Dunia imeshughulishwa na imeingiwa hofu kubwa juu ya tishio la maambukizi na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona ambao wataalamu wa afya wameupa jina la (Covid-19), ambao umeiathiri sana nchi ya China kwa watu kupoteza maisha na kuwa na idadi kubwa ya waathirika.
Watu wengi wameambukizwa au kuathiriwa na virusi vya corona katika nchi mbalimbali. Alhamdu Lillaah, Tanzania hadi sasa ipo salama na hakujaripotiwa lolote baya kuhusiana na ugonjwa huo hatari.
Kidini, tunapaswa kumuelekea Mwenyezi Mungu tukitubia makosa yetu na kumuomba atuepushie mtihani huu ambao mpaka sasa umezitingisha nchi kubwa zenye uwezo mkubwa wa kiuchumi, kila moja ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana nao.
Kwa muktadha huo, hatuna budi kuitikia mwito wa Mheshimiwa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Bin Zubeir Bin Ally Mbwana, unaotutaka kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aiepushe Tanzania na watu wake na balaa la maambukizi na kusambaa kwa virusi vya corona, wito ambao umeitikiwa pia na Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli, Ijumaa ya Februari 28, mwaka huu alipoungana na Mufti na viongozi wengine wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aiepushe Tanzania na maradhi ya homa ya virusi vya Corona, kudumisha amani na utulivu na kuombea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, ufanyike vizuri na kwa amani.
Ugonjwa wa homa ya virusi vya Corona ni miongoni mwa magonjwa ya kuambukiza na ni hatari sana kwa kuwa maambukizi yake ni kwa njia ya hewa na njia kuu ya kukabiliana nao kwa hivi sasa ni kuweka karantini.
Karantini ni kuzuia miendo ya watu ambao wanaweza kuathiriwa na ugonjwa wa kuambukiza ilhali ugonjwa huo kwao bado haujathibitishwa. Istilahi ya karantini hutumiwa pia kama mgonjwa anazuiliwa kukutana na watu wengine ili kuzuia uenezaji wa ugonjwa hatari.
Katika Uislamu, suala la karantini tunaliona katika mafundisho ya Mtume Muhammad (Allah Amrehemu na Ampe Amani) pale alipoelekeza kuhusu ugonjwa wa tauni (kipukusa) kwamba unapozuka katika mji fulani, basi waliomo katika mji ule wasitoke na walio nje ya mji ule wasiingie.
Mtume Muhammad aliuelezea ugonjwa wa tauni na kisha akasema: “…Basi unapozuka katika mji nanyi mpo humo, msitoke. Na unapozuka nanyi hampo katika mji huo, basi msiuendee”. (Hadith hii inayotokana na Usama Bin Zaid (Allaah Amridhie) inapatikana katika kitabu cha Hadith za Mtume Muhammad kiitwacho Sahih Al-Bukhary).
Tunachojifunza kutokana na mafundisho haya ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ni umuhimu wa kuchukua hatua zinazofaa katika kuzuia maambukizi ya magonjwa yanayoambukiza kama ugonjwa huu wa corona.
Tishio la maambukizi na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona limeathiri, kwa wakati huu, Ibada ya Umrah baada ya Serikali ya Saudi Arabia kuzuia kwa muda utoaji wa viza za kuingia nchini humo kwa shughuli ya Ibada ya Umrah na kuutembelea Msikiti wa Mtume Muhammad uliopo Madina na kulizuru Kaburi lake lililomo katika msikiti huo.
Katika barua yake ya kuelezea hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Saudi Arabia katika kukabiliana na tishio la maambukizi na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Ali Jabir Mwadini, amebainisha kuwa Serikali ya Saudi Arabia imetangaza kusitishwa kwa muda, ujio wa wageni kwa ajili ya Ibada ya Umrah. Aidha, watu waliopewa viza za kitalii ambao wanatoka katika nchi zilizoathirika, nao hawataruhusiwa kuingia Saudi Arabia. Vilevile, raia wa nchi za Ushirikiano wa Nchi za Ghuba (GCC) nao kwa wakati huu hawataruhusiwa kuingia Saudi Arabia kwa kutumia vitambulisho.
Yote haya yanatuonyesha umuhimu wa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuujua ugonjwa huu na dalili zake na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya wanayotoa kila mara kuhusu ugonjwa huu na maambukizi yake. Tuyafanye hayo huku tukiendelea kuomba toba kwa makosa yetu na kumuomba Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema atuepushie balaa hili.
