Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya thelathini kujeruhiwa katika maandamano ya Alhamisi yaliyoenea nchini Kenya kupinga mapendekezo ya nyongeza ya ushuru. Madaktari walisema mwathiriwa alivuja damu hadi kufa baada ya kupata jeraha la risasi katika mji mkuu, Nairobi.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema wanane kati ya waliojeruhiwa walikuwa katika hali mbaya. Makumi ya watu walikamatwa wakati wa maandamano yaliyofanyika katika miji kadhaa.
Waandamanaji hao vijana wanapinga nyongeza ya ushuru iliyomo katika mswada tata wa fedha, ambao ulisomwa kwa mara ya pili bungeni. Wanahoji kuwa ushuru huo utaathiri uchumi na kulemea Wakenya wanaohangaika kujikimu kimaisha.
Maamlaka Huru ya Kusimamia Shughuli za Polisi nchini Kenya IPOA imesema itafanya uchunguzi kuhusu ufyatuaji wa risasi wakati wa maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha 2024.