Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MKOA wa Pwani unatarajia kukutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na wajasiriamali kwenye Maonyesho ya Biashara ya awamu ya nne yatakayofanyika Desemba 16 hadi 20, 2024, katika viwanja vya Mailmoja, Stendi ya zamani, Kibaha.
Maonyesho hayo yatafunguliwa rasmi Disemba 17 na yataenda sambamba na Kongamano litakalofanyika Disemba 18 katika Ukumbi wa Mwl. Nyerere, Kwa Mfipa.
Akizungumza kuhusu maonyesho hayo kwenye ukumbi wa mkutano wa ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa huo, Alhaj Abubakar Kunenge, alieleza kuwa maonyesho hayo yamewahi kufanyika hapo awali mwaka 2018, 2019, na 2022.
Alisema, mwaka huu wanatarajia washiriki 550 na wageni 25,000 kutembelea maonyesho hayo ili kuona bidhaa na malighafi zinazozalishwa mkoani humo.
Kadhalika, alisema Kongamano litakalofanyika sambamba na maonyesho hayo linatarajiwa kushirikisha watu 400, wakiwemo watendaji wa serikali, taasisi binafsi, na wawekezaji. Pia, mada mbalimbali zitawasilishwa katika kongamano hilo.
“Lengo la maonyesho haya ni kuchagiza na kuinua soko la bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa,” alisema Kunenge.
Aliongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweka juhudi kubwa za kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuhamasisha wawekezaji nchini. “Kama mkoa, tunatekeleza jitihada hizi kwa vitendo, ambapo tangu aingie madarakani, viwanda vipya 78 vimejengwa,” alibainisha Kunenge.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais (Kilimo) wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Wakulima (TCCIA), Swallah Saidi, alipongeza mkoa wa Pwani kwa kuandaa maonyesho hayo, akisema yatakuwa chachu kwa wawekezaji.
“Nawaomba wawekezaji, wafanyabiashara, na wajasiriamali kushirikiana na mkoa kwa kujitokeza kwa wingi kwenye maonyesho haya ili kufanikisha malengo yake,” alisema Swallah.