Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba ameishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kuwezesha upatikanaji wa Kliniki ya Himofilia na Selimundu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma – Maweni.
Dkt. Jesca ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Prof. Pascal Rugajo katika uzinduzi rasmi wa Kliniki hiyo amesema uwepo wake katika kanda ya magharibi utasaidia wagonjwa kupata huduma karibu badala ya kuzifuata mbali.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Maweni Dkt. Stanley Binagi amesema MNH kupitia mradi wa kuongeza kasi ya upatikanaji huduma kwa wagonjwa wenye changamoto ya magonjwa ya damu imewezesha ukarabati wa jengo, upatikanaji wa vipimo, vifaa vya mazoezi na dawa kwa wagonjwa wa Himofilia
“Kabla ya uzinduzi huu yalitangulia mafunzo kwa watoa huduma yaliyotolewa na wataalamu wa MNH kuhusu na namna ya kuwatambua na kuwahudumia wagonjwa wa Himofilia kwa wataamu wa maweni na hospitali za jirani, jambo ambalo litawasaidia kumudu uendeshaji wa kliniki hii” amesema.
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. John Rwegasha ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji amesema Muhimbili itaendelea kutekeleza jukumu la kuzijengea uwezo hospitali za rufaa na mikoa ili kuhakikisha kuduma za kibingwa zinafika karibu na wananchi.