Uchunguzi uliofanywa na gazeti JAMHURI umebaini taarifa nyingi za uonevu katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Uonevu na ubabe wa Mkurugenzi, Madeni Kipande, haukuishia kwa wafanyakazi pekee, bali anaburuza hadi wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.
Hali hii inahujumu uchumi wa nchi. Baada ya kuona hatari inayolinyemelea Taifa, mmoja wa wakurugenzi aliamua kuwasilisha hoja ya kumuondoa Kipande madarakani, lakini kwa bahati mbaya kutokana na mizizi mizito aliyonayo Kipande, wenzake watano ndiyo walioondolewa kwenye Bodi, kwa Waziri Dk. Harrison Mwakyembe kuvunja Bodi hiyo na kuteua wateule awapendao. Ifuatayo ni taarifa husika katika tafsiri isiyo rasmi. Endelea….
Utangulizi:
Ndugu Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kuiomba Bodi ya Wakurugenzi kuniruhusu kuwasilisha hoja mbele ya Bodi hii tukufu, kuhusiana na utendaji na mwenendo wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mhandisi Madeni Kipande.
Inawezekana huu ni uamuzi mgumu na wenye kuumiza tutakaopaswa kuufanya tangu kuanzishwa kwa Bodi yetu; na pengine ni uamuzi ambao kila mmoja wetu binafsi au kwa pamoja tutabaki kukumbuka hatua tutakayoichukua leo — iwe nzuri au mbaya.
Ndugu Mwenyekiti,
Katika kufikia uamuzi, naomba tufuate taratibu sahihi kufikia uamuzi katika ngazi ya Bodi, kwamba nipewe fursa ya kuwasilisha hoja yangu, na baada ya hapo Mwenyekiti aulize iwapo hoja hii inaungwa mkono.
Ikiwa hoja itaungwa mkono, kila mmoja wetu apewe fursa ya kutoa maoni juu ya hoja iliyopendekezwa na mwisho aseme iwapo anaiunga mkono au la. Wakati wa mjadala wakurugenzi wapo huru pia kuwasilisha hoja mbadala inayoweza pia kufikiriwa na Bodi.
Baada ya kumaliza mjadala, natarajia nitapewa fursa ya kujibu swali lolote au ufafanuzi au kurekebisha hoja yangu. Baada ya hapo, hoja hii inaweza kupigiwa kura rasmi au vinginevyo inaweza kuhitimishwa kutokana na mjadala wa wakurugenzi iwapo imekubaliwa au la. Ikikubaliwa na wengi, hoja hii itakuwa azimio rasmi la Bodi ya Wakurugenzi.
Uongozi na Mfumo wa Uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania
Ndugu Mwenyekiti,
Naomba nizungumzie juu ya mfumo wa uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania kama unavyooneshwa kwenye Sheria ya Bandari ya Mwaka 2004. Mifumo hii imeainishwa katika Ibara ya 6, 7 na 34 za sheria hiyo.
Bodi ya Wakurugenzi
Ndugu Mwenyekiti,
Niruhusu nianze kuzungumza kidogo juu yetu, Bodi ya Wakurugenzi.
Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania imeanzishwa chini ya Sheria ya Bandari ya Mwaka 2004, Ibara ya 6, inayosema hivi:-
“6 (1) Kutakuwamo na Bodi ya Wakurugenzi ambayo itawajibika kusimamia (kuongoza) biashara na masuala ya Mamlaka.
(2) Bodi itajumuisha:-
a) Mwenyekiti atakayeteuliwa na Rais;
b) Wajumbe wasiopungua watano au wasiozidi wanane watakaoteuliwa na Waziri miongoni mwa watu wenye uzoefu katika uongozi.
(3) Jedwali la kwanza la Sheria hii litasimamia mwenendo na masuala mengine yanayohusiana na Bodi. Jedwali la Kwanza limeambatanishwa kama Kiambatanisho Na. 1.
Ndugu Mwenyekiti,
Ibara 6. (1) iliyorejeshwa hapo juu inaonesha wazi kuwa Bodi ya Wakurugenzi ndicho chombo cha juu katika uongozi wa biashara na masuala ya Bandari. Tuna mamlaka kisheria na mamlaka ya kusimamia biashara na masuala ya Mamlaka ya Bandari Tanzania. Hatuna kizuizi au vyovyote iwavyo chenye kuzuia mamlaka yetu.
Mamlaka ya Bodi
Ndugu Mwenyekiti,
Ibara ya 7 ya Sheria (tajwa) inatamka wazi mamlaka yaliyokasimiwa katika Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania. Inasema,
“7. (1) Kulingana na maelekezo yanayoweza kutolewa na Waziri, Bodi inaweza:-
Kazi yoyote kwa ajili ya Mamlaka, ambayo haikuwa kwenye mpango kazi uliopitishwa na Waziri ambayo gharama yake inayokisiwa haizidi kiwango kinachoweza kuamuliwa na Waziri muda hadi muda.
Fikiria mapendekezo ya sheria kuhusiana na Bandari na kushauri utungwaji wake kwa Waziri; na
Idhinisha utolewaji wa huduma za Bandari, au wezesha maombi ya nchi yoyote jirani na nchi (yetu).
(2) Bodi inaweza kumpa maelekezo Mkurugenzi Mkuu kuhusiana na utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka.
Ndugu Mwenyekiti,
Kama uonavyo, ibara zilizotajwa hapo juu zinaipa uwezo mamlaka Bodi ya Wakurugenzi. Kwa nyongeza tu, na kufafanua zaidi juu ya mamlaka haya, Msajili wa Hazina, ambaye ni mlinzi wa mali zote za umma, alitoa waraka mwaka 2004 ukitoa mwongozo kwa Bodi za Wakurugenzi katika kutekeleza majukumu yake.
Waraka huo umesambazwa tena hivi karibuni kuonesha kuwa bado una umuhimu hadi sasa. Baadhi ya mambo yaliyomo kwenye walaka huo yanaeleza mamlaka ya Bodi za mashirika:
Kuweka sera itakayoongoza Menejimenti katika kutekeleza madhumuni ya Shirika kwa kuzingatia sera iliyowekwa na Serikali kwa sekta inayohusika.
Kupitisha uamuzi kuhusu ajira na nidhamu za wafanyakazi wote wa Shirika kuanzia kwa Mtendaji Mkuu hadi wale wa ngazi ya Mkuu wa Idara.
Kuwajibika na rasilimali za Shirika, na kuhakikisha udhibiti wa utunzaji na utumiaji wa fedha na mali za Shirika.
