–
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Taasisi ya Bahari ya Korea (Korea Maritime Institute) Dkt. Kim Jong-Deog, Mazungumzo yaliofanyika Jijini Dodoma leo tarehe 15 Juni 2023.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ameishukuru serikali ya Korea kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika masuala mbalimbali tangu kuanza kwa ushirikiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo ikiwemo sekta za afya, elimu, maji na miundombinu. Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Korea kwa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji pamoja na masuala ya uchumi wa buluu.
Makamu wa Rais ameikaribisha Korea kushirikiana na Tanzania katika masuala ya tafiti hususani zinazohusu bahari na rasilimali zake, kuimarisha teknolojia za uvuvi, kuwajengea uwezo wataalamu katika kutumia na kusimamia vema rasilimali za bahari, kuanzisha mpango wa kubadilishana ujuzi pamoja na utalii katika ukanda wa bahari. Pia amesema Tanzania inahitaji uwezo katika kuboresha uvuvi, uchakataji na usambazaji wa samaki pamoja na ujenzi na ukarabati wa meli na mitambo ya baharini.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameishukuru serikali ya Korea kwa kuipa Tanzania kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Uvuvi kati ya Korea na Nchi za Afrika (KORAFF) lililofanyika Zanzibar tarehe 14 Juni 2023.
Ameongeza kwamba Tanzania ni mojawapo ya nchi chache duniani zilizojaliwa kuwa na sehemu ya bahari inayokadiriwa kuwa na ukubwa kilometa za mraba zipatazo 64,000, ufukwe wenye urefu wa kilometa 1,424 pamoja na ukanda huru wa kiuchumi upatao kilometa za mraba 223,000 ambao unaongeza wigo wa shughuli za uchumi wa bahari. Amesema faida hiyo ya kijiografia, ni adimu na adhimu kwani inaipa nchi nafasi kubwa ya kufaidi matunda yatokanayo na bahari pamoja na rasilimali zake.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Bahari ya Korea Dkt. Kim Jong-Deog amesema Korea ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika utafiti pamoja na kubadilishana uzoefu kwa kutambua upekee wa Tanzania ilionao katika ukanda wa bahari. Pia amesema Tanzania na Korea zinaweza kushirikiana kwa kuzingatia kufanana kwa uzoefu, changamoto na masuluhisho mbalimbali yanayohusu masuala ya bahari na rasilimali zake.
Dkt Kim ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano imara tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mwaka 1992. Aidha amesema Vyuo na Taasisi za Korea na Tanzania vinaweza kushirikiana zaidi na kuandaa sera za masuala ya bahari kwa maendeleo ya sasa na baadae.