Na Deodatus Balile, Beijing
 
Wiki iliyopita katika safu hii nimeeleza kuwa nimeanza kuandika makala zinazohusiana na viwanda. Nimesema nimeingalia familia ya Watanzania, nikaangalia ugumu wa kazi wanazofanya na aina ya kipato wanachoweka kibindoni, basi nikapata hamu ya kuhakikisha angalau nahamasisha Watanzania 1,000 wanamiliki viwanda.
Naushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini hapa, Ubalozi wa China nchini Tanzania na taasisi ya Bill Gates ya Marekani walioamua kufadhili safari yangu ya kurejea hapa nchini China kuendelea kudadisi na kudurusu suala la kilimo cha muhogo. Nimefika Beijing jana. Tangu niliporejea Tanzania nikitokea nchini hapa Oktoba, mwaka jana niliandika makala za kutosha juu ya fursa ya kilimo cha muhogo.
Ni kwa bahati mbaya Wizara ya Kilimo haikuonyesha mwamko nilioutaraji kuchukua nafasi na fursa iliyopatikana ya kuuza muhogo nchini China. Hapa katikati nimepumzisha makala za muhogo kidogo, lakini nilitaka nipate fursa ya kujifunza kutoka kwa nchi mbalimbali juu ya nini wanachofanya kuhusiana na muhogo.
Sitanii, sasa nimepewa fursa ya kuja tena hapa China kujifunza mchakato mzima wa muhogo kuanzia hatua ya kupanda, kuvuna, kuuchakata hadi kupata bidhaa ya mwisho. Nitakuletea kwa awamu utaalam walionao wenzetu. Moja tu naweza kudokeza kuwa nimekwishaona mashine za kusindika muhogo. Tangu unatoa muhogo shambani ukaanza kusafishwa, kumenywa, kukatwa vipande, kukaushwa, kusagwa na kupakiwa kwenye viroba ukiwa unga tayari kuliwa mashine hii inatumia saa 4 tu.
Nimekumbuka adha tuliyokuwa tunapata hapo kijijini kwetu Nyanga, Bukoba (M) siku tukitaka kula ugali wa muhogo. Ilitubidi kuuchimbua muhogo, kuumenya, kuusafisha, kuuloweka siku sita, baadaye tunauanika si chini ya siku 6 kama kuna jua kali, kisha tunapata makopa ambayo tunatwanga kwa mchi ndani ya kinu, kisha tunatumia chekecheo (akachechebo) kupembua kati ya unga na punje maana kinu na mchi si sawa na mashine.
Kwetu mpaka upate ugali unahitaji siku 15 za kuchakata muhogo, tena viroba viwili tu, lakini kwa wenzetu hapa ni saa 4 umechakata tani 2 au zaidi kulingana na ukubwa wa mashine. Teknolojia yao ni rahisi, bei za mashine zao si za kukatisha tamaa kama za Ulaya. Nimekuja kujifunza na hakika nitaleta mrejesho si katika muhogo tu, bali pia katika mitambo mingine inayorahisisha maisha.
Sitanii, nchi yetu haiwezi kupiga hatua yoyote ya maana ikiwa bado tutategemea jembe la mkono na kiwanda cha ‘siasa na majungu’ kufanikisha pato la kiuchumi. Siasa tumefanya za kutosha. Wakati umefika sasa tujikite katika viwanda tubadili mwelekeo wa uchumi wa nchi yetu. Nafahamu kuna waliopinga wazo langu hili.
Nimewasiliana na wengi baada ya makala ya wiki iliyopita. Aliyenitoa jasho ni mmoja wa wasomaji aliyeniambia hatuwezi kuanza na viwanda tukafanikiwa, bali kwa mawazo yake tuanze na kukuza lugha na utamaduni kisha viwanda vitakuja vyenyewe.  Huyu sikusita kumwambia bado anawaza siasa mkondo ninaosema tutoke huko.
Msomaji kaa mkao wa kula. Nitahakikisha nakuletea kila chembe ya taarifa zenye manufaa kiuchumi hatua kwa hatua, utakuwa na hiyari ya kuzichukua au kuziacha, ila naamini ukizichukua na kuzifanyia kazi, kamwe hutajuta. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ubariki ushirikiano wa China.