Mradi wa Membe Kunusuru SGR

Dodoma: Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amesema kuwa kasi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan bado inandelea katika miradi ya umwagiliaji na kwamba kila mkoa utafikiwa.

Mndolwa amesema miradi yote inaendelea vyema na itakamilika kwa wakati lengo likiwa kuwawezesha wakulima nchini kulima kilimo biashara chenye tija na kuachana na kilimo cha mazoea kinachotumia nguvu nyingi lakini manufaa yake ni madogo.

Mkurugenzi Mndolwa amesema hayo katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ilipotembea Mradi wa Bwawa la Umwagiliaji Membe mkoani Dodoma.

“Sisi Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji tuna nafuu sana. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na miradi yote inaendelea.

“Rais Samia anatekeleza kwa vitendo ahadi zake, kila mkoa utafikiwa na miradi ya umwagiliaji na uchimbaji wa visima, yote ni kuhakilisha serikali inawawezesha wakulima kupata tija, nchi iwe na chakula cha uhakika na ziada tuuze nje, ” alisisitiza.

Mndolwa alisema mathalani kwa sasa Mkoa wa Manyara kuna miradi yenye thamani ya sh bilioni 80 inatekelezwa ukiwamo uchimbaji wa mabwawa na visima vya umwagiliaji, ufugaji wa samaki na utalii.

Akizungumzia Mradi wa Membe uliokamilika kwa zaidi ya asilimia 90, Mndolwa alisema bwawa hilo lenye ujazo wa lita bilioni 12 ambalo lina uwezo wa kumwagilia hekta 2,500 likikamilika litanufaisha watu zaidi ya 1,500.

Alisema mradi huo ni kati ya miradi 22 ukikamilia utawawezesha wakulima kulima na kuvuna mwaka mzima badala ya kusubiri kuvuna kwa msimu.

‘Kubwa zaidi mradi huu ni kati ya miradi ya kimkakati wenye lengo la kudhibiti miundombinu ya Reli yetu ya Kisasa ya SGR isiharibike kwa mafuriko.

“Sote ni mashahidi eneo la Kilosa kila mwaka tunashuhudia uharibifu mkubwa unaotoka na mafuriko. Ukipita na SGR katika eneo hilo kuna maporomoko mengi ya maji na chanzo chake ni hiki lakini ujenzi wa Bwawa hili utasaidia maji kupugua na reli yetu kuwa salama kutoka na maji hayo. “

Alisema ujenzi wa mradi huo una faida kuu tatu, moja ni killimo na ufugaji ukiwamo wa samaki, utalii na uboreshaji wa miundombinu.

Alieleza kuwa, mradi huo utaokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumiwa na serikali kwa wanachi wa Kilosa kuokoa maisha, kununua chakula na kukarabati miundombinu mara kwa mara.

Katibu Tawala Msaidizi Sekfa ya Uchumi, Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba alisema changamoto kubwa kwa jiji la Dodoma ni maji na kwamba ujenzi wa bwawa hilo ni fursa kubwa kwani litasababisha wakulima kulima kwa uhakika.

“Mwaka huu Mkoa wa Dodoma tumepata mvua pungufu jambo ambalo ni hatari kwa kilimo chetu, lakini kuwepo kwa bwawa hili kutabadili kilimo chetu kiwe cha biashara na hali ya uchumi wa mwananchi mmoja itaboreka na hatimaye kuongeza pato la taifa,” alifafanua Aziza.