Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeshuhudia utiaji saini wa mkataba wa kazi ya kusafisha na kukagua bomba la gesi asilia kati ya Kampuni ya Maurel and Prom Exploration Production Tanzania Limited na Kampuni ya Solutions Tag Consulting Limited.
Mkataba huo umesainiwa Machi 6, 2023 huku Meneja Mkuu wa Maurel and Prom Exploration Production Tanzania Limited, Nicolas Engel, amesema wamepata zabuni hiyo kutokana na kazi nzuri wanazozifanya katika miradi ya gesi na mafuta kwa zaidi ya miaka 10.
Pia amesema kufanya kazi na kampuni ya wazawa katika sekta ya gesi na mafuta ni mwendelezo wa azma yao ya kutaka kuacha alama katika eneo hilo.
“Tunataka kuacha alama Tanzania kwa kushirikiana na kampuni za ndani hasa zile zinazojihusisha na miradi ya gesi na mafuta na tumeanza na Kampuni ya Solutions Tag,” amesema.
Amesema mkataba huo uliosainiwa ni kielelezo cha ushirikiano mzuri kati yao na watafanya kazi zao kwa ustadi mkubwa ili kudumisha matumizi endelevu ya bomba la gesi asilia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Solutions Tag Consulting Limited, Peter Kichogo, amesema hapo awali fursa hiyo wasingeipata kwa kuwa kulikosekana wataalamu au kampuni za wazawa.
“Mafuta na gesi ni mojawapo ya sekta inayohitaji utaalamu wa hali ya juu ndiyo maana kampuni zilizopata kazi zilitoka nje ya nchi lakini sasa wazawa tunapata” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Charles Kangoye, amesema zamani fursa ya wazawa kupata kazi katika miradi ya gesi na mafuta hazikuwepo lakini kutokana na jitihada za serikali jambo hilo sasa linawezekana.
“Fursa hazikuwepo ila sasa zimekuja baada ya serikali kwa kutengeneza sheria na kanuni zinazosimamiwa na PURA.
“Tunawaomba Watanzania kuchangamkia fursa za mafuta na gesi zinapojitokeza, hivi karibuni tutaweka kwenye tovuti fursa zinazopatikana katika eneo la mafuta na gesi,” amesema.
Mkataba huo utahusisha kazi ya kusafisha na kukagua (intelligent pigging) bomba lenye urefu wa mita 800 linalotoa gesi asilia kutoka inapozalishwa katika kisima cha MB1 kilichopo Mnazi Bay (Mtwara) hadi ulipo mtambo wa kuchakata gesi wa Mnazi Bay.