Na Mwandishi Wetu, JamhuriMwdia, Dodoma


Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya umwagiliaji nchini.

Lengo ni kuboresha kilimo nchini, na kuongeza hali ya upatikanaji wa chakula ili kufikia adhima ya kuilisha dunia. Vilevile ni kuhakikisha inakabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo upatikanaji wa mvua umekuwa sio wa uhakika.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NiRC), Raymond Mndolwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari, wakati akishiriki kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Alifafanua kuwa uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na serikali una lengo la kuboresha kilimo cha Tanzania kwa kuhakikisha kunakuwa na miundombinu bora ya umwagiliaji.

“Hadi hivi sasa tumeshatekeleza miradi 115, tukiwa na miundombinu ya umwagiliaji ambayo itawawezesha wakulima kuzalisha zaidi ya mara moja kwa mwaka, hivyo watakuwa na uhakika wa chakula na ziada watauza,” alisema Mndolwa.

Mndolwa aliongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji ni kuongeza uzalishaji wa chakula, biashara, na kutimiza lengo lililotolewa na Rais Dkt. Samia la kutaka Tanzania kulisha dunia.

Aliwasisitiza wakulima kuweka nguvu kubwa katika uzalishaji wa chakula na kuhakikisha wanatunza miundombinu ya umwagiliaji ambayo serikali imewekeza, kwani kumekuwa na kasumba ya watu kuharibu miundombinu hiyo.

“Hadi hivi sasa, fedha ambazo serikali imewekeza katika sekta ya umwagiliaji ni zaidi ya shilingi trilioni 1.2. Nimhakikishie Rais Dk. Samia kuwa Tume ya Umwagiliaji itahakikisha inazisimamia fedha hizo na kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakuwa bora na kuleta tija kwa Watanzania,” alisisitiza Mndolwa.

Akizungumza kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Mndolwa alisisitiza kuwa kwa mwaka huu tayari hali ya ukame imeshaanza kuonekana, hivyo wameanza kuchukua hatua za kuvuna maji.

“Mwaka huu hali ya ukame imeshaanza kuonekana. Tusipovuna maji, kilimo hakiwezi kuwa cha uhakika. Tumeshaanza kujenga mabwawa mengi nchi nzima ili kukabiliana na hali ya ukame,” alisema Mndolwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Dkt. Richard Masika, ameipongeza serikali kwa juhudi kubwa zinazofanyika katika kuimarisha sekta ya umwagiliaji nchini.

Dkt. Masika ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume, uliofanyika katika ukumbi wa Midland Hotel, Dodoma.

Katika hotuba yake, Dkt. Masika amesisitiza kuwa majadiliano ya wafanyakazi katika baraza hilo sharti yaendane na malengo ya Tume, ili kuhakikisha malengo ya serikali katika kuinua uzalishaji kupitia kilimo cha umwagiliaji, yanafikiwa.

Aliongeza kuwa ushirikiano na nidhamu ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo hayo.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi,Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mhandisi Said Ibrahim, alisema katika taarifa walizopitia zinaonyesha kuwa wananchi wamepokea miradi ya umwagiliaji kwa furaha kubwa. Alisema miradi hiyo imekuwa ikiwagusa wananchi moja kwa moja kwani inalenga kuimarisha kipato chao kupitia shughuli za kilimo.

“Tunaamini kwa kazi kubwa iliyofanyika, wananchi wataendelea kuiunga mkono serikali kwani imewafanyia mambo makubwa ambayo yanachechemua uchumi wao,” alisema Saidi Ibrahim.