Kuweka miongozo ya utekelezaji wa sera (Policy Guidelines/directives) itakayofuatwa na Shirika katika utendaji kazi wa kila siku.
Kuongoza Menejimenti katika shughuli za utekelezaji kwa kutoa maelekezo yanayohitajika bila kujiingiza katika utendaji wa siku hadi siku. Nakala ya waraka wote imeambatanishwa kama kiambatanisho Na. 2.
Ndugu Mwenyekiti,
Kwa mamlaka yote haya tuliyopewa kushindwa kutekeleza majukumu tutakuwa tunajiangusha wenyewe.
Mamlaka ya Bodi Kuteua Kamati
Ndugu Mwenyekiti,
Sheria ilikwenda mbali zaidi kwa kuipa Bodi mamlaka ya kuunda au kuteua kamati miongoni mwa wajumbe wake, na kama hivyo zitakuwa na mamlaka kamili ya Bodi ya Wakurugenzi. Ibara ya 8 ya Sheria inasema hivi:-
“8 (1) Mamlaka inaweza kuunda na kuteua miongoni mwa wajumbe, idadi ya kamati kadiri itakavyoona inafaa, kwa nia ambayo mamlaka itaona inarahisisha utendaji kupitia kwenye Kamati.
(2) Bodi inaweza, kulingana na hali au vizuizi kama itakavyoona inafaa, kufuta kamati yoyote au mwajiriwa wa Mamlaka ambaye majukumu au mamlaka yake kwa mujibu wa Sheria hii au sheria nyingine yoyote, isipokuwa tu mamlaka ya kuagiza au kutoza kodi, kuweka viwango au kukopa fedha.
(3) Mamlaka yoyote au majukumu yaliyokasimiwa, hivyo yanapaswa kutekelezwa na Kamati kwa niaba ya Mamlaka.
(4) Bodi inaweza kutekeleza mamlaka yoyote iliyopewa au kutekeleza jukumu lolote chini ya sheria hii au sheria nyingine, bila kujali ukasimuji wa mamlaka na kazi zilizofanywa.
Kwa mara nyingine, mamlaka yote haya tuliyopewa, Bodi ya Wakurugenzi hatuna kisingizio chchote kushindwa kutekeleza jambo lolote lililopo mbele yetu.
Mgongano wa Maslahi
Ndugu Mwenyekiti,
Sheria imeweka msisitizo mkubwa katika suala la mgongano wa maslahi miongoni mwa Bodi au watumishi wa Mamlaka, na hili linapaswa kuchuliwa kwa uzito mkubwa. Ibara ya 10 ya Sheria inasema:
“10 (1) Kwa madhumuni ya sheria hii, Mjumbe wa Bodi au mwajiriwa wa Mamlaka atachukuliwa kuwa na mgongano wa maslahi ikiwa anayo maslahi maalum au binafsi yanayoweza kugongana na utendaji halisi wa mhusika au matumizi ya mamlaka yake kama mjumbe wa Bodi au mwajiri wa Mamlaka.
(2) Ikitokea wakati wowote mjumbe wa Bodi au mwajiri wa Mamlaka akawa na mgongano wa maslahi kuhusiana na:-
(a) Suala lolote linaloshughulikiwa na Mamlaka au kuamriwa au,
(b) Suala lolote ambalo Mamlaka kwa busara inataraji litafikishwa mbele yake kwa nia ya kufikiriwa au kufanyiwa uamuzi, mjumbe au mwajiri huyo mara moja anapaswa kutangaza maslahi aliyonayo kwa wajumbe wengine wa Bodi au Mkurugenzi Mkuu na kujizuia kushiriki au kuendelea [kushiriki] mchakato au uamuzi wa suala hilo.
(3) Mara tu mamlaka inapopata taarifa za mgongano wa maslahi wa aina yoyote, inapaswa kufanya uamuzi iwapo mgongano huo unaweza kuingilia utendaji sahihi na wa majukumu ya mamlaka au uwezo wa mamlaka, na mwajiriwa ambaye ana mgongano wa maslahi hapaswi kupiga kura juu ya mwenendo wa kuamua.
(4) Mjumbe wa Bodi au mwajiriwa wa Mamlaka atachukuliwa kuwa na mgongano wa maslahi ikiwa:-
(a) atasindwa bila sababu ya msingi kutangaza maslahi inavyotakiwa;
(b) kwa makusudi akitoa tamko la uongo au lenye kupotosha akiwa na nia ya kushawishi uamuzi kufikiwa.
Ndugu Mwenyekiti,
Ni matumaini yangu kuwa katika mkutano huu leo, kati yetu hakuna kwenye mgongano wa kimaslahi ambao utazuia uwezo wake wa kufanya uamuzi bila upendeleo. Na iwapo yeyote kati yetu anao mgongano wa kimaslahi halisi au wa kufikirika, inatarajiwa kuwa atatangaza hali hiyo kwa ufasaha.
MKURUGENZI MKUU
Ndugu Mwenyekiti,
Kama ilivyo kwa Bodi ya Wakurugenzi, nafasi ya Mkurugenzi Mkuu inaanzishwa chini ya Sheria ya Bandari ya Mwaka 2004. Ibara ya 34 ya Sheria inasema:
“34 (1) Atakuwapo Mkurugenzi Mkuu atakayeteuliwa na waziri kutoka miongoni mwa orodha ya watu watatu waliopendekezwa na Bodi.
(2) Mtu hatakuwa na sifa za kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu isipokuwa tu:-
(a) awe mhitimu wa chuo kikuu kinachotambulika.
(b) awe na angalau uzoefu wa miaka 10 katika eneo moja au zaidi la uongozi, uendeshaji wa bandari, sheria, uchumi, fedha, sayansi au injinia, na;
(c) awe na uzoefu wa masuala ya bandari
(4) Mkurugenzi Mkuu atateuliwa kwa kazi hiyo kwa mujibu wa masharti na vigezo kama vitakavyowekwa katika barua yake ya uteuzi, au kama Bodi ya Wakurugenzi inavyoamua na uamuzi huo kukubaliwa na waziri katika nyakati tofauti.
(5) Mkurugenzi Mkuu atakuwa Katibu wa Bodi.
Ndugu Mwenyekiti,
Mambo makuu matatu yanaweza kuchukuliwa kwa muhtasari kutokana na Ibara ya 6 na 7 ya Sheria hii:
Mkurugenzi Mkuu anawajibika kwa Bodi ya Wakurugenzi. Mkurugenzi Mkuu anateuliwa na Waziri kutokana na mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi. Mkurugenzi Mkuu hapigi kura katika Bodi; ni Katibu wa Bodi.
