Mkutano wa APIMONDIA kuipaisha Tanzania sekta ya ufugaji nyuki, utalii
Na Wilson Malima JAMHURI MEDIA Dar es Salaam.
Mkutano mkuu wa 48 wa Shirikisho la wafuga nyuki duniani (APIMONDIA) umeipa nafasi Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano la Kongresi ya 50 ya shirikisho hilo.
Akizungumza mbele ya vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki ametangaza kuwa utafanyika nchini mwaka 2027 jijini Arusha.
“Tumetangazwa Septemba 8, mwaka huu, jijini Santiago Chile kuwa tumekuwa washindi wa kuandaa kongamano hili,” amesema Kairuki.
Amebainisha kuwa kongresi hiyo itahudhuriwa na watu 6000 watakaoshiriki kwenye mkutano, hatua anayotaja kuwa inaenda kulinufaisha taifa.
“Mataifa mbalimbali kutoka duniani yatashiriki, hivyo kupitia mkutano huu Tanzania itachochea ukuaji wa sekta ya nyuki na uhifadhi utaongezeka.”amesema.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwamo wafuga nyuki nchini kujiandaa kikamilifu kwa mkutano huo, pia amewataka kutumia fursa hiyo kuvutia wawekezaji watakao ongeza tija ya ufugaji nyuki nchini pamoja na kuimarisha biashara ya mazao ya nyuki.
“Tanzania inao uwezo wa kuzalisha asali zaidi ya tani 138,000 kwa mwaka, kiwango kinachozalishwa kwa sasa ni tani 32,691 tu. Natoa wito kwa wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta hii,” amesema.
Tanzania imeibuka mshindi kwa kupata kura 65 baada ya kuzibwaga nchi za; China, Togo na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Shirikidho hili lilianzishwa 1895 na Tanzania ilijiunga na kuwa mwanachama mwaka 1984. Kwa sasa lina nchi wanachama 113 kote duniani.