Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano Na Mazingira) Khamis Hamza Khamis amesema Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha Mpango Mkakati wa kutoa Elimu kwa Umma wa miaka mitano (2022/23-2026/27) kuhusu mazingira.
Lengo la Mpango mkakati huo ni kuhamasisha umma wa Tanzania kuhusu maendeleo endelevu pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Kauli hiyo ameitoa leo Mei 19, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea Bonnah Kamoli aliyeuliza mpango wa Serikali wa kuwapa elimu ya utunzaji mazingira wananchi wanaofanya shughuli za kilimo katika vyanzo na njia za mito ili wafanye kilimo bila kuleta athari za mazingira.
Amefafanua kuwa Mkakati huo wa elimu umehusisha namna ya utoaji elimu kuhusu matumizi ya ardhi ndani ya Mita 60 katika maeneo ya vyanzo vya maji.
“Licha ya Serikali kuruhusu wananchi kufanya shughuli za kilimo kwa umbali wa mita 60 katika maeneo ya vyanzo vya maji, bado kuna changamoto nyingi za uharibifu mkubwa wa mazingira,” amesema.
Kutokana na changamoto hiyo Khamis ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa naomba nichukue fursa hii kuwaomba viongozi wa kisiasa kutumia uwezo wa ushawishi walionao kuhamasisha jamii zinazofanya shughuli za kiuchumi katika maeneo ya vyanzo vya maji kuhifadhi mazingira.