia imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa na kutoa ajira kwa wananchi wengi zaidi.
Pia sekta za viwanda, madini na utalii nazo zimeteuliwa kutokana na uwepo wa fursa za kipekee za rasilimali za uzalishaji na masoko ya bidhaa na uwezo wa bidhaa hizo kuhimili ushindani wa kibiashara.
Sekta hizi zote zitatoa mwanya kwa wananchi kuweza kupata ajira kuweza kujipatia kipato ili kuboresha maisha yao katika nyanja mbalimbali.
Pia zitatoa fursa kwa maendeleo ya miji na huduma nyingine za kijamii na kuchochea ukuaji wa biashara.
Pili, mpango umelenga kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu. Ili uchumi ukue vizuri, ni vema kwenda sambamba na maendeleo ya watu. Mpango huu umelenga kupanua fursa za upatikanaji wa elimu bora kwa watu wote itakayowezesha mwananchi kujiajiri au kuajiriwa.
Vilevile, umejikita katika kuimarisha afya za wananchi ikijumuisha huduma za matibabu, usalama wa chakula na upatikanaji wa viini lishe vya mwili, maji safi, mazingira safi ya kuishi na hifadhi ya jamii.
Tatu, Mpango umelenga kujenga mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji. Mpango umeazimia kuimarisha mifumo ya kisheria ili iwe rafiki katika kuvutia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme, miundombinu ya reli, barabara, bandari, usafiri wa anga na majini pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).
Nne, kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mpango. Hii inajumuisha kutanzua vikwazo vya utekelezaji na kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya mpango.
Aidha, eneo hili limeainisha marekebisho yanayopaswa kufanyika ya kisera, sheria na taratibu za kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa mpango.
Changamoto kubwa inayofanyiwa kazi na Serikali ni hali ya viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo utendaji kazi wake umekuwa wa kusuasua.
Taarifa iliyotolewa bungeni mjini Dodoma na Waziri mwenye dhamana ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, inasema kuwa kati ya viwanda 106 vilivyofanyiwa tathmini, viwanda 45 vinafanya kazi, 24 vinasuasua na 37 vimefungwa.
Viwanda vingine 35 ambavyo vimebaki, vitafanyiwa tathmini ili kujua hatima ya viwanda hivyo.
Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni, anapendekeza kuwa ni muhimu Serikali ikawekeza zaidi katika kuendeleza sekta ya kilimo, kwa kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea aina ya urea inayotokana na mabaki ya gesi itakayouzwa kwa bei nafuu.
Ili kuzalisha mbolea, unahitaji kuwa na phosphate, calcium na madini mengine yanapatikana hapa nchini isipokuwa nitrogen inayotoka nchi za Uarabuni na nchi za Scandinavia.
“Kwa kuwa tunazalisha gesi na imesafirishwa hadi Dar es salaam, kijengwe kiwanda cha kutengeneza nitrogen itakayotumika kwenye viwanda vya mbolea vitakavyozalisha mbolea itakayokidhi viwango na bei rafiki kwa wakulima,” alisisitiza Mhe. Jitu Soni.
Aidha, anashauri kuwa pembejeo za kilimo zinazozalishwa na kuuzwa hapa nchini zikiwamo mbegu, zisitozwe kodi kama ilivyo kwa pembejeo za kilimo zinazoingizwa nchini kutoka nchi za nje, jambo ambalo anasema litapunguza bei na litasisimua ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya kilimo.
Anapendekeza uwekezaji mkubwa ufanywe katika miundombinu ya reli ikiwamo ya Kati, reli ya kutoka Tanga, Kilimanjaro, Arusha hadi Uganda ambayo pamoja na kusafirisha abiria na mizigo yao, itumike pia kubeba shehena ya saruji na chokaa kwenda nchini humo.
Anasema kuwa ili mpango wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano uweze kufanikiwa, ni lazima sheria ya ununuzi ya mwaka 2014 ihuishwe, ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Serikali zinazopotea kutokana na kupandishwa kwa bei za bidhaa na huduma zinazohitajika na Serikali ikilinganishwa na bei ya soko.
Anabainisha kuwa sheria hiyo imekuwa kichaka cha kupoteza fedha za Serikali kutokana na vitendo vya rushwa na ufisadi wa baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu.
Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Waitara Mwita Mwikwabe, anasema kuwa mpango wa maendeleo wa miaka 5 ni mzuri ukitekelezwa kwa makini na kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa ikiwamo kuinua sekta ya viwanda.
“Mpango huu ni mzuri sana ila ushauri wangu ni kwamba Serikali itafute ama itengeneze vyanzo vingi vya mapato na kuwaelimisha watu umuhimu wa kulipa kodi, na mapato hayo yatumike kwa manufaa ya wananchi,” alisema Mhe. Mwikwabe.
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula, anasema miradi ya kipaumbele kama vile umeme, maji, afya, miundombinu ya reli na barabara, ikisimamiwa vizuri, nchi itapiga hatua kubwa kimaendeleo.
Anasisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushiriki kujenga na kukuza uchumi wa nchi, kwa kujenga viwanda vyenye tija vitakavyoongeza ajira kwa makundi mbalimbali kwa vijana pamoja na Serikali kuweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji wa mitaji na teknolojia kutoka ndani na nje ya nchi.
