Na Bashir Yakub
Kisheria ndoa inapokuwa imefungwa kuna haki za msingi ambazo huibuka. Hizi huitwa haki za moja kwa moja (automatic right).
Huitwa haki za moja kwa moja kwakuwa hazina uhiari katika kutekelezwa kwake. Kuwapo kwa ndoa ndiko kuwapo kwake, hivyo haihitaji mtu kuziomba. Kimsingi haki hizi zipo nyingi, ambapo tutaona baadhi yake hapa, huku makala ikijikita katika haki moja ya matunzo kwa wanandoa.
- 1. Baadhi ya haki zinazoibuliwa na ndoa
(a) Haki ya tendo la ndoa. Hii ni haki ya lazima kwa wanandoa na kutokuwapo kwake kunaweza kubatilisha ndoa iwapo mmoja wa wanandoa ataamua kufanya hivyo. Ni haki ambayo huchukuliwa kama ndiyo ndoa yenyewe, hivyo kuifanya kuwa na umuhimu wa pekee.
( b ) Haki ya kutumia jina la mume. Hii ni haki aliyonayo mwanamke ambapo anaruhusiwa kutumia jina la mume wake badala ya lile la baba yake. Hata hivyo sheria haikueleza iwapo mwanamume naye anaweza kutumia jina la mke wake, au la baba wa mke wake, au la ukoo wa mke wake.
Pia si tu mwanamke ameruhusiwa kutumia jina la mume wake, isipokuwa hata lile la ukoo wa mume wake.
(c) Haki ya kutumia mali za familia kwa pamoja. Haijalishi mali hizo ni za mwanamke, mwanamume ataruhusiwa kutumia na haijalishi mali hizo ni za mwanamume, mwanamke ataruhusiwa kutumia. Isipokuwa yawe matumizi ambayo hayako kinyume cha sheria.
(d) Haki ya kutunza watoto/mtoto kama yupo. Ikiwa familia imebarikiwa kuwa na mtoto/watoto, wanandoa kwa pamoja wanawajibika kuwatunza watoto hao kila mtu kwa nafasi yake. Hii ina maana mke anawajibika zaidi kuwa mwangalizi mkuu wa kila siku wa watoto huku mume akilazimika kutoa matumizi hasa yale ya kifedha.
( e ) Haki ya kugawana mali pindi ndoa inapovunjika. Hii huhusisha mali zote ambazo huitwa mali za machumo ya pamoja baina ya mke na mume.
( f ) Pia ipo haki ya kurithi na kurithiana iwapo kuna kifo cha mmoja wa wanandoa. Mke aweza kurithi mali za mume wake, halikadhalika mume. Hii huenda mpaka kwa watoto waliopatikana katika ndoa, ambapo huweza kurithi mali za baba, mama au wote wawili.
( g ) Haki ya matunzo baina ya wanandoa. Hii ndiyo itakayojadiliwa japo kwa ufupi.
2. Mume kumtunza mke
Sura ya 29 ya Sheria ya ndoa Kifungu cha 63 (a) kinasema kuwa ni wajibu wa kila mume kumtunza mke/wake zake kutokana na njia za kipato chake. Neno njia za kipato chake maana yake ni namna anavyopata kipato ndivyo atavyotakiwa kutoa matunzo kwa mke wake. Haiwi kuwa mume anapata kipato kidogo halafu alazimishwe kutoa matunzo makubwa. Ushahidi wa namna anavyopata kipato chake ndio utakaoainisha kiasi cha matunzo kwa mke wake.
Aidha, kwa mujibu wa kifungu hicho, matunzo yanayoongelewa hapa yanahusisha makazi, mavazi, chakula na huduma nyingine kama za afya n.k. Kitu cha msingi hapa ni kuwa ni lazima kwa mume kutoa vitu hivi kwa mke wake.
3. Mke kumtunza mume
Kifungu hichohicho cha 63 ( b ) kinasema kuwa utakuwa ni wajibu wa kila mke, lakini mwenye uwezo kutoa matunzo kwa mume wake iwapo mume huyo ana ulemavu/hajiwezi jumla au sehemu ya mwili wake, kiakili au kimwili, hivyo kutokuwa na uwezo wa kuingiza kipato kutokana na hali hiyo.
Kwa kifungu hiki tunaona kuwa mke anao wajibu wa kumtunza mume wake lakini iwapo tu kwanza, ana uwezo. Pili, mume awe na tatizo ambalo kwalo hawezi kuingiza kipato na tatizo hilo liwe la kimwili au kiakili. Kumbe, basi tunaona kuwa mwanamume kumhudumia mke wake ni lazima hata mke awe mzima wa afya huku hafanyi kazi, wakati mke kumhudumia mume ni pale tu atakapokuwa ana tatizo ambalo linamfanya asiweze kufanya kazi. Lakini pia sheria imesema mke atatoa huduma iwapo ana uwezo wakati neno iwapo ana uwezo, haikuliweka kwa mume. Kwa mume kutoa ni kutoa tu.