*Katika kumlinda Katibu Mkuu akanusha maelekezo aliyotoa Mkulo hotelini
*Soma mgongano wa kauli na nakala za mashinikizo ya Wizara ya Fedha kwa CHC
Siri nzito na zenye kuitia aibu Serikali juu ya mgogoro wa uuzaji wa kiwanja Na. 10 kilichopo Nyerere Road kwa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL) zimeanza kuvuja.
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la Jamhuri kwa wiki tatu sasa na kufanikiwa kupata nyaraka nzito kutoka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), zinafanana kwa kila hali na nakala ya nyaraka zilizopo Wizara ya Fedha, unashitua.
Mwishoni mwa wiki bila kujua kuwa Jamhuri linazo nyaraka za siri, Wizara ya Fedha na Uchumi imetoa tangazo katika baadhi ya magazeti kwa lengo la kumsafisha Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, katika kashfa ya kuuza Kiwanja Na. 10 kwa kampuni ya Mohammed Enterprises, lakini uhalisia wamemvua nguo.
Mkulo amefanya uamuzi wa ajabu kwa kuwashinikiza watendaji wa serikali kumuuzia kiwanja hicho Mohammed Enterprises.
Mgogoro wa kiwanja hiki una historia ndefu inayoanzia miaka 1990 pale kampuni kadhaa zilipokinyemelea ila zikashindwa kukinunua. Mgogoro huu ulikua zaidi baada uamuzi wa Kampuni ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kumuuzia Mohammed Enterprises kiwanja Na. 192 mwaka 2003.
Kiwanja hiki Na. 192 au Na. 11 kama kinavyojulikana sasa, kilikuwa kinatumia barabara moja na kiwanda Na. 191 kilichokuwa kinatumiwa na Kampuni ya Biashara Dar es Salaam (DRTC). Katika mazingira yasiyoeleweka DRTC iliuziwa kiwanda Na. 191 na kikaamua kuziba njia inayokwenda kiwanja cha nyumba yake ambacho ni cha METL.
Mnunuzi wa kiwanja Na 191 aliyekuwa Meneja wa DRTC, Mery Msira, alikwenda Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kupewa kibali cha kuyatoza magari ya METL Sh 500,000 kila siku ya Mungu, kwa kutumia barabara inayokatiza kwenye kiwanja chake kama ilivyokuwa awali kabla ya wawili hao kuuziwa viwanja hivi.
METL waliamua kwenda mahakamani na wakapata hati ya zuio, inayomzuia Msira kufunga hiyo njia. Alichokuwa akilalamikia Msira ni kwamba magari ni makubwa na yanamkosesha raha katika biashara na wateja wake, hivyo kufidia bughudha wanayopata ni heri wafidiwe Sh 500,000 kila siku kama ushuru wa kutumia kipande hicho cha barabara kisichofikia mita 20.