Kadhalika, tuna wajibu mkubwa katika udugu wetu wa kibinadamu kuwaombea ndugu zetu wa China ambao wameathiriwa kwa namna mbalimbali na maambukizi na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona kwa roho za wale waliotangulia mbele ya haki, wale waliokumbwa na virusi na pia changamoto mbalimbali ambazo China inazipitia zikiwemo changamoto za kiuchumi na kijamii.
Yanayoikabili China ni mtihani na wajibu wetu ni kuwaombea Mwenyezi Mungu awanusuru na katu tusiwe ni wafasiri na wachambuzi wa adhabu za Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Tuendelee kunasihiana kuwa watu hapa duniani wapo wa aina mbili: Waliotiwa katika majaribu na wale walisalimishwa na majaribu, basi waonee huruma waliopatwa na majaribu na wala usifurahie majaribu yaliyowafika, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu ana uwezo, akitaka, kuwaondolea majaribu waliyonayo na akakutia wewe majaribuni. Mwenyezi Mungu Mtukufu atuepushie!
Tuzingatie pia kwamba ingawa China ndipo taarifa za awali za balaa hili ziliporipotiwa lakini leo athari za maambukizi ya virusi vya corona zinaripotiwa kutoka nchi mbalimbali. Itoshe kuwa wakati Saudi Arabia inatangaza kusitisha utoaji wa viza kwa ajili kwenda kutekeleza Ibada ya Umrah kama njia ya kukabiliana na maambukizi na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona, tayari Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imeripoti kwamba kati ya watu 26 waliopata maambukizi nchini Kuwait, saba ni raia wa Saudi Arabia ambao inadaiwa walikwenda Kuwait wakitokea Iran na kwamba wamewekwa kwenye uangalizi maalumu huko Kuwait. Yaa Allaah tuepushie maambukizi na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona.
Mbali ya taarifa hii, kuna taarifa mbalimbali za kugundulika walioambukizwa na wagonjwa wa virusi vya corona sehemu mbalimbali na pia zikiwahusisha watu mashuhuri katika jamii zao.
Kadhalika, si China tu inayoathirika kiuchumi bali wale wote waliokuwa wakiamiliana na China katika shughuli zao za biashara pia wameathirika. Vyombo vya habari nchini vimeripoti kuwepo wafanyabiashara wa chini na wa kati nchini ambao wameathirika kiuchumi baada ya mizigo yao waliyoilipia kushindwa kuletwa nchini kwa sababu ya tishio la maambukizi na kuenea kwa virusi vya ugonjwa wa corona nchini China.
Mashirika kadhaa ya ndege yameamua kutosafiri kwenda China kwa hofu ya tishio la maambukizi na usambaaji wa virusi vya corona. Tumuombe Mwenyezi Mungu atuepushie balaa hii ili dunia itulie na shughuli na miamala mbalimbali ya kibiashara na utoaji huduma irudi katika hali zake za kawaida.
Nihitimishe makala hii kwa kuwanasihi watumiaji wa mitandao ya kijamii kuacha tabia ya kusambaza kila wanachokipokea bila ya kukifanyia utafiti au kuhakikisha usalama na umakini wa chanzo cha taarifa hiyo, ili tusije tukayadhuru masilahi ya nchi ambayo ndiyo masilahi yetu kwa tabia hii ya kupenda kusambaza taarifa zenye kuzua hofu na taharuki.
Nasema hili kutokana na mtumiaji mmoja wa mitandao kutoa taarifa ya kuwepo muathirika wa virusi vya corona ambaye ni raia wa China katika hoteli moja nchini wakati si kweli.
Taarifa hii iliyozua hofu na taharuki ilikanushwa na wamiliki wa hoteli hiyo na kutoa ithibati ya kutokuwepo kwa maambukizi ya virusi vya corona nchini Tanzania kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani.
Ewe Mola wetu wa haki, Muumba wa Mbingu na Ardhi na vilivyomo tunakuomba sisi waja wako dhaifu utunusuru na maambukizi na kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa corona.
Tunakuomba Yaa Allaah uwape faraja itokayo kwako ndugu zetu waliothiriwa na maambukizi ya virusi vya corona popote walipo duniani.
Ewe Mola wetu wa Haki wape faraja na utulivu ndugu zetu Watanzania waliopo nchini China na waliokumbwa na karantini ili wafuate maelekezo ya wataalamu wa afya na uwakinge na uwanusuru na balaa hili. Allaahumma Aaamiiin.
Haya tukutane Jumanne ijayo, In-Shaa-Allaah!
Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.
Simu: 0713603050/0754603050