Ndugu Mwenyekiti,
Nia ya kupitia vifungu hivi vya sheria ni kujiwekea msingi wa majadiliano na mapendekezo ninayotaka kutoa leo.
Kwa muhtasari, napenda sote tutambue kuwa Sheria inatupa mamlaka ya kufanya uamuzi juu ya mambo ya Mamlaka ya Bandari Tanzania.
UTENDAJI WA INJINIA KIPANDE NA TABIA YAKE
Ndugu Mwenyekiti,
Sababu iliyonifanya niamue kuwasilisha hoja hii kwenye Bodi leo ni kwa sababu sote tunafahamu mwenendo na tabia ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Injinia Madeni Kipande.
Lakini kwa sababu mbalimbali, bado hatujachunguza hali kwa umakini na kufanya uamuzi mara moja na wa kudumu. Na hata tulipojadiliana, tulikubaliana kukuomba wewe Mwenyekiti kujadiliana naye na kumshauri juu ya mashaka yetu. Tuna uhakika mkondo huu haujaleta matokeo chanya hadi sasa.
Ndugu Mwenyekiti,
Napenda kutoa baadhi ya mifano ya utendaji na tabia za Injinia Kipande aliyeshindwa kutimiza matarajio kwa mtu anayeshika nafasi kama hii. Ifuatayo ni baadhi ya mifano hii:-
KUSHINDWA KUTEKELEZA NA KURIPOTI KWENYE BODI MAPENDEKEZO YA RIPOTI YA MBAKILEKI
Ndugu Mwenyekiti,
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, aliunda Kamati ya Uchunguzi kuchunguza chanzo cha utendaji mbovu katika Bandari, kwa mtazamo wa kupata mapendekezo juu ya hatua za kuchukuliwa kusaidia Mamlaka ya Bandari Tanzania kurejesha ufanisi na nafasi yake katika ukanda na kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.
Kamati ya Uchunguzi iliwasilisha ripoti yake kwa Waziri, na kutokana na hiyo ripoti, Waziri akafanya uamuzi mgumu wa kuvunja Bodi ya Wakurugenzi wa TPA na kuunda Bodi mpya ya Wakurugenzi. Huu ndiyo wakati tulipoteuliwa. Kwa kauli ya Waziri mwenyewe, wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi waliteuliwa kwa umakini kutoka katika orodha wajumbe tarajiwa wa Bodi.
Timu iliyoteuliwa ilitajwa kuwa na ujuzi stahiki, uzoefu, wenye utayari na uadilifu katika kutumikia Taifa letu kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania. Timu hii ilipitia hatua zote stahiki za kuchunguzwa kabla ya kuteuliwa. Kwa maana hiyo, utayari wetu kutumikia Taifa hili hautiliwi shaka.
Kazi ya kwanza iliyofanywa na Bodi mpya ilikuwa ni kupokea na kutolea uamuzi ripoti iliyoandaliwa na Mbakileki, kwani ripoti hii ilikuwa inatoa msingi wa kuchukua hatua za haraka zilizopaswa kuchukuliwa na Bodi. Bodi ilitumia muda mwingi mjini Tanga kupokea ripoti na kujadiliana na Kamati ya Uchunguzi.
Kwa mantiki hiyo, Bodi ya Wakurugenzi iliandaa kikao kingine Bagamoyo kutolea uamuzi zaidi ripoti na kukubaliana hatua za kuchukuliwa na Bodi na Uongozi kutekeleza mapendekezo ya Kamati ya Uchunguzi.
Moja ya uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi ilikuwa ni kusimamisha kazi watu wote waliokuwa wanatuhumiwa kuwa chanzo cha kudorora kwa utendaji na mambo mengine katika TPA mara moja. Na kwa maana hiyo, Bodi ilichukua hatua za kinidhamu stahiki dhidi ya wahusika.
Kwa upande mwingine, na muhimu, Bodi ya Wakurugenzi iliandaa mpango yakinifu kuelekeza maelekezo ya Uchunguzi. Katika mpango huo, Bodi ilitoa maelekezo kwa kila pendekezo la Kamati ya Uchunguzi.
Mpango wa Utekelezaji na maelekezo pamoja na ripoti vilikabidhiwa kwa uongozi wa TPA kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu kumwezesha kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote na kutoa mrejesho kwenye Bodi juu ya hatua iliyopigwa katika utekelezaji.
Hadi leo, Bodi ya Wakurugenzi haijapata mrejesho wowote juu ya utekelezaji wa maelekezo na Bodi ya Wakurugenzi ina taarifa za uhakika kwamba mapendekezo mengi yaliyopaswa kutekelezwa na Mkurugenzi Mkuu hayajatekelezwa. Kiambatanisho namba 3 kinaeleza kwa njia ya jedwali suala, mapendekezo, maagizo ya Bodi na utekelezaji wake hadi leo.
3.2 KUSHINDWA KUTEKELEZA MAELEKEZO YA BODI
Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, kama ilivyoanzishwa na Sheria ya Bandari ya Mwaka 2004 inawajibika kusimamia biashara na masuala ya bandari. Hii ina maana kuwa Bodi ya TPA ni Bodi ya Uongozi na si Bodi ya Ushauri, hivyo uamuzi unaofanywa na Bodi kupitia kwenye mkutano ya Bodi Kamili au Kamati zake unapaswa kutekelezwa na Uongozi, labda Bodi iamue vinginevyo.
Kusisitiza suala hili, Ibara ya 34 ya Sheria ya Bandari inasema:- 34 (1) Atakuwapo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, ambaye pia atakuwa Mtendaji Mkuu na atawajibika kwenye Bodi kwa uongozi sahihi na usimamizi wa majukumu na masuala ya Mamlaka.
Sheria pia inaeleza kwa uwazi katika Ibara ya 7, kwamba “7 (2) Bodi inaweza kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu kuhusiana na utendaji katika jukumu lolote la Mamlaka.
Hali ilivyo ni kuwa tangu tuteuliwe katika Bodi ya Wakurugenzi maelekezo mengi ya msingi na uamuzi wa Bodi hayatekelezwi na Mkurugenzi Mkuu na wakati mwingine anayabadili kutimiza matakwa yake. Mifano ya maelekezo ya msingi yaliyotolewa na Bodi, lakini hayakutekelezwa na Mkurugenzi Mkuu ni pamoja na:-
Kuandaa Kanuni za Kiutendaji kwa TPA
Kuajiri Mshauri kupitia mfumo wa uongozi kwa nia ya kuleta ufanisi katika nafasi za ajira. Kuajiri Mshauri wa kukagua mfumo wa ICT. Orodha ya maelekezo ya Bodi ambayo hayajatekelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu imeambatanishwa kama kielelezo namba 4.
