Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Gabriel Fuime, amewataka wakazi wa Ilala kujitokeza kwa wingi kushiriki sensa ya watu na makazi inayofanyika kuanzia Jumapili wiki hii. Fuime aliiambia JAMHURI mwishoni mwa wiki kuwa kuna umuhimu mkubwa wa wakazi wa Ilala kujitokeza kwenye sense, kwani bila kufanya hivyo mgawo wa fedha kutoka serikalini utapungua.
“Nataka wakazi wa Ilala walifahamu hili. Mgawo wa dawa kitaifa unategemea idadi ya watu. Ilala tuna watu wengi wanaoshinda mchana na kurejea kwao jioni, kwani ndipo makao makuu na ndipo zilipo ofisi zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tunalifahamu hili tatizo la kupata wageni zaidi ya 400,000 mchana wanaoondoka jioni, lakini sasa tunapaswa kufahamu ni wangapi wanalala Ilala. Idadi ya watu ndiyo inayotumika kutoa mgawo wa dawa kitaifa.
“Pili bajeti ya maendeleo ya kiwilaya msingi wake ni idadi ya watu katika halmashauri. Idadi ya watu ndiyo inayotumiwa kutoa fedha za maendeleo. Hivyo mtu anapokuwa hajahesabiwa ina maana tunapunjwa katika mgawo wa fedha wa kitaifa,” alisema Fuime.
Alisema mipango ya maendeleo kama ujenzi wa miradi ya barabara, maji, umeme, shule, hospitali na mingine inategemea idadi ya watu wanaoishi katika wilaya husika, hivyo kadiri Ilala itakavyokuwa na wakazi wengi ndiyo itakavyopata fedha nyingi za maendeleo.
Alitolea mfano wa nchi ya Nigeria kuwa baadhi ya wananchi nchini humo walikuwa na utaratibu wa kuhesabiwa mara mbili hadi tatu, hii ikiwa na maana kwamba wakifanya hivyo wanaifanya mikoa wanayotokea kuonekana ina idadi kubwa ya watu na hivyo kupewa fedha nyingi, lakini akashangaa kusikia baadhi ya watu wanapanga kususia sensa kwa hapa nchini.
Mkurugenzi huyo alisema sensa itasaidia kuratibu na kuimarisha mifumo ya utambuzi wa raia kama vitambulisho vya taifa, anwani za makazi na mifumo mingine itakayolinganishwa baada ya sensa kufahamu kwa uhalisia nani anaishi wapi.
Sensa ya watu na makazi itafanyika Jumapili Agosti 26 kwa wananchi wote waliolala kwenye nyumba yoyote ile siku ya Jumamosi kuamkia Jumapili na uhesabuji utaendelea hadi Septemba 2, 2012. Makarani watakuwa wakipita nyumba hadi nyumba na kuchukua takwimu za wahusika.