Bunge limepitisha “Azimio la Bunge” linaloitaka Serikali ipambane ili kukomesha viashiria vyote vya udini nchini mwetu. Ni Azimio zuri.
Kinachogomba hapa ni kasi ya Serikali yetu katika kushughulikia mambo makubwa na yanayoashiria kuwapo mpasuko katika Taifa. Serikali imekuwa legelege mno. Kuanzia kwenye kitongoji hadi Ikulu, hakuna anayetaka kulaumiwa!
Azimio hili limekuja baada ya maafa yaliyosababishwa na bomu lililorushwa kanisani mjini Arusha.
Mtiririko wa matukio ya nyumba za ibada za Wakristo kushambuliwa, yanaongezeka. Tatizo la Serikali mara zote limekuwa ukimya wake. Wakati mwingine inafanya mambo, lakini kwa ukimya, wananchi, hasa wale wanaoshambuliwa, wamelazimika kuamini kuwa hakuna kinachofanyika.
Azimio la Bunge lina udhaifu. Udhaifu wenyewe ni pale wabunge wanapojiaminisha kuwa dhima ya kupambana na uharamia huu ni ya vyombo vya dola pekee. Serikali inapaswa kuongeza kasi ya kushughulikia taarifa inazopewa. Hatuwezi kukaa kimya mitaani kwetu tukajiaminisha kwamba wajibu wa kutokomeza viashiria vya udini ni wa Polisi, Usalama wa Taifa, na kadhalika. Tunajidanganya. Hii ni kazi yetu sote.
Kwa msingi huo, na kwa kuamini kuwa dhima ya mapambano haya ni ya kila mmoja wetu, nimefika Mtaa wa Hombolo, Area ‘C’ mjini Dodoma. Hapo nimeshuhudia maduka mawili ya nyama (bucha). Bucha moja ipo upande wa kushoto, nyingine ipo upande wa kulia. Ukitazama maandishi na nakshi kwenye maduka hayo, utaona yalicholenga (angalia picha). Inawezekana bucha hizi zikawa zinamilikiwa na mtu mmoja, au zaidi.
Hoja yangu kwenye picha hizi, hata kama bucha zinamilikiwa na mtu mmoja, ni haya majina yake. Hii bucha ya kwanza inaitwa “New Salumu Butcher”. Nyingine inaitwa “Justine Butcher”.
Kwanza, naomba ieleweke hapa kwamba kila mtu ana haki ya kutumia jina analotaka (la kiungwana) kwenye biashara yake. Jina la biashara ni utashi wa mtu. Ndiyo maana tulizoea kuona kuna bucha zenye majina kama vile Kongwa, Kyagata, Sumbawanga, Kishapu, Oldonyo, Zenj, n.k. Mara nyingi tulizoea kuona majina ya bucha yakiendana na kule kunakopatikana ng’ombe wengi au inakotolewa nyama. Hali kama hiyo tumeishuhudia pia kwenye mazao. “Mchele wa Kyela”, “mchele wa Mbarali”, “ndizi Bukoba, ndizi Moshi”, n.k.
Sina kumbukumbu ya hapo awali kusoma jina la bucha ikiitwa Juma, Joseph, Abdallah, Halima, Julius au Ali! Sikumbuki. Hizi bucha za “Salumu” na “Justine”, zinanishawishi niamini kuwa zimepewa majina haya kutokana na vuguvugu hili la udini linaloendelea kuivuruga nchi yetu. Tena basi, kwanini majina haya yawe kwenye bucha mpya? Laiti kama yangekuwapo tangu miaka ile ambayo hatukuwa na fukuto hili, ningeweza kuelewa.
“New Salumu” na “Justine Butcher”, hata kama ni mali ya mtu mmoja, ni viashiria vya udini. Ni viashiria kwa sababu bucha moja ina jina ambalo linatumiwa zaidi na Waislamu, na nyingine ina jina ambalo utalikuta zaidi kwa Wakristo. Hii ina maana kwamba wateja katika bucha hizi wanashawishiwa kununua nyama kutokana na “ipi bucha ya mwenye imani kama yao”. Haya yametokea mkoani Mwanza na Geita ambako wapuuzi wachache walidiriki kuandika kwenye bucha zao maneno kama “Islam Butcher” na wengine “Christian Butcher”.
Ndugu zangu, kama kweli Serikali imedhamiria kutekeleza Azimio la Bunge la kutokomeza viashiria vya dini, sioni kwa nini ifumbie macho bucha za aina hii. Naomba ieleweke hapa kwamba kabla ya vuguvugu hili, kuna wafanyabiashara waliotumia majina yao kwenye biashara, zikiwamo za mabasi, na kadhalika. Lakini sidhani kama ni busara wakati huu wa sekeseke la udini kupamba moto, kuruhusu mambo kama haya kwenye bucha na kwingineko.