Ameshauri Serikali ivifuatilie viwanda vyote ilivyobinafsishwa kwa sekta binafsi kama vile viwanda vya nguo, ngozi, maziwa, viwanda vya kusindika samaki, na kuongeza thamani ya mazao, ili vianze uzalishaji kulingana na mikataba ya mauziano viweze kusisimua uchumi, kukuza ajira na kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi kama ilivyokusudiwa.
Mbunge wa Jimbo la Busanda, Lolensia Bukwimba, ameitaka Serikali iwekeze katika sekta ya nishati ikiwa ni pamoja na kupeleka umeme vijijini ili kuweza kuchochea maendeleo na kuwezesha uwekezaji katika viwanda.
Upatikanaji wa nishati ya umeme utachochea kukua kwa miji ikiwa ni pamoja na kutoa fursa za biashara kubwa na ndogo, hivyo kuchangia katika mapato ya Serikali kupitia kodi zitakazokuwa zinalipwa na wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali.
Pia Serikali kutilia mkazo upatikanaji wa maji safi na salama nchini, ni jambo la msingi ili kuondoa adha ya wananchi kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kuwekeza katika shughuli za uchumi.
Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu, naye alipokuwa akitoa mchango wake katika mpango wa Taifa wa maendeleo, alisema kuwa upatikanaji wa maji safi na salama utachochea maendeleo ya sekta nyingine ikiwamo maendeleo ya viwanda pamoja na kuboresha afya za wananchi.
Ili kuchochea maendeleo ya viwanda uimarishwaji wa miundombinu ni jambo la kutilia mkazo hasa reli na barabara, kwani zitawezesha katika usafirishaji nafuu wa malighafi na bidhaa hivyo kuchochea maendeleo ya viwanda nchini.
Katika kuinua sekta ya viwanda, kilimo ndiyo mhimili mkuu wa sekta hiyo kwani ndiyo unaotoa malighafi zinazotumika kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali viwandani. Ni vema sekta ya kilimo ikapewa kipaumbele na kutengewa bajeti ya kutosha ili kuimarisha sekta hiyo kuweza kuharakisha mapinduzi ya viwanda.
Upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo za kutosha kwa wakati mwafaka, ni muhimu kuzingatiwa ili kutoa fursa kwa wananchi walio wengi kujikita katika sekta hiyo muhimu.
Ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, Serikali haina budi iweke nguvu katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kuweza kupata malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda. Kutegemea mvua pekee kutarudisha nyuma jitihada za kuinua sekta ya viwanda nchini.
Pamoja na hayo, mfumo wa ukusanyaji kodi ni vema uimarishwe ili kila Mtanzania aweze kulipa kodi. Suala la kodi ni la kila Mtanzania ambapo kila mmoja anapaswa kulipa kodi anayostahili ili kuweza kuongeza pato la Taifa.
Mbunge wa Viti Maalum, Upendo Peneza, akitoa mchango wake alisisitiza kuwa kuna ulazima wa Serikali kuboresha mifumo ya kodi na kuangalia upya suala la misamaha ya kodi ili kufunga mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.
Hata kwa yule asiyetoa kodi kwa namna moja au nyingine, bado ana jukumu la kuisaidia Serikali kubaini wakwepa kodi kwa kutoa taarifa za wafanyabiashara wasio waaminifu na pia kudai risiti kila wanapofanya ununuzi.
Tatizo la ukwepaji kodi limekuwapo kwa muda mrefu, ambapo hivi karibuni baada ya uongozi wa awamu ya tano kuingia madarakani, tumeshuhudia taasisi za Serikali na binafsi zikihusishwa na ukwepaji kodi ikiwamo upitishaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo makontena yalipitishwa bila kulipiwa kodi hivyo kusababisha Taifa kupoteza mapato.
Uamuzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanzisha matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs) kwa wafanyabiashara katika biashara zao itasaidia kuhakikisha kuwa Serikali inapata mapato stahiki.
Hivyo basi, kama Taifa mpango huu ukitekelezwa vizuri kama ulivyowasilishwa, utaleta mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa wananchi kwa kuwaongezea fursa za kuajiriwa na kujiajiri.
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuimarisha uchumi wa viwanda kuweza kuondokana na utegemezi ili nchi iwe na mahusiano ya kibiashara na iwe na uhuru wa kiuchumi.
Kutokana na mikakati na vipaumbele vilivyobainishwa na mpango huo ikiwamo sekta ya viwanda, ni dhahiri kuwa sekta hiyo itatoa ajira kwa vijana wengi nchini, hivyo kupunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la ajira nchini ambalo limekua kwa kasi kubwa hivi karibuni.
Msisitizo mkubwa wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ni kuhakikisha kuwa watendaji wa Serikali na wananchi kwa ujumla wanabadilisha mazoea kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa.
Ufuatiliaji wa utekelezaji wa mpango huu wa maendeleo wa miaka mitano, unatakiwa kufanyika kwa karibu ili matokeo yake yaweze kupimwa hatua kwa hatua na kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.
Sote kama Taifa tunawajibika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta mapinduzi ya viwanda nchini, kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla na kuweza kufikia uchumi wa kujitegemea.