Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iko katika maandalizi ya mapendekezo ya muswada kwa ajili ya kupeleka bungeni ili liridhie na kupitisha sheria itakayoweza kuruhusu mtu kuandika wosia ili viungo vyake kutumika baada ya kufariki.
Viungo hivyo ni pamoja na moyo, figo ambavyo vinaweza kutumika kumuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa viungo hivyo.
Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Prof Mohamed Janabi, amesema endapo mapendekezo yao yatapata baraka za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na baadaye kutungiwa sheria na Bunge, yataweza kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya hapa nchini.
“Tunadhani, endapo mapendekezo haya yakipata baraka ya wizara na wabunge kuona umuhimu wake na kuupitisha, utaweza kupunguza upungufu wa viungo vya binadamu katika taasisi hii,” amesema Janabi.
Ametoa mfano nchini Marekani, kila baada ya dakika 10 mtu mmoja huwekwa kwenye foleni ya watu wanaosubiri kuwekewa moyo mpya ili kuendelea kuishi, hali kama hiyo ipo duniani kote lakini huko wanazo sheria ambazo ndiyo kwanza zimeanza kufikiriwa hapa.
“Hali hiyo hutokea baada ya moyo wa mgonjwa kuonekana hauwezi kufanyiwa matibabu na hivyo njia pekee ya kuokoa maisha yake ni kupata moyo mpya ambao mgonjwa huwekewa kwa njia ya upasuaji (transplant),” amesema Janabi.
Amesema umefika wakati kwa Watanzania kuanza kujiwekea utaratibu wa kuacha wosia ili viungo vyao kutumika mara baada ya kufikwa na umauti kwa lengo la kuwasaidia watu wengine wenye uhitaji.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo, Dk Tulizo Shemu, amesema kwa mwaka 2016 taasisi hiyo imefanya uchunguzi wa tiba kwa wagonjwa 973, kati ya wagonjwa hao 620 walipatiwa matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua kwa kupitia mishipa ya damu (Catheterization) na wagonjwa 353 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua.
Amesema taasisi hiyo ina ushirikiano wa karibu na Hospitali ya Appolo Bangalore ya nchini India pamoja na hospitali nyingine za kimataifa za magonjwa ya moyo, hali ambayo imeendelea kuwaimarisha kitaaluma.
“Taarifa za Shirika la Umoja wa Kuchangia Viungo Marekani inasema takribani watu 22 hufariki dunia kila siku nchini humo, wakiwa katika foleni ya kusubiri mtu wa kujitolea moyo kuokoa maisha yao,” amesema Shemu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema wizara haina pingamizi na wazo hilo, kwani kinachohitajika ni ubunifu utakaoweza kuja kusaidia Watanzania wenye uhitaji.
Amesema wizara itaangalia na kujiridhisha na utaratibu huo, kwani kuna nchi nyingi duniani ambazo zinatumia njia hizo na zimewasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza upungufu huo wa viungo.
“Wizara siku zote ipo makini kusimamia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya mifumo, na rufani ya utoaji tiba kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya hadi ngazi za juu,” amesema Mwalimu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), robo ya watu wazima kutoka nusu ya nchi za Afrika zilizofanyiwa utafiti, wapo katika hatari ya kukabiliwa na magonjwa ya moyo kutokana na kuwa na nidhamu mbaya katika mlo.
Ripoti hiyo ya WHO imesema matumizi ya tumbaku, sigara na pombe ni chanzo kikubwa cha mtu kuweza kupata ugonjwa wa moyo, hasa katika nchi nyingi za Kiafrika ambako unywaji wa pombe na matumizi ya tumbaku yapo juu.
Shirika hilo limesema kuwa matatizo yote haya ya afya yanaweza kuzuiwa kwa kula kwa nidhamu, kunywa kwa kiasi na kufanya mazoezi ya kutosha kwa lengo la kuuwezesha mwili kupambana na magonjwa nyemelezi.
Wakati huo huo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imepanga kufanya upasuaji wa kifua kwa wagonjwa wapatao 700 na wengine 1,000 kufanyiwa upasuaji bila ya kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Catheterization.
Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Prof. Mohamed Janabi, amesema Taasisi hiyo ya (The Jakaya Kikwete Cardiac Institute) inajiandaa kutoa mafunzo katika fani ya Upasuaji wa Moyo, Usingizi na Tiba ya Moyo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Amesema Taasisi hiyo imeleta ahueni kwa wagonjwa wa moyo nchini, ambapo kati ya Januari na Machi mwaka huu, imehudumia wagonjwa wa nje 14,257. Wagonjwa waliolazwa ni 912 na imefanya upasuaji kwa wagonjwa 148.
Amesema kati ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mwaka jana, ni wagonjwa 5 tu ndiyo waliofariki dunia ambayo ni asilimia 3.4, kiwango ambacho ni kidogo kuliko wastani uliokisiwa na wataalamu wa afya wa asilimia 13.
“Hali hii inatia matumaini kwa kiwango kikubwa japo taasisi bado inakabiliwa na changamoto za hapa na pale ambazo zinahitaji juhudi za pamoja kukabiliana nazo,” amesema Prof. Janabi.
Prof. Janabi ameliambia JAMHURI kuwa taasisi imekuwa na kambi maalumu ya matibabu ya moyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia kuanzia Machi 10 hadi Aprili 15, ambapo wagonjwa 25 wakiwamo watoto 15 na watu wazima 10 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji.