DAR ES SALAAM
Na Aziza Nangwa
Katika mwili kiungo ni kitu muhimu kwa maisha ya mwanadamu, ndiyo maana hata kimoja kikitetereka mtu hawezi kufanya kazi zake ipasavyo.
Tunaona namna gani wanasayansi duniani kote wanavyohangaika kubuni mbinu mbalimbali ili kutatua changamoto ya viungo kwa watu waliovipoteza na kuwasaidia warejee katika majukumu yao ya awali kwa kuwawekea vifaa mbadala kwenye maeneo yaliyoathirika.
Kwa upande mwingine tunaona ni jinsi gani teknolojia duniani kote inavyokwenda kwa kasi, kuhakikisha mwanadamu anapata kitu mbadala baada ya kupoteza cha awali, hasa kiwe na matumizi ya kisasa zaidi baada ya kupoteza.
Hapa nchini serikali kupitia Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) wanatumia wataalamu wao kuwapeleka nje ya nchi kuwasomesha ili waweze kupambana kutengeneza viungo mbadala mbalimbali vitakavyowasaidia wagonjwa kurejea kufanya kazi zao kama kawaida.
Moi wanawatumia wataalamu wao kuhakikisha ni jinsi gani wanavyopambana kutengeneza viungo mbalimbali bandia ili viwasaidie waliovipoteza.
Baada ya jitihada kubwa ya kuwasomesha wataalamu hao, kwa sasa MOI imekwenda mbali zaidi hadi kutengeneza mikono mbadala ya silikoni, kama moja ya viungo bandia vya kisasa vinavyofaa kwa wagonjwa wenye kuhitaji kutumia mikono kama awali.
Hii inafaa kwa wagonjwa walio na hali mbaya ya kiungo kilichobaki baada ya kukatwa, baada ya kuugua kisukari, ajali au kwa uvimbe.
Aina hii ya ‘prosthesis’ ya umeme ni kiungo bandia cha juu zaidi kwa sasa kutumika duniani na kinatumia mfumo wa umeme.
Mkono wa myoelectric umewekwa mahususi kwa ajili ya kuhisi ishara za ujasiri wa misuli iliyokatwa ifanye kazi kama kawaida.
Kifaa hiki kina umeme mdogo uliounganishwa kwenye ngozi na hupokea voltages ndogo zinazosababisha kukaza kwa misuli ya mtumiaji.
Katika makala hii, Gazeti la JAMHURI lilipata bahati ya kuzungumza na Dk. Geofrey Mwakasungula ambaye ni mtaalamu wa Vifaa Tiba Visaidizi wa MOI. Pamoja na mambo mengine, anasema kazi ya kitengo chake ni kushughulika na wagonjwa waliopoteza viungo vyao kutokana na sababu mbalimbali.
Anasema kitengo hicho kina jukumu la kuwatengenezea vifaa mbadala wagonjwa waliopoteza viungo vyao ili waendelee na shughuli zao za kawaida.
Pia anasema serikali inahakikisha MOI inakuwa na vifaa saidizi vya kisasa kwa wagonjwa wenye mahitaji ya viungo vyote bila kuhitaji kwenda nje ya nchi.
“Vifaa saidizi kwa asilimia 70 vimekuwa vikitumiwa na kundi la vijana na kwa uchache ni watoto, wazee na wanawake kutokana na mazingira yao, kwa sababu kundi lao limekuwa ndiyo muhimu katika familia,” anasema.
Dk. Mwakasungula anasema kwa upande wa watoto wamekuwa wakitengeneza vifaa saidizi, hasa kwa wale wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Kuna aina mbili za vifaa visaidizi visivyoingia mwilini mwa mwanadamu ambavyo ni prosthesis – kiungo hakipo kabisa na orthosis – kiungo kipo lakini hakifanyi kazi ipasavyo, hivyo kinawekwa ili kumsaidia mgonjwa afanye kazi zake vizuri.
Dk. Mwakasungula anasema katika kuwekewa vifaa saidizi kwa mtu yeyote aliyepata ajali ya kukatika kiungo ni lazima wamfanyie vipimo vya kiuchunguzi ili kujua hali yake kabla ya kumtengenezea kifaa saidizi.
Anasema vifaa saidizi kwa mtu aliyevunjika kiungo huchukua muda wa miezi mitatu ili kutoa nafasi kusubiri kidonda kipone ndipo wamwekee kifaa bandia.
Anasema kabla ya kuwekewa vifaa bandia mgonjwa anapewa semina ya utumiaji wa kifaa anachohitaji na baada ya hapo ndipo wanatengeneza kulingana na mazingira ya mgonjwa ili kiwe rafiki kwake wakati wa matumizi.
Anasema kwa sasa wagonjwa wanaofika kununua viungo bandia ni kundi la vijana wa kiume kuanzia umri wa miaka 15 hadi 30 na wengi wao wakiwa madereva wa bodaboda.
