*Wawaomba wadau kuchangia 

Sh milioni 800 kwa mwaka kufanikisha

DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) inatarajia kufuta tatizo la watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa na migongo wazi kwa kuwafanyia upasuaji wa kuwawekea vipandikizi.

Akizungumzia tatizo hilo, Bingwa wa upasuaji, magonjwa ya ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, Dk. Hamisi Shabani, anasema tatizo la  mtoto kuwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi ni matokeo ya ukosefu wa virutubisho ambavyo ni vyakula vyenye folic acid na vidonge vyenye madini vinavyotolewa kwa wajawazito na wenye upungufu wa damu.

Dk. Shabani anasema ugonjwa wa mgongo wazi au vichwa vikubwa unaweza kumkumba mtoto yeyote ambaye mama yake hakupata virutubisho anavyotakiwa avipate kabla ya kushika mimba. 

Anasema kwa kawaida virutubisho hivyo vinapatikana katika vyakula vyote vyenye protini na vina uwezo wa kumzuia mama kwa asilimia kubwa asipate changamoto ya kuzaa mtoto mwenye ulemavu wa mgongo wazi na kichwa kikubwa.

Ugonjwa wa mgongo wazi au (spinal bifida) na vichwa vikubwa ni ulemavu anaozaliwa nao mtoto na akishaupata matibabu yake ni upasuaji wa haraka ili kuzuia tatizo lisiendelee na katika hatua hii mama anatakiwa kumuwahi pindi anapozaliwa tu afanyiwe matibabu.

“Wasichana wengi hivi sasa wamekuwa wakijifungua watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa sababu wamekuwa wakishika ujauzito huku wakiwa hawajui kama wana upungufu wa madini ya folic acid,” anasema.

Dk. Shabani anasema ili mama aweze kuepuka kuzaa mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi anatakiwa kabla ya kushika mimba ale vyakula vyenye protini kama mayai, mboga mboga, maziwa, mahindi, maharage, parachichi, embe na kadhalika.

Anasema wazazi wenye watoto hawa wengi wanakuwa hawajui hadi pale mtoto anapozaliwa ndipo anaonekana tofauti. Wengine wanazaliwa na kichwa kikubwa au mgongo wazi, na huyo anakuwa na kidonda nyuma ya mgongo hivyo daktari atajua ana tatizo litakalohitajika kufanyiwa upasuaji wa haraka.

“Changamoto hii ikitokea mzazi anatakiwa achukue hatua za haraka za kumleta mtoto hapa MOI ili afanyiwe tiba ya upasuaji wa haraka wakati akiwa mdogo, kwa sababu akichelewa kufanyiwa anaweza asiweze kutibika, kwani itakuwa imeshakamata sehemu ya ubongo,” anasema. 

Dk. Shabani anasema mtoto anayewahi mapema kufanyiwa upasuaji anakuwa yupo salama zaidi na inamfanya apone haraka kwa asilimia kubwa kuliko akichelewa kupata matibabu anakuwa katika hatari ya kupata ulemavu wa kudumu na  mara nyingi anakuwa na mtindio wa ubongo kwa sababu anakuwa amechelewa.

“Kwa asilimia kubwa wazazi wa watoto wenye ulemavu huu bado wana mwitikio mdogo, kwa sababu walio wengi wanapata unyanyapaa mkubwa kwenye jamii, hasa nyumbani, hivyo kusababisha waendelee kukua na ulemavu huo maisha yao yote, ambapo kama wangewaishwa ungetibika kabisa,” anasema.

Dk. Shabani anasema tafiti zinaonyesha asilimia kubwa ya kina mama wenye watoto hao wameachwa na waume zao na kusababisha kuwa na maisha magumu na wao wameliona hilo na kutoa nafasi kwa wazazi kuwapeleka wagonjwa kutibiwa bure na kuwaondoa katika hali ya ulemavu.

Anasema dalili za mtoto aliyepata ulemavu wa kuwa na kichwa kikubwa hazina tofauti na mgongo wazi na wazazi lazima wawe waangalifu hasa pale anapozaliwa ili wamsadie kutopata ulemavu wa kudumu kwa kumfanyia upasuaji wa haraka.

Anasema mtoto mwenye ulemavu wa kichwa kikubwa akizaliwa utosi wake unakuwa tofauti na  wengine kwa sababu hauchezi na mikono yake inakuwa mara kwa mara inakakamaa na mwishowe kama hakupata matibabu mapema kutamsababishia kuathirika kwa ubongo.

“Mtoto mwenye mgongo wazi anakuwa na kidonda mgongoni, miguu inakuwa na ulemavu, anakuwa na matatizo ya haja kubwa na haja ndogo zinakuwa zinatoka mfululizo na asipowahiwa anakuja kupata tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi anakuja kuwa na kichwa kikubwa,” anasema.

Pia anasema kwa asilimia kubwa matibabu ya mgongo wazi na kichwa kikubwa yanatakiwa kutibiwa mara moja pindi mtoto anapogundulika kupata dalili za awali kwa kupatiwa matibabu ya kufanyiwa upasuaji na kuwekewa vifaa maalumu katika mwili wake vitakavyomsaidia kuondoa tatizo hilo kwa haraka.

“Baada ya upasuaji anatakiwa mtoto kuhudhuria kliniki mara kwa mara hadi atakapotolewa vipandikizi, hivyo kwa sababu asipotolewa anaweza kupoteza maisha, kwani baadhi ya wazazi wamekuwa hawarudi tena baada ya upasuaji wa kwanza,” anasema.

