Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan amewavisha nishani mbalimbali Majenerali, Maafisa na Askari wa JWTZ jijini Tanga tarehe 04 Desemba 2024.

Nishani hizo ni pamoja na Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Nne, Nishani ya Utumishi Uliotukuka, Nishani ya Utumishi Mrefu, Nishani ya Utumishi Mrefu na Tabia Njema, na Nishani ya Miaka 60 ya JWTZ.

Aidha, Jenerali Mkunda amewavisha nishani ya Jumuiya ya SADC Maafisa na Askari walioshiriki Ulinzi wa Amani nchini Msumbiji chini ya mwavuli wa Jumuiya hiyo.

Jenerali Mkunda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kwa kufanikisha Wanajeshi kutunukiwa Nishani na pia amewapongeza Maafisa na Askari wa Kanda ya Tanga kwa kutunikiwa Nishani hizo.

Amewataka kuendelea kulinda Mipaka ya Nchi na Kufanya Mafunzo na Mazoezi ya hali ya juu pamoja na kuyaishi Mambo Manne kwa Mwanajeshi ambayo ni Nidhamu, Uaminifu, Uhodari, na Utii ili waweze kutimiza Majukumu ya Ulinzi wa Nchi kwa ujumla.