Wiki hii nilikusudia kuandika makala fupi kueleza yale niliyoyaona kwa majirani zetu wa Mashariki na Kusini mwa Afrika. Kama ilivyo ada ya mtembezi, yapo mabaya, lakini yapo mazuri pia anayoyaona awapo matembezini. Naomba kazi hiyo niifanye kwenye matoleo yajayo.
Nimeguswa na uamuzi uliotangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, uliomlenga aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu.
Kabla sijaenda mbali, niseme siandiki kumtetea wala kuhoji uamuzi uliotangazwa na Waziri Lukuvi. Lukuvi, na bila shaka uongozi wa juu wa Serikali wanajua kwanini wamemwondoa. Sihoji hilo kwa sababu mamlaka ya uteuzi ndiyo hiyo hiyo yenye mamlaka ya utenguzi. Kwa hiyo sihoji sababu za kuondolewa kwake, bali nataka walau kutambua mchango wa Mtanzania huyu kwenye ustawi wa taifa letu.
Nayasema haya mapema ili kuwahadharisha mabingwa wa kupindisha maneno, hasa kama ikitokea njia ya uwasilishaji ni ya kuhadithiwa badala ya mhusika kusoma nilichoandika!
Namsema Mchechu akingali hai ili nimtendee haki. Namzungumza kwa sababu hatukukutana barabarani! Nimemfahamu tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakati huo nikiishi Msasani na yeye akiwa kwa wazazi wake katika eneo hilo. Kwa Mzee Mchechu ndiko tulikokusanyika kuangalia mashindano ya Kombe la Dunia kama haya yanayoendelea sasa. Nyumbani kwao ndiko tulikojazana sebuleni kuangalia masumbwi ya kina Mike Tyson. Haya mambo wanayajua wa wale wa wakati huo.
Mchechu akingali mdogo alitushangaza wengi wetu. Akili yake kwenye biashara ilikata kama wembe mpya. Mbele tu ya makazi ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, alikuwa na duka la vyakula na la vinywaji –maarufu kwa jina la Nelly’s Grocery. Hapo palikuwa kivulini kwa wengi.
Mchechu akiwa bado mwanafunzi alimiliki daladala, pikipiki na kadhalika. Hii ilikuwa miradi yake. Hapakuwapo mkono wa wazazi au ndugu zake. Sana sana tulichojua amekipata kwa baba yake ni uwanja alioutumia kuweka biashara zake. Uwanja huo ulikuwa wa familia yao. Japo kwa rika tulionekana tuko sawa, nikiri kuwa mwenzetu alionekana mahiri mno kwenye ‘usakaji maisha’.
Sikuwa na sababu ya kumwuliza, hasa baada ya kufahamu wakati huo akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam masomo yake yalikuwa ya ‘fedha’. Kwa hiyo huyu ni mtu aliyebobea kwenye masuala ya fedha, si kwa bahati mbaya, bali kwa karama aliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Anayedhani Mchechu amepata fedha baada ya kupelekwa NHC anajidanganya! Wasifu wake pekee unathibitisha kuwa huyu mwenzetu kwa lugha ya mitaani ni ‘mchakalikaji’ wa kweli kweli.
Baada ya kutoa hiyo bashraf, sasa naomba walau niseme machache yanayohusu utendaji kazi wa Mchechu akiwa NHC. Hapa sitogusa kabisa maeneo mengine aliyofanya, lakini itoshe tu kusema ameshakuwa MD & CEO wa CBA Bank, Standard Chartered Bank Tanzania Limited, Citibank, Barclays Bank Tanzania Limited, Mwenyekiti wa Serengeti Breweries Ltd, Mwenyekiti wa Amboni Sisal Properties Limited na Mwenyekiti wa Amboni Beach Limited, Mwasisi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Rightway Schools, Mjumbe wa Bodi ya Benki ya KCB Tanzania Limited; Mwenyekiti wa East Africa Breweries Limited, Mkuu wa Ukaguzi Chuo Kikuu cha Tumaini; Mkurugenzi wa Tanzania Investment Center (TIC); Mkurugenzi na Mwanachama Mwanzilishi wa CEO Roundtable, Mjumbe wa Kamati za Baraza la Biashara la Taifa, na kadhalika na kadhalika. Umri wake na nafasi alizoshika vinatoa ujumbe mahsusi- kuwa huyu ni mtu mahiri kwenye masuala ya fedha na uongozi.
Simzungumzi Mchechu aliyeondolewa NHC, bali namzungumza Mchechu kama mmoja wa vijana wenye uwezo mkubwa waliofanya mapinduzi yenye kuonekana kwa macho katika ujenzi wa taifa letu.
Namzungumza Mchechu kama kijana Mtanzania mzalendo ambaye kuondolewa kwake NHC hakuwezi kufifisha wala kuizika rekodi iliyotukuka ya mageuzi makubwa na ya kweli aliyoyafanya kwenye shirika hilo tajiri kuliko mashirika yote ya umma katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Namzungumza Mchechu kama kijana aliyechukuliwa mwaka 2010 kutoka kwenye maisha manono ya kibenki, kwenye ofisi yenye viyoyozi na posho nzuri, na kupelekwa kuongoza shirika mfu ambalo hata viti vya kukaliwa na wafanyakazi havikuwapo.
Tumtazame Mchechu yule ambaye alipelekwa NHC iliyoonekana shirika lisilowiana na heshima na umaarufu wake kwa wakati huo, lakini akakubali kwa kuamini Tanzania itajengwa na Watanzania. Hakutaka kumkwaza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa wakati huo, John Chiligati, ambaye pengine kwa kushaurina na viongozi wakuu waliona hazina ndani yake.
