Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amerejea nchini baada ya kushiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi, uliofanyika nchini Malawi.
Kabla ya kurejea Tanzania, Mhe. Kombo aliagwa rasmi na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Balozi Agnes Kayola pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Mwayiwawo Polepole, kama ishara ya mshikamano kati ya mataifa hayo mawili.
Mkutano huo ulianza tarehe 25 Februari 2025 kwa kikao cha maafisa waandamizi kutoka pande zote mbili na kuhitimishwa tarehe 26 Februari 2025 katika ngazi ya mawaziri.
Katika mazungumzo ya JPCC, Tanzania na Malawi zilijadili maeneo muhimu ya ushirikiano, yakiwemo biashara, afya, ulinzi na usalama, mawasiliano, na miundombinu, kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kijamii.
Mafanikio makubwa yalipatikana katika mkutano huo, ikiwa ni pamoja na kusainiwa kwa hati ya makubaliano katika sekta ya afya na mkataba wa kuhamishiana wafungwa kati ya mataifa hayo mawili, hatua inayotarajiwa kuimarisha mifumo ya haki na usalama wa raia.
Mkutano huu umeendeleza uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Malawi, kufungua fursa mpya za maendeleo, na kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.

