Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salam

Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Dkt. George Fasha, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, tarehe 30 Novemba 2024, ameshiriki katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Usimamizi wa Shughuli za Bandari Mashariki na Kusini mwa Afrika (PMAESA), zilizofanyika Serena Hotel, jijini Dar es Salaam.

Sherehe hizi za Jubilei ya miaka 50 ya ubora na mabadiliko ya utendaji wa shughuli za kibandari kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika pia zimehusisha uzinduzi rasmi wa Kitabu cha Mwongozo wa Umoja huo.

PMAESA inasherehekea Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ni Umoja uliojikita katika kuboresha utendaji kazi wa Bandari na kushughulikia changamoto mbalimbali muhimu ili kuhakikisha ubora katika shughuli za utekelezaji bandarini na huduma bora za usafirishaji kupitia Bandari zilizo chini ya Wanachama wake zinatatuliwa ipasavyo.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Mwenyekiti wa PMAESA, Wakili Msomi Modjadji Phyllis Difeto, na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum.