Na Isri Mohamed, JamhuriMedia
BAADA ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba vs Tanzania Prison uliomalizika kwa mnyama kufungwa mabao 2 kwa 1 akiwa nyumbani, mjadala mkubwa ulioibuka ni kiwango cha golikipa Aishi Manula ambaye alianza golini akibezwa kuwa ameshuka kiwango na hakustahili kuanza bora angeendelea kubaki Ayoub Lakred.
Ni kweli mpira unauma sana na maumivu yake wakati mwingine huleta hasira zinazomfanya mtu kuzungumza lolote lile, ila kwa hili la Manula tuoneni aibu kidogo, cha kushangaza maneno hayo yanasemwa na Watanzania ambao wamemshuhudia Manula katika ubora wake kwa zaidi ya misimu miwili mfululizo kwenye klabu na timu ya taifa ina maana mnataka kusema jina la ‘Tanzania One’ ameitwa kimakosa.
Aishi Salum Manula bado ni Tanzania one, bado ni Golikipa mzuri tena sana Makosa ni sehemu ya mchezo hakuna mchezaji asiyekosea .
Mnapojaribu kumpandisha Ayoub msimshushe Air manula , ni kweli kwenye mchezo wa jana kuna makosa kayafanya kwa uzoefu wake angeweza kufanya kitu bora zaidi ya kile kwenye hilo simtetei lakini narudia tena makosa ni sehemu ya mchezo.
Huyu Ayoub ambaye hivi sasa kila mtu anamuona bora kuliko Manula, mbona alifanya makosa kwenye mchezo dhidi ya Power Dynamos pale nchini Zambia kila mtu alimkataa Mashabiki wa Simba walitamani Aishi Akae golini hata akiwa bado hajapona.
Kipindi Ayoub anafanya yale makosa sio kwamba alikuwa anafanya kwa makusudi kulikuwa na sababu zilizomfanya afanye vile ikiwemo ugeni, ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza ligi ya Tanzania akitokea Morocco, lilikuwa ni suala la muda tu kurejea kwenye ubora wake ambao mnamuona nao hivi sasa
Hata kwa Manula ni kipindi cha mpito tu, anayoyapitia wote tunajua ni kwa muda mrefu alikuwa nje kwa sababu ya majeraha amerudi amekutana na ratiba ngumu mara mechi ya derby ya kariakoo, baada ya hapo aliumia tena alivyorudi AFCON hii hapa , kwa hiyo ni suala la muda atarejea kwenye ubora wake, kinachoendelea hivisasa kazini kwake haimaanishi ameisha, ni mapema mno kumkatia tamaa.