Mpango mpya ulianzishwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) maalum kwa ajili ya watu kujiunga kutoka sekta binafsi umevutia wananchi wengi kwenye maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Themi Njiro Arusha

Mpango mpya huo ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na viongozi wakuu wa kitaifa unatoa fursa kwa wananchi kutoka sekta isiyo rasmi  kwa wajasiriamali, wafanyakazi, wafanyabiashraa ndogondogo kujiunga kwa ajili ya mafao ya baadae.

Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, Josephat Komba amesema tangu maonesho ya Nanenane yaanze wamepata wanannchi wengi ambao wamefika kwenye banda lao kutaka kujua namna ya kujiunga na mfuko huo.

Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, Josephat Komba, akihudumia wanachama waliotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya  Nanenane mkoani Arusha. Maonesho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo Vijana na Wanawake ni Msingi Imara Mifumo Endelevu ya Chakula.

“Tumepata idadi kubwa ya wananchi. Mpaka sasa tumeishaandikisha wananchi zaidi ya 55 kutoka sekta isiyo rasmi na wengine wanasema watakuja ofisini kwetu  kwa ajili ya kujiunga na mpango huo maalumu,” amesema.

Amesema tangu maonesho hayo yaanze ameshuhudia vijana, wajasiriamali wadogo wakitaka kuwa na shauku ya kujua namna ya mpango maalumu huo jinsi ya kujiunga.

“Wananachi wengi wengi waliofika hapa wengi ni akina mama lishe, vijana, wakulima na wajasiriamali wadogo wadogo,” amesema.

Amesema mwitikio wa vijana kutaka kujiunga na mpango huo maalumu utawasaidia sana kwa sababu akiba ya kesho inaanzia leo.

“Vijana wengi wana kipato hivyo basi ni vizuri wakaanza kuwa na utamaduni wa kuwekeza kwa ajili ya kesho,” amesema.