3.3 KUKWAMISHA MPANGO WA KUAJIRI WATENDAJI WAANDAMIZI
Mfano mwingine wa Mkurugenzi Mkuu anavyodharau/kaidi Bodi ni jinsi alivyoshughulikia kazi ya kuajiri watendaji waandamizi.
Amechelewesha kutangaza nafasi hizo. Ilichukua karibu mwezi mzima tangu Kamati ya Bodi ya Masuala ya Wafanyakazi na Ajira ilikabidhi tangazo Mkurugenzi Mkuu, na kimsingi ni leo tu yalipotolewa kwenye vyombo vya habari. Mara zote Mkurugenzi amekuwa akija na visingizio na maelezo, na kisingizio cha mwisho alichotoa ni kuwa tangazo lilikuwa limepelekwa Wizara ya Uchukuzi kupitiwa kabla ya kuwekwa magazetini.
Wajumbe wa Bodi walipofuatilia wizarani, iligundulika kuwa tangazo hilo lilikuwa halijapelekwa wizarani. Ni baada ya hapo, Mkurugenzi Mkuu aliamua kulipeleka tangazo wizarani baada ya shinikizo kutoka wizarani na kwenye Bodi.
Baada ya tangazo, Mkurugenzi Mkuu anadaiwa kuwatisha wafanyakazi [wa Bandari] kuwa hakuna anayepaswa kuomba kazi yake, vinginevyo, atashughulikiwa [wote walioomba kazi hii; Hassan Kyomile na Franciscas Muindi, amewashughulikia kweli. Kyomile ameondolewa kwenye ukurugenzi wa ununuzi na kupelekwa Tanga kuwa meneja wa Bandari hiyo, wakati Mama Muindi amemsimamisha kazi wiki iliyopita kwa maelezo kuwa uchunguzi dhidi yake unaendelea]. Inaelezwa kuwa Mkurugenzi Mkuu ameagiza apewe majina ya wote walioomba nafasi yake.
Kama mnavyokumbuka, Bodi ya Wakurugenzi iliamua kutafuta msaada wa taasisi ya kusimamia mchakato wa ajira kusaida katika kuchambua na kusaili, na tuliamua kuelekeza uongozi kutangaza kwa maslahi ya taasisi kufanya kazi hii.
Taratibu za ununuzi zilifuatwa sawia, na kama sehemu ya ununuzi, Mkurugenzi Mkuu alitakiwa kujiuzulu [kwa kuwa aliomba kazi hii] kabla ya taasisi hii kupewa kazi ya usaili. Mkurugenzi Mkuu alifanya nini? Alikataa kujiuzulu, alipiga kura ya turufu dhidi ya uamuzi na maelekezo ya Bodi.
Kwa mara nyingine, mtizamo wa Bodi ulikuwa kutafuta maridhiano naye na mchakato ulilazimika kuanza upya kutafuta taasisi ya kusaidia mchakato.
Hii peke yake tu, imechelewesha mchakato mzima kwa uchache miezi mitatu, hivyo kuchelewesha juhudi za kujaza nafasi haraka kadiri inavyowezekana.
Kama vile hiyo haitoshi, wakati wa mkutano wa Bodi uliofanyika Agosti 24, 2013 Mkurugenzi Mkuu alitoa kauli za wazi kuonesha nani hamtaki [Katika Bodi ya Wakurugenzi] kushiriki katika mchakato wa ajira alipomkataa wazi Dk. Hilderbrand Shayo kushiriki.
3.4 KUSHINDWA KUENDELEZA UHUSIANO MZURI KATI YA WAFANYAKAZI, WATEJA NA BODI YA WAKURUGENZI
Katika ngazi ya Mtendaji Mkuu wa taasisi, muhimu zaidi si utaalamu ulionao, bali uwezo wa kufanya kazi na watu. Injinia Madeni Kipande amethibitisha mara kwa mara kwamba hana uwezo wa kushirikiana na watu, hivyo anajipotezea sifa ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi muhimu kama hii yenye wafanyakazi zaidi ya 3,000.
Kama Mtendaji Mkuu alitarajiwa kuimarisha uhusiano na wafanyakazi, wateja na wadau wengine, lakini amekuwa kinyume na hali hii. Wakati tukifahamu kuwa kila binadamu ana udhaifu wake, hivyo si rahisi mtu kuelewana na kila mtu, lakini kwa Injinia Kipande kuelewana na mtu yeyote ni jambo la pekee kutokana na kanuni alizojiwekea kwamba yeye, kila mtu ni mbaya, mwizi, Chadema, anatokana na kabila fulani au dini fulani, hivyo hampendi na ni sehemu ya uongozi uliopita na kadhalika.
Tumesikia malalamiko mengi kutoka kwa wateja, marafiki, wadau, watumishi na pia tuna ushuhuda wetu kama wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ambapo mara kadhaa Injinia Kipande ametumia lugha isiyo na staha dhidi yetu, na wakati mwingine matusi.
3.5 KUWACHANGANYA WAFANYAKAZI WANAWAKE
Kama nyongeza juu ya mtazamo wake kuhusiana na watu, Injinia Kipande ana mwenendo wa pekee wa kutoheshimu, kuchanganya au pia kutukana watumishi wanawake ambayo ni kinyume na mkakati wa kuwawezesha wanawake katika uongozi [ameshinikiza hadi Bodi ya Wakurugenzi ya sasa haina Mkurugenzi mwanamke hata mmoja kati ya wakurugenzi sita].
Kama tunavyokubaliana kuwa wanawake, sawa na wanaume, wanaweza kuwa na udhaifu wao na wanaweza kutenda makosa ya kinidhamu, lakini tulichokiona kwa Injinia Kipande sicho unachokitarajia kutoka kwa mtu anayeshikilia nafasi kama hii.
Ninayo mifano angalau minne ya wanawake waliolalamika rasmi kwenye Bodi ya Wakurugenzi juu ya kutendewa ndivyo sivyo na Injinia Kipande katika kipindi cha miezi sita tu iliyopita. Hawa ni Francisca Muindi, Janeth Ngowi, Winnie Mulindwa na Vulfrida Teye. Barua za malalamiko kutoka kwa wanawake hawa waliotajwa zimeambatanishwa kama kielelezo Na 5.
Nafahamu wanawake wengi zaidi ambao wangependa kulalamika, lakini bado hawajapata nguvu ya kuja kwetu, hasa hasa baada ya kubaini kuwa waliokuja kwetu wamesulubiwa zaidi [wengi amewasimamisha kazi].