Dk. Shabani anasema kwa sasa wanawafanyia upasuaji watoto 60 kwa mwezi, kwa mwaka watoto 800, na wanaohitaji matibabu ya migongo wazi na vichwa vikubwa hawana fedha za kutosha za kuwawezesha kuwafanyia huduma hiyo.

“MOI tunawafanyia matibabu ya upasuaji watoto hao bure ambao kwa mwaka wanatumia Sh milioni 800 kwa ajili ya kuwafanyia tiba watoto hao ili kuwarejesha katika hali zao kama watoto wengine.

“Changamoto iliyopo kwa sasa ni wazazi wengi wanaokuja katika hospitali hii wanakuwa wamechelewa, kwa sababu wamekuwa na dhana kwamba ulemavu wa watoto hao ni suala la kishirikina na linatakiwa kupelekwa kwa mganga wa tiba asili, hivyo hutumia muda mrefu kuwapeleka huko, mwishowe wanawaleta hospitalini wakiwa wamechelewa, kwa hiyo hatuna jinsi, tunawaacha kuwafanyia upasuaji,” anasema.

Kuhusu gharama za matibabu kuwa kubwa, anasema ni kwa sababu wagonjwa hao wanahitajika kutumia vipimo vya CT-Scan, MRI na viambatanishi wanavyowekewa katika upasuaji, na vyote vinahitajika kununuliwa ikiwamo chakula bora ili kuwapatia lishe kutokana na utapia mlo mkali kisha baada ya kuimarika wanafanyiwa upasuaji.

Dk. Shabani anasema wazazi wanaokutana na changamto hii wengi wao ni wasichana wenye  umri wa miaka 18 hadi 25 na wamekuwa hawajui  kula vyakula vilivyo bora bali mara nyingi wanakula chipsi, ndiyo maana wanatumbukia katika kuzaa watoto wenye mgongo wazi na vichwa vikubwa.

Anasema hali hiyo hutokea wiki mbili za mwanzo za ujauzito kutokana na uti wa mgongo wa mtoto kukwama kujiunga kikamilifu kama inavyopaswa kuwa kwa taratibu za kimaumbilie na matokeo yake uvimbe unaofanana na mfuko hutokea baada ya mishipa ya fahamu kujikusanya sehemu moja nje ya uti wa mgongo na baada ya hitilafu hizo mtoto anayezaliwa huwa mlemavu kwa kukosa hisia katika mfumo wa haja kubwa na ndogo pamoja na miguuni.

Anasema asilimia 60 ya watoto wanaozaliwa kila mwaka wana tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi kutokana na wazazi wao kuwa na utapiamlo mkali kabla ya kupata mimba.

Kuhusu mikakati ya MOI, anasema wataendelea kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kujikinga na tatizo, ikiwamo lishe bora yenye virutubisho vya folic acid wakati wa ujauzito.

Pia anasema wataendelea kuhimiza jamii kuhusu umuhimu wa kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito na kuelewesha jamii kuhusu dalili za awali za mtoto mwenye tatizo hili na umuhimu wa kumuwahisha hospitalini mapema kwa matibabu.

Anasema wataendelea kutoa tiba bora kwa watoto wenye matatizo haya wafikapo hospitalini kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata fedha za gharama za matibabu.

Anasema watafundisha wataalamu kwenye hospitali nyingine nchini jinsi ya kuwatibu watoto hao ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Muuguzi wa Chumba cha Upasuaji cha MOI, Mariamu Kumbwani, anasema kazi yake kubwa ni kuangalia usalama wa mgonjwa na vifaa vitakavyotumika kufanya upasuaji kabla na baada.

Mariamu anasema kabla mgonjwa hajafanyiwa upasuaji anahakikisha anayetaka kufanyiwa ndiye mtoto sahihi na aina ya matibabu, kwa kuzungumza naye au mzazi wake ili kujiridhisha na kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Anasema baada ya hapo anaangalia maelekezo ya daktari wa usingizi na kuangalia kama amepima vipimo vinavyohitajika na baada ya upasuaji mgonjwa anatakiwa kupelekwa wapi, wodi ya kawaida au ICU.

Anasema baada ya hapo anaangalia usalama wa vifaa vinavyohitajika kufanya upasuaji huo kama vipo sawa, ikiwamo mashine na taa ili kumrahisishia daktari kuifanya kazi yake kwa usalama wa hali ya juu.

Baada ya upasuaji, anasema anaangalia maelekezo ya daktari kama mgonjwa ameandikiwa wodi maalumu au chumba cha kawaida.

“Kama ni wodi ya kawaida, mgonjwa anachukua nusu saa hadi saa nzima. Akitakiwa wodi maalumu anatakiwa kwenda moja kwa moja,” anasema. 

Mmoja wa wazazi aliyeleta mgonjwa kutibiwa, Jeremia Mushi, anasema mtoto wake amekuwa akisumbuliwa na tatizo hilo tangu alipozaliwa.

Mushi anasema mara kwa mara alikuwa akisumbuliwa na degedege ndipo madaktari wakashauri afanyiwe upasuaji ili aweze kuwa sawa.

“Leo nimeshuhudia mtoto wangu akiwa amefanyiwa upasuaji salama, naishukuru MOI  kwa kumfanyia mtoto wangu, namuomba Mungu aendelee kuwa salama,” anasema.