Takriban wanafunzi saba wa chuo kikuu wamefariki baada ya kuvuta moshi kutoka kwa jenereta katika studio ya muziki katika jimbo la Bayelsa lenye utajiri wa mafuta nchini Nigeria.
Vijana hao wanasemekana kufanya kazi hadi Jumatatu usiku na kulala kwenye studio iliyofungwa huku jenereta ikiendelea kufanya kazi.
Wanashukiwa kupungukiwa na hewa ya kaboni lakini polisi wanasema uchunguzi unaendelea.
Biashara na kaya nyingi nchini Nigeria zinategemea jenereta zinazotumia dizeli au petroli kwa sababu ya ugavi wa umeme usiotosheleza.
Miili sita ilipatikanaJumanne asubuhi, huku mmoja wao, aliyepatikana akiwa amepoteza fahamu, akikimbizwa katika hospitali ya karibu lakini akafariki baadaye, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Wakazi wa eneo hilo walipiga kelele walipochungulia kupitia dirisha la studio na kuona miili hiyo ikiwa imetapakaa sakafuni.
Polisi walifika na kuzingira eneo hilo baada ya kuhamisha miili katika eneo la Amarata la Yenagoa – mji mkuu wa jimbo la Bayelsa.
“Uchunguzi unafanywa lakini kulingana na kile tumeona, sumu ya kaboni kutokana na moshi wa jenereta huenda imechangia vifo hivi,” msemaji wa polisi Musa Mohammed aliambia BBC.
Walioathiriwa walikuwa ni wahitimu wa shahada ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Niger Delta (NDU) kinachomilikiwa na serikali huko Amassoma, ambao walijihusisha na biashara ya kurekodi muziki ili kujikimu kimaisha wanapoendelea na masomo yao.
Hii si mara ya kwanza kwa moshi wa jenereta kuua watu nchini Nigeria, mzalishaji mkuu wa mafuta barani Afrika.
Mnamo 2009, angalau wanafamilia 13, wakiwemo watoto wanne, walikufa baada ya kuvuta moshi yenye sumu kutoka kwa jenereta yao ya umeme walipokuwa wamelala katika kijiji cha kusini-mashariki mwa jimbo la Imo.