*Asema wasikubali yawakute ya Buhemba

*Aahidi kuwatetea bungeni kwa nguvu zote

Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), amejitokeza hadharani kuwaunga mkono wananchi wa Mtwara wanaopinga kujengwa kwa bomba la gesi kwenda jijini Dar es Salaam.

Amesema anasubiri Mkutano wa Bunge utakaoanza mjini Dodoma mwezi ujao ili awatetee. Mwanasiasa huyo anaungana na wenzake kadhaa, akiwamo Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnein Murji (CCM), ambaye ametetea waziwazi uamuzi wa wananchi hao.


Kada mwingine wa CCM aliyewaunga mkono Mtwara ni Waziri Mkuu mstaafu John Malecela, ambaye amesema Mtwara wana haki ya kuanza kufaidi rasilimali hiyo.


Ametumia msemo wa, “Ukikaa karibu na waridi, lazima unukie.” Mkono ametoa msimamo wake alipozungumza na JAMHURI kwa simu akiwa nchini Marekani ambako amekwenda kufanyiwa uchunguzi afya yake.


“Nipo mbali, lakini waambie wananchi wa Mtwara nawaunga mkono asilimia mia moja. Lazima tuungane kukataa hii mikataba ya kinyang’au.


“Nawakaribisha wananchi wa Mtwara waende Buhemba katika Jimbo la Musoma Vijijini waone mashimo yaliyoachwa na hawa wanaoitwa wawekezaji. “Buhemba hawakuacha kitu… walichimba dhahabu wakaondoka. Hawakuacha hata pete, hakuna barabara, hakuna zahanati, dhahabu yote walichukua wakapeleka Afrika Kusini. Lazima tuungane kukataa mambo haya.


“Nasema fundisho lipo Buhemba, afadhali kabisa wananchi wa Mtwara wakatae, nipo mbali lakini nawaunga mkono mia kwa mia.


“Pale Buhemba kulikuwa na manyang’au, hawakuacha kitu, afadhali mkoloni alikuwa anapora mali na akawa anatuachia majengo na reli, lakini hawa hakuna kitu kabisa.


“Bungeni nitawaunga mkono wananchi wa Mtwara. Naunga mkono viwanda viwekwe pale Mtwara, kila mtu ana haki ya kuwa wa kwanza kufaidi rasilimali inayopatikana katika eneo lake.

Nasisitiza kuwa wananchi wa Mtwara waende Buhemba waone tulivyoachiwa mashimo. Wasirudie makosa kama ya Buhemba,” amesisitiza Mkono.