Milipuko ya mizinga imeitikisa Goma Jumatatu, saa chache baada ya wanajeshi wa Rwanda na wapiganaji kundi la waasi la M23 kuingia mjini humo. Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu mgogoro unaokaribia kutokea.
Mpaka kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) karibu na mji wa Goma uliojaa majeshiumefungwa Jumatatu, chanzo kutoka ubalozi wa Ulaya na mashahidi walisema, saa chache baada ya waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda kuingia mji huo mkuu wa mkoa wa Kongo Mashariki. Rwanda imekana kuhusika licha ya ripoti za kuaminika kutoka Umoja wa Mataifa kuonyesha kuwa inawaunga mkono waasi wa M23.
“Mpaka umefungwa,” kilisema chanzo cha ubalozi katika mazungumzo na shirika la habari la AFP.
“Hakuna anayekuja, hakuna anayekondoka, isipokuwa baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na familia zao waliohamishwa asubuhi hii,” alisema mfanyakazi wa misaada katika kivuko kikuu cha mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Waasi pia wameufunga uwanja wa ndege wa Goma na kuchukua udhibiti wa kituo cha redio cha serikali kilichokuwa kikiendelea kucheza muziki.
Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa, Bintou Keita, alikiambia kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumapili usiku kwamba “tumekwama,” huku uwanja wa ndege ukiwa umefungwa na barabara zote zimefungwa.