Ndugu Mwenyekiti,
Sote tunafahamu juhudi ulizofanya kuwasuluhisha Injinia Kipande na mama Muindi. Unafahamu ilivyokuwa rahisi kumfanya mama Muindi kuahidi kufanya kazi kwa moyo mkunjufu chini ya Injinia Kipade. Lakini pia unafahamu ilivyokuwa ngumu kumshawishi Injinia Kipande kukubali kufanya kazi kwa amani na mama Muindi.
Pia tunafahamu kilichotokea ulipotoa taarifa kwenye Bodi ya Wakurugenzi katika mkutano uliofanyika Tanga kuwa umefanikiwa kusuluhisha mgogoro kati ya Injinia Kipande na mama Muindi, pale Injinia Kipande bila heshima yoyote juu ya juhudi zako na mkutano uliofanya naye, aliposema kuwa kamwe hatafanya kazi kwa amani na mama Muindi, kwake, hii ni vita inayopaswa kuendelea kwa muda wote atakaokuwa TPA.
Leo sote tu mashuhuda wa manyanyaso yanayoendelea dhidi ya mama Muindi kutoka kwa Injinia Kipande, na hadi sasa sisi kama Bodi tumeshindwa kutimiza wajibu wetu kama sehemu mbadala na wasuluhishi wa mwisho. Na hii yote inatokana na majivuno ya Injinia Kipande, ambayo kwa muda mrefu tumeyavumilia au kuyaruhusu!
Sifahamu nini kilitokea kutokana na malalamiko ya mama Mulindwa na mama Ngowi, lakini nina uhakika mambo hayakuisha kwa heri upande wao. Karibuni tumepokea malalamiko rasmi kutoka kwa mama Vulfrida Teye, ambapo sote tunafahamu kuwa ameendelea kumtaja kama mtu mbaya. Anafika mahala anakwenda kinyume na misingi ya haki ya msingi, ambayo kila mtu anahesabiwa hana kosa hadi inapothibitika!
Nia ya kuleta hoja hii si kumlinda yeyote, lakini ninaona mwelekeo ambapo wanawake wanaondoka kwa kasi katika nafasi za viongozi waandamizi bandarini chini ya uangalizi wetu.
Katika mkutano wa Bodi uliopita wa Agosti 24, 2013 sote tulikuwa mashahidi kuwa Injinia Kipande alikuwa akiwasiliana na Mkuugenzi wa Huduma za Sheria, Kokutulage Kazaura, kwa kutumia kauli ambazo hukutarajia Afisa Mtendaji Mkuu kuzungumza na kiongozi wake mwandamizi mbele ya Bodi ya Wakurugenzi. Hakuna anayeweza kushangaa ukisikia kesho amefukuzwa na hakutakuwapo mwanamke katika viongozi waandamizi wa Bandari.
Ndugu Mwenyekiti,
Mtakumbuka kuwa wakati wa vikao vya nidhamu juu ya watumishi kadhaa wa TPA, Bodi ya Wakurugenzi ilitoa uamuzi juu ya Maka Marcelina Kisanko kutoka Idara ya ICT, na tuliagiza arejeshwe kazini, lakini ashushwe cheo kuwa Afisa Mwandamizi badala ya meneja.
Ndugu Mwenyekiti,
Ikikupendeza, unaweza kufahamishwa kuwa hadi sasa, uongozi umekataa kumrejesha kazini na hivyo yupo nyumbani baada ya maelekezo ya Bodi kutolewa [tangu Mei 13, 2013 ilipoamuriwa arejeshe kazini, hadi leo bado Kipande amekataa kumrejesha, anamlipa mshahara bila kufanya kazi]. Hii inahusisha yote kukataa kutekeleza maelekezo ya Bodi na kukatisha tamaa watumishi wanawake.
3.6 MKATABA NA e-CTN
Injinia Kipande aliilazimisha TPA kuingia kwenye mkataba (uliobatizwa hati ya makubaliano) na kampuni ya Ubelgiji kutoa huduma ya ilichokiita Electronic Cago Tracking Note (e-CTN – Mfumo wa kufuatilia mizigo kielektroniki). Alifanya hivyo bila kufuata taratibu za ununuzi wa umma ikiwamo kutokuwapo zabuni.
Injinia Kipande pia alikataa kusikiliza ushauri wa kisheria uliotolewa na Idara ya Huduma za Kisheria ya TPA, ushauri uliotolewa na Kurugenzi ya Ununuzi na Ugavi na ushauri kutoka kwa viongozi wengine wa TPA.
Kwa nyongeza, alikataa wito na mwaliko wa Msimamizi, SUMATRA, kujadiliana katika suala hili kabla SUMATRA haijatoa uamuzi wake.
Hata baada ya Bodi ya Wakurugenzi kuelekeza uongozi kuachana na mkataba huu, Injinia Kipande aliendelea na alizungumza na vyombo vya habari akisisitiza kuwa wanaopinga mfumo huu ni maaduni wa TPA, msemo alioutumia dhidi ya baadhi ya Wakurugenzi wa Bodi katika kuamua suala hili. Nakala ya mkataba wa e-CTN imeambatanishwa kama kielelezo Na 6.
3.7 KUSHINDWA KUTEKELEZA VIPAUMBELE VYA MSINGI VYA BODI YA WAKURUGENZI
Ndugu Mwenyekiti,
Utakumbuka kuwa Bodi ya Wakurugenzi kwa muda sasa imekuwa ikijifunza kazi za msingi za TPA, hivyo imeamua kuweka vipaumbele vya msingi kwa ajili ya miezi sita ya awali au kwa ajili ya mwaka 2013, na hivyo ndivyo vilistahili kuwa vipaumbele vya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari au vingekuwa msingi wa kujadiliana na vipaumbele kati ya Bodi na uongozi.
Injinia Kipande alikabidhiwa rasmi vipaumbele hivi katika mkutano wa Bodi na baada ya majadiliano kuhusiana na muda wa utekelezaji yalifanyika marekebisho kuingiza mapendekezo yake. Baada ya hapo, mapendekezo hayo yamewekwa kabatini, na anaendelea kutekeleza anachodhani ni muhimu; maelekezo ya Bodi hutekelezwa kwa bahati tu yanapoangukia katika anachodhani kuwa ni muhimu.
Kwa mara nyingine, hii inathibitisha dharau [ya Kipande kwa Bodi ya Wakurugenzi] isiyopaswa kuvumiliwa tena. Vipaumbele vya Bodi vimeambatanishwa kama Kielelezo Na 7.
3.8 KUCHELEWESHA MPANGO WA MATOKEO MAKUBWA SASA (BRN)
Mpendwa Mwenyekiti,
Sote tunakumbuka aibu tuliyopata kama wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA katika warsha iliyoandaliwa na Wizara ya Uchukuzi katika Hoteli ya White Sands Agosti 22, 2013. Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Injinia Kipande, alikiri mbele ya Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dk. Harrison Mwakyembe, kwamba TPA ilichelewa kufahamishwa juu ya Mpango wa BRN, na hivyo basi TPA haijachukua hatua yoyote kutekeleza Mpango Kazi wa BRN.
Inapaswa kufahamika hapa kuwa alichofanya Injinia Kipande mbele ya Bodi ya Wakurugenzi kwa Waziri, ilikuwa ni uongo. Injinia Kipande anafahamu kuwa [kabla ya mkutano huo] alikuwa ameshiriki katika mkutano wa usafirishaji na yeye alitia saini andiko la Mpango wa Usafirishaji chini ya BRN. Wakati huo alikuwa akiijulisha Bodi kuwa wana kazi nyingi wakishughulika na Mpango wa BRN.
Kwa nyongeza, watumishi wa TPA walikuwa wakishiriki vikao vya BRN kuhusiana na usafirishaji, hivyo TPA ilikuwa na taarifa kamili. Juni, 2013 TPA ilialikwa kwenye vikao kujadili BRN na ilituma wawakilishi kuhudhuria, wakiwamo wajumbe wa Bodi walioombwa kusambaza CD na maandiko ya BRN.
Kwa mantiki hiyo, TPA ilifahamu kila kitu kuhusu BRN ila haikutilia maanani mpango huu na hivyo haikuwa na mkakati wa kiuongozi kuhakikisha BRN inaingizwa katika mpango mkakati na utekelezaji wa TPA ilivyokubaliwa katika mpango kazi.
Matendo yake yamechelewesha utekelezaji wa malengo ya BRN na ni kutokana na uzembe wa kutekeleza vipaumbele vya Serikali.
Hii si tabia inayotarajiwa na ya kuvumiliwa kwa mtu anayeshikilia nafasi muhimu kama hii. Andiko lenye saini ya Injinia Kipande kwenye BRN limeambatanishwa kama Kiambatanisho Na 8.
3.9 KUMDANGANYA WAZIRI
Kaimu Mkurugenzi Mkuu amekuwa na tabia ya kudanganya juu ya mapato ya Bandari ya Dar es Salaam kuonesha kuwa anafanya kazi kubwa kuliko uongozi uliopita. Sote tunakubaliana kuwa uongozi uliopita ulikuwa na matatizo makubwa ya uadilifu na kiutendaji, lakini hakuna sababu ya kusema uongozi kuhalalisha uwepo wetu; utendaji wetu utathibitisha umuhimu wa sisi kuwapo au kutokuwapo.
Injinia Kipande amekuwa akimwambia Waziri kuwa mapato katika Bandari ya Dar es Salaam yameongezeka kutoka Sh bilioni 28 mwezi Juni/Julai 2013 hadi wastani wa Sh bilioni 50 Desemba 2013. Takwimu tamu kutamkika!
Hivi karibuni magazeti yamemnukuu Waziri akisema mapato ya mwezi yameongezeka kutoka Sh bilioni 24 hadi Sh bilioni 42! Chanzo cha taarifa zote hizi, hakika ni Kaimu Mkurugenzi ambapo tunafahamu kuwa Waziri anategemea taarifa kutoka kwake kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Uhalisia wa mapato kwa mwezi ni kiasi gani? Kiwango cha juu ambacho Bandari ya Dar es Salaam imepata kukusanya ni cha mwezi Januari 2013, ambapo mapato yaliyokusanywa yalifikia Sh bilioni 34.67!
Bila kujali kuwa makusanyo kwa ujumla mwaka huu yamekuwa makubwa kuliko mwaka uliotangulia, inapaswa kufahamika kuwa makusanyo ya mwaka 2012/13 kwa Bandari ya Dar es Salaam yalishindwa kutimiza lengo kwa asilimia 7.44 sawa na Sh bilioni 26.38.
Ikiwa mtu anaweza kumpa taarifa za uongo Waziri, na kumruhusu Waziri kutoa taarifa hadharani kwa taarifa potofu kwa nia, hapaswi kuvumiliwa kwa siku moja zaidi. Nakala ya mapato ya TPA ikionesha makusanyo kwa mwaka 2012/2013 imeambatanishwa kama kielelezo Na. 9.
3.10 KUTOHESHIMU SHERIA ZA KAZI
Injinia Kipande amekwenda mbali na kuvuja sheria za kazi kwa matendo yake. Amekwenda kinyume na sheria zote mbili; Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Mwaka 2004 na Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002.
Hii inaweza kuthibitishwa kutokana na maelekezo yake kuwa nafasi za Mkurugenzi wa Masoko na Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi zitangazwe kwa sababu wameomba kazi kwa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA [anayoishikilia yeye].
Hakuna mahala popote katika sheria za utumishi wa umma inakoruhusiwa, na iwapo agizo hili lingetekelezwa, ingeharibu heshima ya TPA na ingeleta mgogoro wa kazi wa hali ya juu.
Nakala ya barua kutoka kwa Injinia Kipande ikielekeza kuwa nafasi mbili zitangazwe imeambatanishwa kama kielelezo Na. 10.
3.11 TUHUMA HEWA DHIDI YA BODI YA WAKURUGENZI
Ndugu Mwenyekiti,
Kwa muda sasa Injinia Kipande ametumia mbinu ya kuchafua majina ya baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi. Amekuwa akisambaza tuhuma zisizo na msingi na uvumi kwa baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi katika utaratibu ambao usingetarajia Mtendaji Mkuu kufanya hivyo.
Nia yake ya msingi imekuwa ni kuharibu sifa za wajumbe wa Bodi kwa nia ya kuifanya jamii na hasa maafisa waandamizi wa Serikali kama Waziri mwenyewe wajenge mtazamo hasi dhidi ya Bodi ya Wakurugenzi.
Amewatuhumu baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kuwa ni Chadema au wafuasi wa upinzani, akisambaza taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa hawana uwezo katika wafanyayo, ni Wachagga, wana udini na kadhalika.
Ametumia fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali kujaribu kusambaza sumu kwao na kuna dalili kuwa baadhi wameangukia kwenye mtego wake. Nia yake imekuwa ni kuondoa heshima ya wakurugenzi hivyo watu waunge mkono maovu yake TPA.
Inawezekana Injinia Kipande hafahamu kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA ina rekodi nzuri ya utendaji katika sekta mbalimbali ambazo zimeishaitendea mema nchi yao katika nafasi mbalimbali, na ni watu wenye sifa za pekee.
Kuwatuhumu Wakurugenzi wa Bodi kama afanyavyo Injinia Kipande haijapata kutokea katika mashirika ya umma nchini Tanzania, na haipaswi kuvumiliwa kwa siku moja zaidi.
3.12 DHARAU KWA BODI YA WAKURUGENZI
Ndugu Mwenyekiti,
Kama ilivyoelezwa hapo juu, Injini Kipande si tu amekataa kutekeleza maelekezo ya Bodi katika nyakati tofauti, bali ametumia pia lugha isiyo na staha dhidi ya Wajumbe wa Bodi, kama kusema “Hamnitishi kitu”, “mna nini kunizidi mimi nyie”, “Hamna lolote” na kadhalika.
Ndugu Mwenyekiti,
Utakumbuka tabia na mwenendo wa Injinia Kipande tukiwa Dodoma, kama mfano tu. Jinsi alivyokujibu nje ya viwanja vya Bunge baada ya Kikao cha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, baadhi yetu tuliokuwa karibu nawe tulilazimika kuondoka kuepuka udhalilishaji uliotokea.
Pia utakumbuka tukio lililotokea siku Wizara ilipoandaa chakula cha jioni, jinsi alivyokuwa anakueleza masuala ya baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, mbele ya watu wengine. Alipuuza juhudi zako zote za kumtuliza.
Ndugu Mwenyekiti,
Pia utakumbuka kauli zake katika kikao na Waziri, katika ofisi ya Waziri. Mwenendo wake ulikuwa kinyume kabisa na matarajio Mtendaji Mkuu anavyopaswa kuwa kwa Bodi yake na Waziri. Hata hivyo, tulikubali kumvumilia kwa gharama dhidi yetu.
Kuna mifano yake zaidi ya 100 dhidi ya Bodi ya Wakurugenzi, na katika mifano hiyo yote wajumbe wa Bodi binafsi ama wameamua kupuuza, au kuvumilia tabia kwa matumaini kuwa ingekoma baada ya muda. Haijaacha na inazidi kuwa mbaya.
Kilele cha tabia yake mbovu kilithibitika katika Mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi uliofanyika Agosti 24, 2013 ambapo Injini Kipande alitoa kauli kwa majigambo ya hali ya juu, zisizo na staha na zenye kukaribia matusi na maneno mengine ambayo hayajawahi kutolewa na watendaji wakuu wa shirika kwa Bodi ya Wakurugenzi mbele yao.
Mwenendo wake ulionesha ukosefu wa heshima kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, na Bodi yote ya Wakurugenzi, na kwa mtazamo mpana kutoheshimu mamlaka ya uteuzi. Hii haiwezi na haipaswi kuvumiliwa zaidi.
Kwa mtazamo wangu, hii inaweza kuwa mara ya kwanza katika historia ya mashirika Tanzania kwamba Mtendaji Mkuu anawakejeli Wakurugenzi wa Bodi na anaendelea kuwa ofisini kwa siku zaidi, bila kutaja wiki nzima.
Ukiangalia historia ya matendo yake yaliyozaa kukaidi Bodi ya Wakurugenzi, inapaswa kusemwa bayana kuwa Bodi imevumilia matendo na tabia yake kwa miezi sita iliyopita.
Ndugu Mwenyekiti,
Pia tumeshuhduia jinsi Injinia Kipande anavyochagua katika Bodi nani yuko tayari kufanya naye kazi na nani hamtaki, hamheshimu na kwa uwazi anatangaza kuwa anataka waondoke kwenye Bodi.
Mpaka sasa tunafahamu kuwa idadi ya wajumbe wa Bodi ambao Injini Kipande yuko tayari kufanya nao kazi ni wachache, na inazidi kupungua siku hadi siku. Umeshuhudia kuwa iwapo mjumbe wa Bodi anatoa mawazo yake kwa uhuru juu ya njia bora ya kuendesha masuala ya TPA, na mawazo yake yakawa tofauti na anachokiamini, mtu huyo mara moja anageuka adui na wakala wa adui.
Ndugu Mwenyekiti,
Utakumbuka kuwa Bodi imekwishaeleza hofu yake kwako na tumeyajadili katika fursa kadhaa. Ni matumaini yangu kuwa leo tutatoka kwenye kulalamika kuingia kwenye vitendo.
4 HII YOTE INAMAANISHA NINI?
Katika aya zilizotangulia, nimeeleza dazeni ya masuala na mifano ya matendo na tabia ya Injinia Kipande kwa mwaka mmoja. Na haya ni yale tu kati ya machache niliyopata fursa ya kuyafahamu, lakini nina uhakika kuna mengi zaidi ya haya yanayofahamika kwa Bodi ya Wakurugenzi, au mengine ambayo sote hatuyafahamu kwa sasa. Lakini suala kubwa mbele yetu kwa sasa, ni hii yote inamaanisha nini kwa ujumla wake? Kwangu, inamaanisha masuala muhimu yafuatayo:-
4.1 UKOSEVU WA UWEZO UONGOZI WA KIMKAKATI
Ndugu Mwenyekiti,
Kwa matendo, mwenendo na utendaji, Injinia Kipande amethibitisha kuwa ana upungufu wa msingi katika uwezo wa uongozi wa kimkakati. Kwa muda wa mwaka mmoja uliopita, na kutokana na matendo, tabia na utendaji, ameshindwa kutuonesha mwono, mwelekeo na matumaini, ambayo kwa mawazo yangu ni sifa tatu za msingi kwa kiongozi wa ngazi ya aina hii.
Hadi sasa hajakutana na wadau muhimu wa biashara ya Bandari. Kwa mawazo yangu, anaiendesha TPA kama duka, gereji au usimamizi wa ujenzi.
4.2 UZEMBE WA JUMLA
Utendaji wa Injinia Kipande unaweza kusemwa kwa muhtasari kuwa ni uzembe wa jumla kwa kutokuwa na uwezo wa kutekeleza vipaumbele vya msingi vya Bodi na Taifa. Hii pia inaifanya Bodi ya Wakurugenzi nayo kuwa na uzembe wa hali ya juu ikiwa itamvumilia kwa siku moja zaidi!
4. 3 KUTOKUWA NA UWEZO
Injinia Kipande amethibitika kutokuwa na uwezo na weledi kwa kiwango ambacho matendo yake yanaifanya hata Bodi kuonekana kuwa haina uwezo. Hii ni kutokana na yeye kushindwa kutekeleza maelekezo ya Bodi ya Wakurugenzi.
Sote tunakumbuka mkutano ulioitishwa na Waziri wa Uchukuzi Aprili 18, 2013 ambao Waziri aliilaumu Bodi kwa kushindwa kutekeleza baadhi ya masuala, na ukweli kwamba tulihitimisha kwa kukubaliana kuwa udhaifu huu ulitokana na utendaji na tabia binafsi ya Injini Kipande, lakini tulionekana kama Bodi isiyo na maana. Ni matumaini yangu kuwa hatutavumilia hali hii zaidi.
4.4 UKAIDI
Sote tu mashahidi mara kadhaa ambapo Injini Kipande kwa uwazi amekaidi Bodi, kwa mjumbe mmoja mmoja na Bodi yote ya Wakurugenzi. Suala la karibuni ni hili tunalokabiliana nalo sasa.
Katika utendaji wa umma, ukaidi ni uasi. Ni matumaini yangu kuwa leo Bodi ya Wakurugenzi wa TPA itaiona na kuichukulia kuwa iko hivyo.
5. NINI KIKO HATARINI?
Ndugu Mwenyekiti,
Baada ya kusema yote haya, ni muhimu tukajiuliza leo, ikiwa hatutoi ufumbuzi wa suala hili, ikiwa hatuchukui hatua tutapoteza nini? Nini kipo hatarini?
5.1 UCHUMI WA NCHI YETU
Sote tunafahamu kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni lango la uchumi wa Taifa letu. Hivyo, sote tunawajibika kuhakikisha kuwa lango letu linafanya kazi kwa ufanisi na uaminifu wa hali ya juu. Na tusipowaonesha wanaotumia lango hili kwamba geti hili linaendeshwa kwa weledi, uchumi wetu utaumia kwa kiwango kikubwa, na tutawajibika.
5.2 UTENDAJIWA TPA
Kwa utendaji huu wa Injinia Kipande, kuna kila dalili kuwa tunaelekea kuona mshuko wa utendaji wa TPA kutokana na sababu za kupungua kwa morali ya utendaji wa watumishi na watendaji na imani, hivyo kupunguza wigo wa wateja.
5.3 UADILIFU NA KUAMINIKA KWETU
Ndugu Mwenyekiti,
Napenda kusisitiza kuwa Bodi ya Wakurugenzi kuna kila dalili tunaweza kupoteza heshima yetu kutokana na kutochukua hatua; kimsingi tayari tumeanza kupoteza heshima kwa kutoyapatia ufumbuzi masuala yaliyo wazi kwa kila mtu.
Ndugu Mwenyekiti,
Kwa kushindwa kuchukua hatua, tunaulizwa maswali kila mahala kuhusiana na heshima yetu, je, tumenunuliwa? Tumeahidiwa nini kiasi kwamba tunageuka upande mwingine wakati makosa makubwa na matusi yakitokea?
Ni matumaini yangu leo, tunapaswa kutumia fursa hii kudhihirisha nafasi yetu na kurejesha heshima.
6. WITO WA KUCHUKUA HATUA
Katika mkutano wa Agosti 24, 2013 ulisema jukumu la Bodi ya Wakurugenzi ni kulinda taasisi na nilikubaliana na wewe. Pia, nilisema katika mkutano huo kwamba kulinda taasisi inamaanisha kuisahihisha taasisi.
Ndugu Mwenyekiti,
Leo ningependa kunyumbulisha zaidi kauli hii, kwamba jukumu letu kama Bodi ya Wakurugenzi ni kulinda taasisi kwa gharama yoyote.
Hata hivyo, ningependa kusema kuwa kulinda taasisi kwa gharama yoyote haimaaanishi kuwalinda watu binafsi ndani ya taasisi kwa gharama yoyote. Kulinda watu binafsi katika taasisi kwa gharama yoyote kimsingi inaharibu taasisi unayopaswa kuilinda, na tutawajibishwa.
Ndugu Mwenyekiti,
Leo, ni uamuzi kati ya kulinda taasisi yetu, TPA kwa gharama yoyote na kulinda watu binafsi ndani ya TPA kwa gharama yoyote.
Ndugu Mwenyekiti,
Kama unavyofahamu, tumekuwa na majadiliano kadhaa kuhusu masuala haya niliyoainisha leo. Na unafahamu, tumekuomba kuwasilisha masononeko yetu kwa Injinia Kipande mara kadhaa.
Kama unavyofahamu, tumekuwa na majadiliano naye mara kadhaa, Kama unavyofahamu, tumekutana na Waziri mara kadhaa na kujadili masuala haya.
Lakini pia, tupo hapa leo tukizungumza suala lilelile tulilokwishazungumza, kwani kwa sasa hali ni mbaya kuliko awali.
Siku zilizopita, tulidhani baada ya muda mambo yangebadilika na kuwa mazuri na katika baadhi ya nyakati tumesema “tujipe muda”, na sasa “muda umetufundisha” kuwa mambo yanaweza yakawa mabaya zaidi kadiri muda unavyopita, na si kuboreka.
Ndugu Mwenyekiti,
Ni wito wa kuchukua hatua,
Ni wito wa kusimama pamoja,
Ni wito wa kuokoa Taifa letu,
Ni wito wa kutimiza wajibu wetu sasa,
Ni wito wa kurejesha mamlaka yetu,
Ni wito wa kurejesha heshima yetu iliyopotea,
Ni wito wa kudhihirisha umuhimu wetu,
Ni witu wa kutekeleza mamlaka yetu ya kisheria.
7 MAAZIMIO YANAYOPENDEKEZWA
Ndugu Mwenyekiti,
Baada ya kusema haya yote na kutokana na ukweli, ushahidi na mifano niliyowasilisha, napenda kumalizia kwa kupendekeza maazimio ambayo yakubaliwe na Bodi yako katika mkutano huu.
Ndugu Mwenyekiti,
Napendekeza kwamba, Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari ya Tanzania iamue kwamba:-
Kumsimamisha kazi mara moja Injinia Madeni Kipande, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, kuruhusu uchunguzi juu ya mambo yaliyotajwa hapo juu na mambo mengine yanayohusiana na utendaji na tabia yake tangu alipoingia Bandari.
Kuanzisha uchunguzi huru juu ya tabia na matendo ya Injinia Madeni Kipande kwa nia ya Bodi kuchukua hatua stahiki baada ya hapo.
Ndugu Mwenyekiti,
Nawashukuru wote kwa kunisikiliza na naomba kuwasilisha hoja kwa majadiliano na uamuzi.
John Ulanga,
Bodi ya Wakurugenzi, Mamlaka ya Bandari Tanzania,
Agosti 31, 2013