Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar
Mkutano wa Jukwaa la Kitaifa la Uziduaji unatarajiwa kufanyika jijini Dodoma kati ya Novemba 24 hadi 25, 2022.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa HakiRasilimali, Adam Anthony, mkutano huo wanauandaa ili kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya uziduaji kukutana na kujadili kwa umakini, kubadilishana uzoefu, kujifunza kwa ajili ya kuendeleza uwazi na uwajibikaji katika sekta hiyo.
“HakiRasilimali ni mtandao wa mashirika 17 yanayotetea masuala muhimu na ya kimkakati katika sekta ya madini, mafuta na gesi asilia. Shirika linaamini katika uwazi na uwajibikaji wa sekta ya uziduaji kwa ustawi wa Watanzania wote.
“Jukwaa la Uziduaji linalenga kushawishi uundaji wa sheria na sera bora, usimamizi bora wa mapato ya sekta ya uziduaji na kuhamasisha sauti za jamii katika kujihusisha na michakato ya sekta ya uziduaji na kujenga ushirikiano utakaokuza maendeleo endelevu kwa Watanzania,” amesema Anthony alipozungumza Novemba 15, 2022 kuhusu mkutano huo.
Vilevile amesema tangu mwaka 2010, asasi za kiraia zinazofanya kazi katika sekta ya madini, mafuta na gesi hapa nchini Tanzania zimekuwa zikiandaa mkutano ya majadiliano ya kitaifa ya kila mwaka katika sekta uliofahamika kama ‘Tanzania Mining Indaba’.
Hata hivyo, amesema tangu mwaka 2019 mkutano huo ulibadilika jina na kuitwa Jukwaa la Uziduaji na katika mikutano yote majadiliano muhimu yamefanyika katika kuendeleza mifumo ya ushauri kati ya azaki, serikali, bunge na kampuni za uziduaji katika kuboresha utawala wa sekta hiyo.
Amesema matokeo ya majadiliano haya ni pamoja na ahadi za serikali kufanyia kazi masuala yanayohusiana na jamii ili kupunguza athari zinazosababishwa na uwekezaji katika uziduaji kama vile kucheleweshwa kwa fidia ya ardhi na ukiukwaji wa haki za binadamu hasa wanawake katika mnyonyoro wa thamani wa sekta hiyo.
Amezitaja mada zitakazojadiliwa katika mkutano wa mwaka 2022 wa Jukwaa la Uziduaji kuwa ni ‘sekta ya uziduaji; ujenzi wa uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu’.
Nyingine ni uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji, utawala wa kudumu na uwekezaji, madini ya kimkakati na mchango wake katika nishati nchini Tanzania, changamoto na matatizo ya jamii katika sekta ya uziduaji, jinsia na uziduaji na siasa za kimataifa katika sekta ya uziduaji.
“Lengo kuu ni kuwaleta pamoja wadau katika sekta ya uziduaji kwa ngazi zote kujadili kwa kina, kubadilishana uzoefu na kujifunza ili kuendeleza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji na kuunda mifumo endelevu ya ukuaji wa sekta unaochagizwa na asasi za kiraia. Yote haya ni katika juhudi za kufikia dira ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2025.
“Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na Wizara ya Madini na taasisi zake, Wizara ya Nishati na taasisi zake, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Kampuni za Uziduaji, washirika wa maendeleo, balozi mbalimbali, azaki, mashirika ya jamii, Mashirika ya Dini, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, vyama vya madini vya mikoa, wachimbaji wadogo na vyombo vya habari,” amesema.