Na Mwamvua Mwinyi, JahuriMedia,Kibaha
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ,CCM (MNEC) kupitia Wazazi ,Hamoud Jumaa ameeleza nguzo pekee ya ushindi katika uchaguzi wa Serikali ya Mitaa 2024 pamoja na uchaguzi Mkuu 2025 ,ni wanaCCM kudumisha umoja na mshikamano pasipo kuweka mipasuko isiyokuwa na tija .
Aidha amewataka wanaCCM kujipanga kuelekea katika chaguzi hizo kwa kuwa na umoja madhubuti ,kushawishi wanachama wapya,kulipa ada na kuchangia maendeleo ya Chama .
Jumaa ambae alikuwa mgeni rasmi wakati wa majumuisho ya ziara ya Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Mwalimu Mwajuma Nyamka, ambapo anasisitiza mahusiano mazuri .
Vilevile, anawaasa wale walioanza rafu mapema kabla ya uchaguzi hizo waache viongozi waliopo madarakani watimize wajibu wao kwasasa.
“Hapa Mbunge wa jimbo hili ni Silvestry Koka ,bado ni mbunge wa jimbo hili, hajamaliza muda wake,muacheni afanye kazi ,msimvunje moyo, kama kuna watu wanataka kuchangia Chama wachangie kwa kufuata kanuni na taratibu bila kutumia kigezo cha kutoa misaada ili kumyumbisha “
“Chama hiki hakiwezi kujengwa na mtu mmoja, mwanachama mwenye nia ya kujitolea anaweza kujitolea lakini afuate taratibu na kutoa taarifa kwa Chama ili kuondoa misuguano isiyo ya lazima “alifafanua Jumaa.
Vilevile Jumaa alikipongeza Chama hicho wilaya ya Kibaha Mjini ,chini ya Mwenyekiti Nyamka kwa kusimamia utekelezaji wa ilani.
“Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa, Dkt Samia Suluhu Hassan anaitendea haki ilani ya Chama kwa kutekeleza miradi mbalimbali nchini kuanzia matawi,mashina,kata,wilaya na mikoa, na sisi tunapaswa kusimamia utekelezaji huo na wilaya hii mnafanya vizuri “alieleza Jumaa.
Awali Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Mwajuma Nyamka, alisema katika wilaya hiyo utekelezaji wa ilani, umetekelezwa kwa asilimia 90.
Alieleza, kwenye ziara yake amezunguka kata zote 14 na kuzungumza na mabalozi wa mashina,wenyeviti na wanachama.
Jumaa alieleza, katika wilaya hiyo kuna zaidi ya wanachama 50,000 na wanachama wapya ni 2,652 .
Nae mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka,aliwashukuru wanachama, mabalozi wa mashina, wenyeviti kuendelea kushirikiana ili kukiimarisha Chama.
Koka alieleza, kila Kiongozi atimize wajibu wake kwa nafasi yake, na yeye atahakikisha anaendelea kusimamia changamoto za wananchi na kuwasemea kero zao ili zipatiwe ufumbuzi.