Kwa upande wa wazee, anasema wanaokwenda ni kuanzia umri wa miaka 55 hadi 65 na wengi wao wakiwa wamepoteza mikono na miguu kutokana na matatizo ya sukari.
Anasema vifaa mbadala wanavyotoa ni vya kisasa na hawajawahi kutoa mgonjwa kwa rufaa kwenda nje ya nchi kwa sababu wanavyo vya kutosha.
“Kwa sasa watu wanaokuja kutibiwa hapa MOI na kuondoka wengi wao wanauhitaji wa vifaa bandia lakini wanaoweza kumdu gharama ni wachache kutokana na uwezo wao kuwa mdogo na bei za vifaa kuwa juu,” anasema.
Dk. Mwakasungula anasema kifaa kimoja kinaweza kuuzwa Sh milioni tano na kuendelea, na kwa mtu mwenye kipato cha kawaida hawezi kununua haraka hadi ajipange ndipo atapata huduma.
Anataja changamoto ya malipo ya gharama za kulipia utengenezaji wa vifaa mbadala kuwa ni kubwa, hivyo ni vema serikali ikaingiza gharama za huduma hizo za vifaa visaidizi kwenye bima ya afya ili iwe mkombozi kwa wananchi na kupunguza watu waliopoteza viungo kuwa tegemezi kwenye jamii.
Kwa upande wake, Bingwa wa viungo bandia wa MOI, Dk. James Jacob, anasema katika kitengo chake mgonjwa akipelekwa wanamfanyia uchunguzi wa tatizo alilonalo, umri na uzito ili kujua afya yake na kumpanga katika orodha ya watu wanaohitaji na aina ya kifaa anachohitaji.
Anasema wanafanya hivyo kabla ili kujua kama mgonjwa anayehitaji kiungo mbadala ni wa kawaida au ana kisukari. Kwa sababu wanatofautiana katika utengenezaji wa vifaa vyao.
“Idara yetu inatengeneza vifaa vya aina mbili; kuna vifaa kwa ajili ya wagonjwa wa dharura siku hiyohiyo, na wale wa kawaida ambao vifaa vyao huchukua siku tano kukamilika,” anasema.
Dk. Jacob anasema kila siku ni lazima watembelee wodini na kushirikiana na madaktari ili kuona kama kuna mgonjwa anayehitaji kuwekewa vifaa visaidizi kutokana na vipimo vinavyoonyesha.
“Hapa MOI sisi tuna mikono ya bandia inayofanya kazi nzuri kama kiungo cha awali cha mwanadamu, hii hasa inawafaa zaidi watu wa maofisini na wale wenye kisukari kwani ni salama na wala hawachubuki,” anasema.
Pia anasema katika utengenezaji wa vifaa bandia kwa mguu kuna changamoto kubwa kama ukikatwa vibaya na ndiyo maana wanakaa na madaktari katika semina mbalimbali na kuwashauri namna nzuri ya ukataji wa mguu kwa mgonjwa.
“Shida ya mguu ukikatwa karibu na goti ni shida, lakini ukikatwa mbali ni rahisi hata kupata kifaa sahihi na haraka kwa ajili ya mgonjwa,” anasema.
Naye Ofisa Vifaa Tiba Visaidizi wa MOI, Joyce Valisango, anasema kitengo chake kimekuwa kikipokea oda ya vifaa mbadala kwa kundi kubwa la vijana kuliko wazee na makundi mengine.
“Kwa sasa vifaa mbadala ni ghali kuagiza nje ya nchi, hivyo MSD isaidie kununua nje ya nchi ili kupunguza gharama kwa jamii na iingizwe kwenye bima ya afya,” anasema.
Joyce anasema kwa kawaida mgonjwa lazima apitie uchunguzi kabla ya kutengenezewa vifaa visaidizi ili visimletee madhara wakati wa kutumia.
Anasema kwa sasa wana vifaa vya kisasa na mashine za kisasa ambavyo mgonjwa hachukui muda mrefu kupata huduma.
Kuhusu ukomo wa muda wa utumiaji wa vifaa visaidizi kwa watu wazima, anasema hakuna ukomo ila inategemea na mtu anakitunza vipi, tofauti na vifaa vya ndani ya mwili ambavyo mgonjwa hulazimika kutolewa baada ya muda tangu matibabu ya awali yalipofanyika.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, anasema wanaendelea kusomesha wataalamu wengi ili wawe wa kutosha kwa ajili ya kutoa huduma.
Vilevile wanaendelea kutafuta malighafi zinazohitajika ambazo bei yake ni rahisi ili kupunguza gharama za utengenezaji
wa vifaa mbalimbali kwa wagonjwa.
Pia Dk. Boniface anasema wataendelea kuelimisha umma umuhimu wa kujikinga dhidi ya ajali, hasa za barabarani, na kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, kwani ndivyo vyanzo vikubwa vya kupoteza viungo.