Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa baada daladala waliokuwa wamepanda kuligonga treni katika makutano ya barabara na reli eneo la Kamata jijini Dar es Salaam.

Ajali hiyo imetokea leo saa 12 asubuhi Mei 18, 2023 wakati daladala hilo linalofanya safari zake kati ya Machinga Complex na Kigamboni kugonga treni katika eneo hilo.

Kamanda wa Kikosi cha Reli Tanzania, Sebastian Mbuta amesema kuwa daladala hilo lilikuwa linatokea Machinga Complex kuelekea Kigamboni likiwa na abiria, liligonga treni iliyokuwa katika majaribio ya kwa ajili ya kuanza safari baadaye.

“Chanzo cha ajali ni dereva la daladala kukaidi amri ya mshika kibendera aliyekuwa akisimamisha magari ya pande zote mbili ili kuruhusu treni hiyo kupita. Wakati daladala inakatiza tayari magari mengine yalishasimamishwa.

“Huyu dereva alikaidia amri akiamini kwamba kwa mawazo yake ataweza kuiwahi treni, baada ya kuigonga kuna abiria mmoja alifariki papo hapo. Majeruhi katika ajali ni 15 kati ya mmoja amevunjika mkono wa kushoto,” amesema Kamanda Mbuta.

Mbuta amesema majeruhi hao kwa sasa wanapatiwa na matibabu katika hospitali ya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na hali zao zinaendelea vizuri, akisema baadhi yao walipata michubuko midogo.