Mkutano wa Kawaida wa 43 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unatarajiwa kufanyika jijini Bujumbura, Burundi tarehe 23 Februari 2023.
Mkutano huo ambao umeanza kwa Ngazi ya Wataalam tarehe19 hadi 20 Februari 2023 utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 21 na 22 Februari 2023 na kuhitimishwa na Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 23 Februari 2023.
Mkutano wa Wataalam utapitia na kujadili agenda mbalimbali muhimu kuhusu masuala ya mtangamano wa Jumuiya hiyo ambazo baadaye zitawasilishwa kwenye Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 21 na 22 Februari 2023 kwa majadiliano na hatimaye agenda hizo zitawasilishwa kwenye Mkutano ngazi ya Mawaziri unaotarajiwa kufanyika jijini hapa tarehe 23 Februari 2023.
Miongoni mwa agenda hizo ni pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vilivyopita katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na forodha, miundombinu, ulinzi na usalama, sheria, utalii, ajira na utawala na fedha; Kupokea taarifa ya mwaka ya Ukaguzi wa Hesabu za Jumuiya kwa mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022; Taarifa ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya; Taarifa kuhusu Taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2023.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Ngazi ya Wataalam unaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi. Ujumbe huo pia unajumuisha Wajumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Katiba na Sheria.
Kadhalika Mkutano huo umehudhuriwa na Wajumbe kutoka nchi zote wanachama ambazo ni Burundi ambaye ni mwenyeji wa mkutano, Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini ambao wameshiriki kwa njia ya mtandao.