Mlipuko katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Pakistan la Khyber Pakhtunkwa umeua zaidi ya watu 40, maafisa wamesema.

Mlipuko huo ulitokea katika mji wa Khar unaokaliwa na kabila la Wabajaur, ambao uko karibu na mpaka kati ya Pakistan na Afghanistan. Ulitokea Jumapili alasiri wakati wa mkutano wa wafanyakazi wa chama cha kidini, Jamiat Ulema Islam (JUI).

Akizungumza kwa njia ya simu na VOA, afisa wa afya wa wilaya Dk Faisal Kamal alithibitisha vifo 43 na kutoa idadi ya watu 80 waliojeruhiwa. Awali, vyanzo vingine vilitoa idadi ya watu 150 waliojeruhiwa.

Afisa wa Polisi wa Wilaya ya Nazeer Khan ameiambia VOA kwamba ushahidi uliokusanywa kufikia sasa unaonyesha kuwa mlipuko huo ni kitendo cha mshambuliaji wa kujitoa mhanga.

Katika ujumbe kwenye Twitter, waziri wa mambo ya ndani wa Pakistan Rana Sanaullah alisema uchunguzi kuhusu tukio hilo uliamriwa.