Wiki kadhaa zilizopita niliandika kwenye ukurasa huu kile kilichonipata mjini Geita. Nikiwa huko niliugua tumbo. Hali ikawa mbaya. Nikaenda katika zahanati moja ya Kikristo. Nikatakiwa kwenye fomu nitaje jina, kabila na dini. Nikawa radhi kutaja jina langu. Kwenye suala la dini na kabila, nilikataa. Mhudumu alipozidi kunishinikiza, niliondoka. Nikawasiliana na daktari wangu. Akaniandikia dawa. Nikaenda kuzinunua katika duka la dawa. Kiutaratibu ilipaswa nimwone daktari, lakini niliona heri dhambi ya kutomwona daktari kuliko hii ya kuulizwa dini na kabila. Dawa nilizonunua ziliniponya.
Ndugu zangu, mambo kama haya yapo hadi polisi na katika nyumba za kulala wageni. Polisi unaulizwa kabila. Tanzania ya leo yenye mwingiliano wa kuoleana, sidhani kama kuna umuhimu mkubwa wa kujua kabila la mtu. Sana sana kama kuna utafiti unaoendeshwa, sawa. Nyumba ya kulala wageni unaulizwa kabila lako! Hivi kama nikifia ndani ya nyumba hiyo, kabila langu litasaidia nini? Anuani yangu ya makazi haitoshi? Mbona kuna Wakurya ambao hawajawahi kukanyanga Mkoa wa Mara? Kujua kabila la mtu ndani ya nyumba ya kulala wageni kunasaidia nini? Haya mambo tunapaswa kuyaondoa. Tuyaondoe katika mahakama, polisi, hospitali, katika nyumba za kulala wageni, na kwingineko.
Yaruhusiwe tu pale ambako, kwa mfano, Wizara ya Afya au hospitali inapotaka kujua kwanini kabila fulani linakumbwa na mtindio wa ubongo, kwanini kabila fulani linapata maambukizi ya ukoma, na kadhalika. Kwenye utafiti sidhani kama kujua kabila au asili ya mtu ni tatizo sana.
Ndugu zangu, tuna sababu zote za kushiriki mapambano, si tu dhidi ya udini, bali aina zote za ubaguzi katika Taifa letu. Kama wengi walivyosema, huu si wakati wa kunyoosheana vidole, bali ni wakati wa kushikamana kuhakikisha kuwa sifa ya Tanzania ya kuitana “ndugu”, tunaiendeleza.
Kwa upande wa wanahabari, tuna wajibu mkubwa katika mapambano haya. Tumeanza kukiuka maadili kwa kuandika mambo ambayo hapo awali tulizuiwa kwenye miiko ya uandishi. Tunafanya kosa kubwa kuandika habari za ugomvi kwa kutaja kabila moja dhidi ya kabila jingine, au kuandika mlinzi wa kabila…ameua watu wa kabila fulani. Tunaporipoti habari za aina hiyo tutumie tu wafugaji, mlinzi, mtu fulani, na kadhalika. Kutaja makabila au dini wakati wa kuripoti habari zenye vimelea vya chuki, ni kuzidi kumwaga petroli kwenye moto ambao umeshaanza kuwaka.
Tumeishi pamoja kwa miaka mingi kwa upendo wa hali ya juu bila kujali tofauti zetu za kiimani. Juzi tu, rafiki yangu mmoja ambaye si wa dini yangu, amemsaidia mdogo wangu kupata matibabu nje ya nchi. Tunasaidiana kwa hali na mali bila kujali tofauti zetu za dini. Kuna nyumba nyingi za Wakristo ambao wana watumishi Waislamu.
Mara zote, hata kama Wakristo ni 10 na Mwislamu ni mmoja, linapokuja suala la kuchinja, hutafutwa Mwislamu ili hawa 10 wasimkwaze Mwislamu mmoja. Huo ndiyo udugu na huko ndiko kuvumiliana. Tufanye kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa mahali salama.
Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunarejea kwenye misingi tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa letu. Tukianza kuchinjana, hakuna nchi, katika ukanda huu, itakayohimili kuhifadhi Watanzania wote hawa. Kwa hili la bucha za “Salumu” na “Justine”, tunasubiri kuona kama kweli Azimio la Bunge linatekelezwa.
Mungu Ibariki Tanzania