PARIS, UFARANSA

Ufaransa inaishutumu Morocco kwa matumizi mabovu ya teknolojia ya kishushushu inayofahamika kama Pegasus – kuwadukua viongozi wake akiwamo Rais Emmanuel Macron na mawaziri 14.

Programu hiyo inayotengenezwa nchini Israel kwa ajili ya udukuzi wa simu za watu, imeshitukiwa kuwa ndiyo inayotumiwa na Morocco kuwadukua viongozi hao.

Shutuma hizo zinapamba moto zaidi baada ya kuwapo taarifa kuwa simu ya mkononi na namba ya simu ya Rais Macron tayari vilikuwa vimeorodheshwa kwenye orodha ya wanaotakiwa kudukuliwa.

Hata hivyo, haijajulikana kama programu hiyo ilikuwa tayari imeingizwa kwenye simu ya Rais Macron au la, japokuwa namba yake ni miongoni mwa namba 50,000 zilizopaswa kudukuliwa tangu mwaka 2016.

Mbali na Rais Macron kutajwa kuwa kwenye orodha ya kudukuliwa, pia Rais wa Iraq, Baram Salith; Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na mawaziri wakuu wa Pakistan na Misri nao wanatajwa kuwamo katika orodha hiyo.

Kutokana na kitendo hicho, tayari Macron amebadili simu yake na namba yake ya simu na ameagiza mfumo wake wa ulinzi kupitiwa upya.

Hata hivyo, uongozi wa Marocco umepinga shutuma hizo ukidai kwamba tuhuma hizo hazina ukweli huku ukikataa kuwa hautumii programu ya Pegasus.

Programu hii huathiri zaidi simu aina ya iPhone na vifaa vinavyotumia Android, ambapo mtumiaji wa programu hiyo huweza kuchota ujumbe wa maandishi, picha, barua pepe na kurekodi simu zote zinazopigwa katika simu ya anayedukuliwa.

Mbali na viongozi wa serikali kuwa kwenye orodha ya kudukuliwa, wengine wanaolengwa ni wanaharakati, waandishi wa habari, wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa wa mataifa mbalimbali.

Mpaka sasa idadi kamili ya simu ambazo zimeshadukuliwa haijajulikana japokuwa mataifa ya Hungary, Israel na Algeria yameanza kufanya uchunguzi dhidi ya matumizi ya Pegasus.

Mbali na Morocco kulaumiwa kwa kuitumia vibaya programu hiyo, Kampuni ya NSO Group iliyotengeneza inapingana na madai ya kutumiwa vibaya kwa programu hiyo.

Kampuni hiyo inadai Pegasus imetengenezwa mahususi kwa ajili ya kupambana na ugaidi na makosa ya kihalifu na kwamba hutumika kwa matumizi ya kijeshi, usalama na watunga sheria.

Katika utetezi huo, NSO wanadai pia huwa programu hiyo huuzwa kwa mataifa yanayosifika kwa kulinda na kuheshimu haki za binadamu.

Kwa miaka ya hivi karibuni kampuni hiyo pia imeingia kwenye lawama baada ya kutajwa kwamba inaruhusu serikali kandamizi kuitumia kudukua taarifa za watu wasio na hatia.

Mmoja wa waathirika wa programu hiyo anatajwa kuwa Jamal Khashoggi, mwandishi wa safu wa Gazeti la Washington Post aliyeuawa Istanbul, Uturuki.