Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Shinyanga

Mkuu wa Shule ya Sekondari Chambo iliyopo katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Zaharani Patrombeyi (44,) amekufa baada ya kunywa kitu kinachodhaniwa kuwa ni sumu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, SACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio ambapo amesema tukio hilo lilifanyika Januari 29, 2025, majira ya saa 5 asubuhi katika kijiji na kata Chambo, Tarafa ya Dakama.

SACP Magomi ameeleza kuwa baada ya mwalimu huyo kunywa kimiminika alizidiwa na ndipo alipokimbizwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa ajili ya matibabu lakini alipoteza maisha Januari 31 majira ya asubuhi.

Amesema kuwa uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea kwani hakuacha ujumbe wowote kuhusiana na tukio hilo.

“Alijaribu kujiua kwa kunywa kitu kinachosadikika kuwa ni sumu ambacho bado tunasubiri uchunguzi wa daktari, na kwa bahati mbaya sana majira ya asubuhi mwalimu huyo amefariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama,” amesema Kamanda Magomi.

Aidha, SACP huyo amesema kuwa jaribio la kujiua ni kujichukulia sheria mkononi na endapo mwalimu huyo asingefariki basi angeshtakiwa kwa kujaribu kujiua kwa sababu ni kosa kisheria.