Takriban watu 25 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 50 wamejeruhiwa kufuatia mlipuko wa bomu uliotokea katika stesheni ya treni ya Quetta, jimbo la Balochistani nchini Pakistani. Mlipuko huo ulitokea wakati treni ya abiria iliyokuwa imejaa watu ikijiandaa kuondoka mapema asubuhi.

Kundi la wanamgambo la Balochistan Liberation Army (BLA) limekiri kuhusika na shambulio hilo, ambalo polisi wametathmini kuwa lilitekelezwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga. Jimbo la Balochistani limekumbwa na ongezeko la mashambulizi hivi karibuni, huku kundi la BLA likidai kuwa linapigania uhuru na udhibiti wa rasilimali za eneo hilo.

Kamishna wa jiji la Quetta amethibitisha idadi ya vifo, ikiwemo mshambuliaji, na kueleza kuwa bomu hilo lilikuwa na uzito wa kati ya kilo sita na nane za vilipuzi. Raia wa kawaida pamoja na wanajeshi wameathirika, huku hofu na taharuki zikitanda katika eneo hilo.

Afisa mwandamizi wa polisi, Muhammad Baloch, ameiambia BBC kuwa mlipuko huo ulikuwa wa ghafla na wenye athari kubwa. Video zinazosambaa mitandaoni zinaonesha wakati mlipuko ulipotokea, na hali ya taharuki ikitawala miongoni mwa watu waliokuwa katika harakati za kuabiri treni hiyo.

Shuhuda Aelezea Tukio la Kutisha Mmoja wa manusura, Abdul Jabbar, aliyekuwa akielekea kwenye stesheni baada ya kununua tikiti, alisema alihisi kama amekutana na “siku ya hukumu”. Alisema, “Siwezi kuelezea hofu niliyokumbana nayo leo, ilikuwa kana kwamba siku ya hukumu imefika.”