Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba, Joseph Omog ametakiwa kujiuzulu mara moja baada ya timu hiyo kuondolewa mapema katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) ambalo wao ndio walikuwa mabingwa watetezi.

Simba ilifungishwa virago na Green Warriors inayoshiriki ligi daraja la pili baada ya kufungwa jumla ya penati 4-3 kufuatia kutoka sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 za mchezo.

Wito wa kumtaka Omog kujiuzulu umetolewa na Mohammed ‘Mo’ Dewji ambaye ndiye aliyeshinda zabuni ya kuwekeza ndani ya klabu hiyo baada ya Simba kukubali kubadilisha mfumo wa kujiendesha.

Kupita ukurasa wake wa Twitter, Mo Dewji ameandika, “”Kwa kuwa bado sina mamlaka ya maamuzi kwenye klabu ya Simba, kama mwanachama na mshabiki wa Simba, namuomba OMOG kwa heshima na taadhima ajiuzulu.”

Mbali na Mo, mashabiki wengi wa Simba wlionyesha kuchukizwa kwa kitendo cha timu hiyo kutolewa, kwanza katika hatua za awali kabisa za michuano hiyo, lakini pia kuondolewa na timu inayoshiriki daraja la pili ambayo waliamini isingewasumbua.

Hadi sasa hakuna taarifa yoyote kutoka ndani ya klabu hiyo kuhusu shinikizo hilo lililotolewa na Mo.