Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi- Dar es salaam

Mkutano wa Umoja wa askari wa kike duniani (IAWP-international Association of Women Police) kanda ya Afrika unatarajiwa kufanyika jijini Dar es salaam kuanzia Julai 22-29, 2023 ambapo utaambatana na mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo askari wa kike na watekelezaji sheria wa bara la Afrika.

Akiongea na askari wa kike ambao ni washiriki wa Mkutano huo kutoka chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) Mkuu wa Chuo hicho kamishna msadizi mwandamizi wa Polisi SACP Dk. Lazaro Mambosasa amewataka askari hao Kwenda kushiriki Mkutano huo ambapo amewaomba kujifunza kutoka kwa askari wengine wa mataifa ya Afrika na Ulaya ambao watashiriki Mkutano huo uliolenga kujenga mahusiano na mashirikiano katika mapambano ya uhalifu Afrika.

SACP Dk. Mambosasa ameongeza kuwa katika Mkutano huo askari hao wanayo nafasi ya kuwaoneshe ukarimu wageni kama ilivyo desturi ya Jeshi hilo ikiwa ni Pamoja na kutangaza utalii kwa askari hao ambao watashiriki Mkutano huo, amebainisha kuwa kufanya hivyo watakuwa wamemsadia Amiri Jeshi Mkuu Dk. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza vivutio vya utalii hapa Nchini.

Kwa upande wake Mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP Pili Fobbe ambaye ni kaimu matroni kutoka chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) amemshuru Mkuu wa Chuo hicho kwa kuwapa nasaha ambazo watazitumia katika mkutano wao uliobeba kauli mbiu isemayo “huduma kwa jamii kupitia uwezeshaji wa wanawake katika utekelezaji wa sheria”.

Amesema Mkutano huo utawapa fursa ya kuwajengea uwezo katika mambo ya ulinzi wa amani, uongozi pamoja na maswala ya uhalifu wa kimtandao ambapo amebainisha kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea mbinu na kuongeza maarifa katika kukabiliana na uhalifu katika bara la Afrika.

Nae mwanafunzi wa kozi ya uofisa Christer Kayombo ambae ni mshiriki katika Mkutano huo amebainisha kuwa kutokana na ushiriki wa mataifa mbalimbali katika Mkutano huo watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na uelewa wa namna ya kushughulika na uhalifu wa aina mbalimbali katika bara la Afrika.