Tupac alilelewa katika mazingira magumu, jamii yake ilimpatia jina la ‘Black Prince’ kwa kuwa mama yake alimpenda mtoto wake.
Tupac alikulia katika mazingira ya ‘kitemi’ kutokana na kushindwa kupata malezi bora, huku mama yake akishindwa kuwa karibu ili kumlea mtoto wake, ingawa alimpenda sana.
Alikuwa akimsumbua sana mama yake kuhusu kumjua baba yake na mama huyo hakuwa na jibu la kuweza kumridhisha zaidi ya kumwambia ipo siku atakuja.
Akiwa na umri wa miaka miwili, Tupac alipata mdogo wake wa kike aitwaye Sekyiwa, naye hakupata kumuona baba yake kwa kuwa alikamatwa kwa wizi wa gari na kuhukumiwa kifungo cha miaka 60 jela.
Afen aliwalea watoto wake chini ya uangalizi wake mwenyewe, waliishi maisha ya taabu na waliamua kuhamia sehemu nyingine iitwayo Bronx na huko familia ilitawanyika ingawa walikuwa wadogo lakini iliwalazimu waende kutafuta pesa ili waweze kuishi lakini mwisho wa siku wanakutana nyumbani na kugawana kile walichopata.
Tupac hakuwa na marafiki waliokuwa wanamkubali kama mmoja wa wanajamii, kwa kuwa waliamini ni mhuni, hivyo hakuwa na marafiki zaidi ya kuishi maisha ya peke yake.
Aliishi maisha ya shida huku akiteseka kutokana na suala la kutomjua baba yake. Kuanzia kipindi hicho, Tupac alianza kuandika mistari ya mapenzi ili kuwafariji, kwa kuwa alikuwa mpweke kiasi cha hata ndugu zake kwa upande wa mama hawakuweza kumkubali.
Alikuwa na kitabu kikubwa cha kutunzia kumbukumbu muhimu na ndani yake aliandika kwamba siku moja atakuja kuwa mtu maarufu sana duniani.
Alipenda sana kuigiza na aliona huko ndiko umaarufu wake utakakojengeka vema na aliona kwamba anaweza sana kuigiza.
Mtoto anapewa kile anachotaka, hivyo mama wa Tupac, Afeni, aliamua kumpeleka mtoto wake wa pekee wa kiume kwenye kituo maalumu kilichokuwa kinajihusisha na masuala ya sanaa huko Manhattan.
Huko aliweza kufahamika akiwa na umri wake mdogo kutokana na kupitia kwenye suala la uigizaji, hapo aliona kwamba ndugu zake wataweza kumheshimu kutokana na watu baki kuanza kumkubali katika jamii.
Akiwa huko, Tupac alianza kuupenda muziki wa rap na hapo aliachana na mistari ya mapenzi na kuangukia kwenye rap. Alifahamika kwa jina la ‘MC New York’ ndani ya New York kwa ajili ya kuweza kumudu ku-rap na watu walifikiri kwamba alikuwa mtu mmoja mkubwa sana, lakini pale alipojitokeza mbele ya watu na kujitambulisha kama MC New York kila mtu alishangaa!
Alijiunga na Shule ya Baltimore School for the Arts na kukutana na watoto wenye rangi nyeupe ambao alitokea kuwachukia, lakini baadaye aliweza kuishi nao vizuri, kwa kuwa aliamini kuwa watu weupe wote ni mashetani.
Kuanzia hapo Tupac aliona kwamba yeye ni msanii ambaye ana uwezo wa kufanya chochote anachotaka baada ya kupata mafunzo aliyoyapata shuleni hapo.