Na Ashrack Miraji, JamhuriMedia, Muhez
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mheza, mkoani Tanga Dkt Jumaah Mhina, ametoa wito kwa wananchi wa Kata ya Kwabada walioendeleza mashamba Katika shamba la Lewa na Saguras ambao bado hawajalipia hati zao za ardhi kuhakikisha wanalipia ili waweze kupatiwa hati za maeneo yao.
Lengo la hatua hii ni kuondoa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa kikwazo kwa maendeleo katika wilaya hiyo.
Akizungumza leo Machi 25, 2025 ofisini kwake, Dkt Mhina alisema kuwa zoezi la ugawaji wa hati litafanyika tarehe 26/3/2025, na litahudhuriwa na mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Mbunge wa Jimbo la Muheza, Hamisi Mwimjuma. Viongozi mbalimbali wa ngazi ya mkoa na wilaya pia wanatarajiwa kushiriki katika hafla hiyo.
“Ni furaha yangu kuwaalika wananchi wote wa Kata ya Kwabada kufika mapema katika zoezi hili la ugawaji wa hati. Ni zoezi lenye manufaa kwa jamii yetu na linafanyika kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ili kuondoa migogoro ya ardhi, ambayo imekuwa changamoto kubwa kwa Wilaya yetu,” alisema Mhina.

Hadi sasa, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza imefanikiwa kupima mashamba 150, ambapo hati 35 tayari zinakwenda kugahiwa Kwa wananchi. Hati 25 bado zipo katika hatua za mwisho za utengenezaji na zinatarajiwa kugawiwa hivi karibuni.
“Zoezi hili ni endelevu, na tumejizatiti kuhakikisha tunamaliza migogoro ya ardhi katika wilaya yetu. Kwa kushirikiana na ofisi ya Kamishna wa Ardhi, tunatekeleza muongozo wa Serikali kuhakikisha kila eneo linapata hati ya kumiliki,” aliongeza Mhina.
Mhina alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imejizatiti kuondoa migogoro ya ardhi nchini kote, na kwamba Wilaya ya Muheza itakuwa mfano wa utekelezaji wa sera hii.
Aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kuwaahidi kuwa haki ya kumiliki ardhi itatolewa kwa wote walio na sifa, kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Serikali.
“Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwaondoa wananchi katika migogoro ya ardhi, na tutaendelea kuhakikisha kila mwenye haki anapewa haki yake. Hii ni chachu kwa wilaya yetu, kwani zoezi hili litahakikisha wananchi wanamiliki mashamba yao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa,” alisema Mhina.
Mkurugenzi Mhina pia alikiri kuwa migogoro ya ardhi imesababisha matatizo makubwa, lakini alisema kuwa utekelezaji wa mpango huu utatoa mwanga wa matumaini kwa wananchi wa Muheza.
Aliwahakikishia wananchi kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha migogoro hiyo inaondoka kabisa, huku haki ya kumiliki ardhi ikiwa ni kipaumbele