Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Google anahofia kwamba taarifa za kijasusi za Akili Mnemba zinaweza kutumiwa na magaidi au ‘majimbo matapeli’ kuwadhuru watu wasio na hatia.

Eric Schmidt aliiambia BBC: “Hofu halisi niliyo nayo sio ile ambayo watu wengi huzungumza kuhusu AI – ninazungumza juu ya hatari kubwa.”

Bilionea huyo wa teknolojia, ambaye alishikilia nyadhifa kuu katika Google kutoka 2001 hadi 2017, aliambia kipindi cha Leo “Korea Kaskazini, au Iran, au hata Urusi” inaweza kupitisha na kutumia teknolojia hiyo vibaya kuunda silaha za kibaolojia.

Alitoa mwito wa uangalizi wa serikali kwa kampuni za kibinafsi za teknolojia ambazo zinaunda miundo ya AI, lakini akaonya kuwa udhibiti wa kupita kiasi unaweza kukandamiza uvumbuzi.

Bw Schmidt alikubaliana na udhibiti wa mauzo ya nje wa Marekani kwenye microchips zenye nguvu ambazo zinatumia mifumo ya hali ya juu zaidi ya AI.

Kabla ya kuondoka madarakani, Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden alizuia usafirishaji wa microchips kwa nchi zote isipokuwa 18, ili kupunguza maendeleo ya wapinzani kwenye utafiti wa AI.