Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amewataka wataalamu wa afya wilayani humo kutoa elimu ya njia sahihi za kunyonyesha watoto.

Amesema elimu hiyo itawawezesha kinamama kupata kizazi chenye afya bora na kushiriki vyema masuala ya uchumi na kijamii kwa siku zijazo.

Ameyasema hayo leo Agosti 7 muda mfupi mara baada ya kufunga maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji watoto duniani yaliyofanyika mjini humo kwa ngazi ya wilaya ya Kisarawe.

Hii ni kazi ya kwanza kwa Jokate tangu ateuliwe na kuapishwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe.

“Uongozi wa Serikali kwa ngazi zote mnapaswa kuweka misingi imara na kuhamasisha jamii yetu ili itilie maanani kunyonyesha watoto kikamilifu.”

Jokate amewakumbusha waajiri kuzingatia sheria za ajira zinazowataka kuwapa likizo ya uzazi ya siku 84 ili waweze kunyonyesha watoto wao kikamilifu.

“Hii si kwa upande wa kinamama pekee bali hata kinababa nao wanapaswa kupewa likizo ya uzazi ya siku tatu pindi wake zao wanapojifungua na hizo siku wanapaswa wazitumie kuwapa misaada mbalimbali wake zao ili waweze kunyonyesha watoto wao kikamilifu,” alisema Jokate.

Awali mratibu wa lishe wilayani humo, Mwanaharusi Issa alisema takwimu zinaonyesha kuwa watoto wenye umri wa miaka mitano wenye utapiamlo mkali katika wilaya ya Kisarawe ni asilimia 0.7 huku wenye utapiamlo wa kadri ni asilimia 13.6.

Mwanaharusi amesema ili kupunguza tatizo la utapiamlo lililopo, wataalamu wa afya wanatakiwa kumuelekeza mama jinsi ya kumpakata mtoto na kumweka kwenye titi ipasavyo mara baada ya kujifungua.

Pia kumuelekeza mama aliyejifungua jinsi ya kukamua maziwa yake ili mtoto aweze kupatiwa pindi anapokua mbali.

Naye meneja wa mradi wa chakula na lishe kutoka shirika lisilo la kiserikali la Feed the Children, Silvia Imalike amesema takwimu za utafiti wa hali ya kidemografia na afya uliofanyika mwaka 2015 zinaonyesha kuwa asilimia 59 ya watoto wa umri wa miezi 0 hadi miezi 6 nchini wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee.