Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini mkoani Mtwara ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum) Kapteni Mstaafu George Mkuchika ametangaza rasmi kutogombea tena nafasi ya ubunge katika uchuguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu maalumu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mjini Newala, mbunge huyo wa jimbo la Newala Mjini amesema katika uchaguzi mkuu huo hatogombea tena nafasi hiyo kutokana na umri alionao kwa sasa ila bado ni mwanachama wa CCM na yuko pamoja na wana Newala.
‘’Kuacha ubunge sijamaanisha kuwa mimi siyo wa Mtwara au Newala, bado tuko pamoja na tutaendelea kushirikiana na wananewala muda na wakati wowote mtakaponihitaji ila kwa sasa kutokana na umri wangu nimeona nipumzike nikiwa bado na heshima yangu,’’amesema Mkuchika.

Hata hivyo ametoa rai kwa wanachama na wanan Nwala kwa ujumla kuwa pale inapofika muda wa kumtafuta mbunge watafute mtu sahihi atakayeendeleza vizuri jimbo hilo na kusaidia maendeleo ya Newala huku akiwashukuru kwa ushirikiano waliouonesha kwa kipindi cha miaka ishiriki sasa akiwa Mbunge.
Aidha, Mkuchika amedumu ubunge tangu Wilaya ya Newala ikiwa na jimbo moja la Newala na sasa kuna majimbo mawili baada ya kugawanywa kuwa Newala Vijijini na Newala Mjini na anaacha alama ya maendeleo makubwa kwa kupitia sekta mbalimbali kama vile maji, afya, elimu, barabara na nyingine.
Akizungumza kwa niaba ya Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Newala Mji, Yusufu Kateule amesema mbunge huyo amekuwa na upendo, huruma na uwezo mkubwa wa kufanya mambo tangu wakati likiwa jimbo moja la Newala.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo akiwemo Katibu wa Kata ya Maumbika, Ally Mbolele amemshukuru mbunge huyo kwa kuwafanyia mambo mengi makubwa wananewala na kitendo cha kutogombea tena nafasi hiyo kumewapa simanzi wanachama na wananewala kwa ujumla.