Tunapomjadili Mchechu, tumjadili kwa kumpa haki anayostahili ya kutambuliwa kama ndiye Mkurugenzi Mkuu wa NHC wa kwanza aliyefanya sensa iliyotuwezesha wenye mali (Watanzania) kujua ukubwa na thamani ya shirika hili.
Akachukua dhima kuzipaka rangi nyumba za NHC walau kuwaonyesha Watanzania kuwa hizi ni mali zao walizo na haki nazo kuanzia kwenye utambuzi hadi kwenye manufaa yake. Kwa utaratibu huo tukatambua nyumba ambazo awali tulidhani zinamilikiwa na watu binafsi. Mpango huu ukawa kama ule uliosimamiwa na Dk. John Magufuli, akiwa Waziri wa Ujenzi ambako alifanikisha kuwapo namba maalumu za DFP kwa magari ya miradi ya wafadhili ambayo kimsingi ni kodi ya Watanzania. Tunapomhukumu Mchechu, basi tukumbuke na hili la utambuzi wa nyumba za NHC.
Mchechu alishiriki vita ambayo pengine ingeweza kumtoa uhai. Kulikuwa na mpango uliosukwa na kusukika – wa baadhi ya Watanzania kujitwalia nyumba za NHC zilizopo Upanga, Dar es Salaam. Wakaweka mawakala ‘wazawa’ ili ionekane hoja hiyo ni ya wengi! Mchechu akabaini janja yao. Mpango wa kujimilikisha nyumba za Upanga ukakwama kwa hoja kwamba sababu zilizoifanya Serikali ya Awamu ya Kwanza izitwae, bado ziko hai na zitaendelea kuwa hai. Waliokuwa wamejipanga kufaidi wakanuna. Wakamchukia kweli kweli.
Mchechu tumhukumu kwa kazi kubwa na iliyotukuka ya kusimamia mapato ya NHC kutoka kwa wapangaji wake wote. NHC ilikuwa kama pombe ya msibani (ambayo ni kama vile haina mwenyewe). Wapo waliojitwalia nyumba wakailipa NHC Sh 200,000 kwa mwezi, lakini wao wakapangisha hadi Sh 1,500,000. Akajenga hoja kwamba kama wapangaji waliopangishwa na ‘kuuziana upangaji’ wanaweza kulipa kiwango hicho, kwanini wao wasiingie mkataba na NHC na wakapunguziwa? Mbinu hiyo ikaongeza mapato ya NHC kwa mabilioni ya shilingi. Amepelekwa NHC ikiwa inakusanya Sh bilioni 3 kwa mwezi, na sasa inakusanya hadi Sh bilioni 9.
Ameichukua NHC ikiwa na kesi 350, lakini naambiwa hadi juzi zilibaki kesi 50 pekee. Kuna genge la watu waliokuwa wakilipwa hadi Sh bilioni 4 kwa kushinda kesi zilizoundwa kwa lengo la kuchota fedha za shirika. Kuna watu waliishi maisha yao yote kwa mbinu hiyo. Mchechu wamewadhibiti.
Wote walioiona NHC kama jaa miaka hiyo, ghafla wakaiona kama mgodi wa dhahabu! Kila mmoja akatamani afaidi yaliyomo. Fitina zikajengwa na kuenea. Ugomvi wa vyeo ukaanza. Vi-memo vya kuteuliwa ujumbe wa Bodi vikawa havina idadi. NHC imenona. Kila mmoja anataka udi na uvumba aifaidi.
Mchechu amesimamia miradi ya NHC Tanzania Bara. Chini yake NHC imepata viwanja kwenye halmashauri karibu zote. Kuna nyumba zimejengwa na zinaendelea kujengwa. Ametekeleza miradi mikubwa mingi.
Mchechu ameondelewa NHC. Nasema sijui kilichomfika, lakini itoshe tu kusema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Ametekeleza wajibu wake wa kulitumikia taifa. Hakuna binadamu aliye mtimilifu. Inawezekana kuna mahali amekosea. Sijui. Hata kama hivyo ndivyo, bado makosa hayo hayawezi kutufubaza akili hata tuipuuze kazi kubwa na iliyotukuka aliyolifanyia taifa letu.
Ameacha alama itakayodumu kwa miaka mingi ijayo. Anayo ya kujivunia, na kwa hakika kwenye kitabu chake cha kumbukumbu ana kila sababu za kuwaandikia wajukuu na vitukuu mlolongo wa mema aliyoyafanya kwa manufaa ya nchi hii.
Mchechu hajachoka akili wala mwili. Bado ana fursa ya kuonyesha kwa vitendo kipaji vyake alichojaliwa na Mwenyezi Mungu. Mwanazuoni David Millar, amewahi kusema, “People do make mistakes and I think they should be punished. But they should be forgiven and given the opportunity for a second chance. We are human beings.”
Naye, Tia Mowry, kwenye kuthibitisha kuwa mtu anapopata fursa ya pili anakuwa bora zaidi, anasema, “Having a second chance makes you want to work even harder.”
Kwa baadhi yetu, Mchechu anaendelea kuwa mmoja wa vijana mahiri walioweza kulitumikia taifa hili kwa mafanikio makubwa. Nawashukuru kwa kuniruhusu nimeseme Mchechu akingali anapumua. Namtakia kila la heri kwenye dhima nyingine mpya kadri itakavyokuwa.